Wasiwasi watanda Tunisia | Matukio ya Kisiasa | DW | 16.08.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Wasiwasi watanda Tunisia

Hali ya usalama ikibakia kuwa tete nchini Misri, raia wa Tunisia wanahofia kwamba ghasia zinaweza zikazuka kwao. Kuna mvutano kati ya serikali ya waislamu wenye msimamo mkali na wapinzani wenye msimamo wa wastani.

Maandamano Tunisia

Maandamano Tunisia

Picha za kutisha za mauaji ya kinyama zinaonyeshwa katika televisheni kwenye migahawa ya Tunis. Picha hizo zimechukuliwa Misri, ambapo hadi sasa mamia ya watu wameuwawa kwenye mapigano kati ya maafisa wa usalama na wafuasi wa rais aliyetolewa madarakani, Mohammed Mursi. Misri ndio mada kuu inayozungumziwa Tunisia kwa sasa. "Nasikitika sana. Si tu kwa sababu sisi pia ni waarabu na waislamu, bali kwa sababu hawa wanaokufa ni binadamu," anasema mkaazi mmoja wa Tunis.

Machafuko yameuwa mamia ya watu Misri

Machafuko yameuwa mamia ya watu Misri

Wingu la huzuni limetanda kwenye mitaa ya Tunis. Si kwa sababu tu ya hali ilivyo Misri. Lakini kwa sababu Tunisia nayo iko kwenye matatizo makubwa ya kisiasa na kicuhumi. Watunisia wanahofia kuwa kisa kilichotokea kwa majirani zao Wamisri kinaweza kuwakumba pia. "Inawezakutokea hata hapa, lakini tunatumaini kuwa haitakuwa hivyo," anaeleza Mtunisia mmoja. "Watu wa Tunis ni werevu zaidi. Nina hofu kwa ajili ya watoto wangu lakini si kwangu binafsi." Kwa miezi kadhaa sasa pamekuwa na vuta ni kuvute ya kisiasa baina ya serikali inayoongozwa na waislamu wenye msimamo mkali na wapinzani wao wenye msimamo wa wastani. Awali, kuangushwa kwa rais Mursi kuliwatia wananchi wa Tunisia moyo. Lakini baada ya kuuwawa kwa Mohamed Brahmi, aliyekuwa mwanasiasa wa upande wa upinzani, matumaini hayo yalififia. Wiki hii raia wa Tunisia walikwenda barabarani kwa maelfu na kuandamana, wakiitaka serikali yao iachie madaraka.

Mkwamo waendelea

Mkuu wa chama cha Ennahda Rached Ghannouchi

Mkuu wa chama cha Ennahda Rached Ghannouchi

Lakini mkuu wa chama tawala cha Ennahda, Rached Ghannouchi, hakubaliani na matakwa ya waandamanaji. Kwa mtazamo wake, Tunisia haiwezi kuongozwa na serikali inayoundwa na wataalamu, kama wanavyotaka wapinzani. "Ennahda inaikataa serikali ya uokozi wa kitaifa. Serikali hiyo ingeitumbukiza Tunisia katika mzozo na kuharibu maamuzi ya kidemokrasia," anasema Ghannouchi. "Serikali inayoongozwa na wataalamu si jibu kwa kile ambacho Tunisia inahitaji kwa sasa."

Hata hivyo, ikilinganishwa na Misri, Tunisia bado ni tulivu. Wakati Misri imegubikwa na machafuko, kilichoko Tunisia ni mkwamo tu. Hakuna kinachoendelea. Pande zinazozozana haziko tayari kukutana katika meza ya mazungumzo na kutafuta suluhu kwa ajili ya nchi yao.

Ingawa taarifa za machafuko Misri zinawatisha wananchi wengi wa Tunisia, wanaendelea kuwa na matumaini kwamba nchi yao itafikia demokrasia ya kweli kwa njia ya amani na utulivu.

Mwandishi: Anne Allmeling

Tafsiri: Elizabeth Shoo

Mhariri: Saumu Yusuf

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com