Wasiiache Somalia | Matukio ya Kisiasa | DW | 16.06.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Wasiiache Somalia

Somalia haistahili huadhibiwa kutokana na makosa ya viongozi wake wa zamani. Kulingana na mjumbe maalum wa Umoja wa mataifa nchini Somalia Ahmedou Ould Abdallah jumuiya ya kimataifa kupaswa kuisaidia Somalia

Gari ya kijeshi mjini Mogadishu

Gari ya kijeshi mjini Mogadishu

Ahmedou Ould Abdallah ambae ameambatana na Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-Moon katika ziara yake nchini Saudi Arabia, anaamini kuwa mkataba wa kusimamisha mapigano uliofikiwa tarehe 9 mwezi huu mjini Djibuti, licha ya kupingwa na mmoja wa viongozi wa makundi ya kiislamu, unaweza kukomesha kipindi cha miaka 17 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe yaani tangu kuanguka utawala wa rais Siad Barre mwaka 1991.

"Makundi yote muhimu ya kisomali yalisaini mkataba huo isipokuwa tu baadhi ya watu wanaozingatiwa na Umoja wa mataifa na Marekani kuwa ni magaidi", amesema Ould Abdallah. Mkataba huo ulisainiwa na serikali ya Somalia na muungano wa makundi ya upinzani yanayojitaja kuwa ni kwa ajili ya ukombozi mpya wa Somalia na mengi ya hayo yakiwa ya kiislamu yenye makao yake nchini Eritrea. Aliyetangaza upinzani wake dhidi ya mkataba huo wa mjini Djibuti, ni Sheikh Hassan Dahir Aweys ambae anasakwa na Marekani akituhumiwa kushirikiana na kundi la kigaidi la Al-Qaida la Ossama bin Laden.

Kwa maoni ya Ahmedou Ould Abdallah, wakati umewadia jumuiya ya kimataifa kwa jumla na hususan Ulaya, Marekani, jumuiya ya kiarabu, Japan na Ashia kuisaidia Somalia kusimamisha mapigano. Ahmedou Ould Abdallah, alizungumza na mfalme Abdallah wa Saudi Arabia kuhusu mpango wa kusainiwa mkataba rasmi mjini Maka katika tarehe itakayopangwa kwa makubaliano na pande husika.

"Kwa muda wa kutosha sasa, nchi za magharibi hutaja kuwa haziwezi kuisaidia Somalia kwani wenyewe wameshindwa kufikia mwafaka, sasa nchi hizo hazina hoja tena", amezidi kusema Ahmedou Ould Abdallah ambae amezitolea mwito nchi hizo za magharibi kutoa nyenzo zinazohitajika kuunga mkono mkataba huo wa mjini Djibuti. Mkataba huo, umependekeza pamoja na mambo mengine undwaji wa kamati za usalama kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa mkataba wa kusimamisha mapigano. Unapendekeza pia kuwepo kamati ya kuimarisha ushirikiano, sheria na maridhiano ya kitaifa.

Kulingana na mjumbe huyo wa Umoja wa mataifa nchini Somalia, Baraza la usalama la Umoja wa mataifa lingetoa idhini sasa hivi ya kupelekwa kikosi cha kijeshi cha kimataifa kudhaminia amani ambacho kitarahisisha pia kuondoka kwa majeshi ya kigeni yalioko Somalia. Kwa hakika mkataba huo wa Djibuti, umepanga kuuomba Umoja wa mataifa uwatume nchini Somalia wanajeshi wa kimataifa wa kulinda amani hadi kufikia miezi minne baada ya kusainiawa mkataba kamili. Wanajeshi hao watatoka katika nchi rafiki isipokuwa nchi jirani wakimaanisha Ethiopia. Umoja wa Afrika ulipeleka wanajeshi kiasi ya 2600 nchini Somalia, ikiwa ni kidogo ya idadi iliokuwa imepangwa ya wanajeshi 8000 na hadi sasa wameshindwa kukomesha machafuko.

Kulingana na Umoja wa mataifa, kwa uchache watu miliopni 2,6 nchini Somalia wanakabiliwa na uhaba wa chakula na wanahitaji misaada ya dharura kuepusha janga kubwa la kibinaadamu.Inakisiwa kuwa tangu kuanza vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Somalia mwaka 1991, watu wapatao laki 3 wameshauwa na majaribio kiasi ya 10 ya kurejesha amani yameshindwa.

 • Tarehe 16.06.2008
 • Mwandishi Nijimbere, Gregoire
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EKG9
 • Tarehe 16.06.2008
 • Mwandishi Nijimbere, Gregoire
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EKG9
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com