Wasiwasi wa mionzi ya nyuklia waongezeka Japan | Masuala ya Jamii | DW | 14.03.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Masuala ya Jamii

Wasiwasi wa mionzi ya nyuklia waongezeka Japan

Waokaji nchini Japan tayari wamegundua zaidi ya maiti 2,000 za wahanga wa tetemeko la ardhi la Ijumaa, huku kitisho kipya cha kuvuja kwa miale ya atomiki baada ya miripuko kwenye vinu viwili vya nyuklia nchini humo.

Kinu cha Fukushima Dai-ichi Namba 3, baada ya mripuko

Kinu cha Fukushima Dai-ichi Namba 3, baada ya mripuko

Juhudi za uokoaji zinaendelea, ambapo miili takribani 1000 imepatikana katika mji wa Minamisanriku, mji ambao umevurugwa vibaya na tetemeko hilo lililoambatana na Tsunami.

Jeshi la Polisi nchini kwa upande wa mji wa Miyagi linasema idadi ya watu waliopoteza maisha kutokana na balaa hilo inaweza kuzidi 10,000.

Katika tukio lingine, Serikali ya Japan imesema watu 11 wamejeruhiwa, mmoja akiwa hali mbaya sana, baada ya kutokea mripuko uliosababishwa na tetemeko hilo katika kinu kimoja cha nyuklia nchini humo.

Miundombinu iliyoharibiwa na tetemeko na Tsunami nchini Japan

Miundombinu iliyoharibiwa na tetemeko na Tsunami nchini Japan

Katibu Kiongozi wa Serikali ya Japan, Yukio Edano, amewataja wanajeshi wanne na wafanyakazi saba wa kinu hicho cha Fukushima Dai-ich kilichoripuka mapema leo, kuwa miongoni mwa wahanga wa ajali hiyo.

Awali hali kama hiyo iliashiria kujitokeza katika kinu kingine, ambacho kilipoteza uwezo wa kujipoza na kuonesha kila dalili ya kuweza kuripuka.

Edano amesema majeruhi mmoja hali yake ni mbaya sana, na amepoteza kabisa fahamu, huku askari wanne ambao hawakujeruhiwa sana hivi sasa wamerejea katika vituo vyao vya kazi.

Hata hivyo, katibu mkuu huyo kiongozi amezugumzia kitisho cha kuvuja miyale ya nyuklia.

"Siwezi kukataa kwamba kuna uwezekano wa mabadiliko ya kimaumbeile ndani ya kinu chenyewe cha kuhifadhia nyuklia yaliyotokana na joto kali. Na kuna kipindi njia zenyewe hazikuwa katika mfumo wa kupozwa na maji." Amesema Edano.

Wanasayansi katika maeneo tofauti duniani wanaanza kufuatilia kwa karibu athari zinazoweza kutokea kutokana na kuripuka kwa vinu hivyo vya nyuklia.

"Kwa sasa inaonekana baada ya miripuko hii hakuna miyale ya nyuklia iliyovuja katika eneo lililokaribu na kinu cha nyuklia, kwa kuwa hakuna thibitisho la la kuvuja na miyale hio na kwamba miripuko imeharibu tu jengo la kiwanda hicho. Hivyo basi hizo ni habari njema." Amesema msemaji wa Shirika la Ujenzi na Usalama wa Vinu vya Nyuklia la Ujerumani (GRS), Sven Dokter.

Tayari wanauchumi ndani na nje ya Japan wameendelea kutathimini hali ilivyo na athari zitakazotokana na balaa hilo kwa kusema uchumi utatetereka kwa ujumla.

Kampuni ya kutengeneza magari ya Honda tayari imetengaza kusitisha uzalishaji mpaka Machi 20 kutokana na tetemeko hilo la ardhi lililotokea Kusini Mashariki mwa Japan.

Kampuni hiyo imefunga karakana zake zote za kutengeneza magari nchini humo na kuacha kiwanda cha kutengeneza pikipiki kilichopo Kisiwa cha Kyushu.

Kutokana na hali hizo zaa athari za tetemeko hilo kubwa, nchi zaidi ya sabini zimeahidi kutoa misaada ya kila aina kwa Wajapani.

Mwandishi Sudi Mnette/RTRE
Mhariri: Miraji Othman

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com