Wasifu wa marehemu Benjamin Mkapa | Matukio ya Afrika | DW | 24.07.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Wasifu wa marehemu Benjamin Mkapa

Mkapa ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 81. Alikuwa rais wa awamu ya tatu nchini Tanzania kati ya mwaka 1995-2005. Kifo chake ni pigo si kwa Tanzania pekee bali Afrika kufuatia michango yake katika siasa za kanda hiyo.

Benjamin William Mkapa, rais wa tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amefariki dunia usiku wa kuamkia Ijumaa akiwa hospitalini jijini Dar es Salaam, akiwa na umri miaka 81, akiwa ameshalitumikia taifa lake kwenye ngazi mbalimbali za uongozi.

Mzaliwa huyu wa Masasi, kusini mwa Tanzania wakati huo mwaka 1938 ikiitwa Tanganyika, alitokea familia ya kimasikini kama walivyo watu wengine kadhaa waliokuja kushika nafasi kubwa maishani mwao.

Akitambuliwa kama msomi wa daraja yake na fasaha wa kuzungumza - iwe Kiswahili ama Kiingereza, Mkapa alianza safari yake ya kielimu kwao, akihudhuria skuli ya wamishionari wa Kikatoliki na kisha kupata cheti chake kutoka Chuo cha Mtakatifu Francis mwaka 1956, kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu maarufu wakati huo kwa Afrika Mashariki nzima, Makerere cha Uganda, ambako kasomea shahada ya kwanza ya masomo ya Sanaa.

Masomo ya Mkapa

Wakati Tanganyika inapata uhuru wake tarehe 9 Disemba 1961, Mkapa alikuwa bado anaendelea na masomo ya juu, lakini tayari alikuwa na mawazo makubwa ya ukombozi wa Afrika kwa sababu kwa wakati huo, Chuo Kikuu cha Makerere lilikuwa jungu walilopikwa takribani vijana wote waliokuja baadaye kujiunga na siasa za ukombozi kwenye mataifa yao.

Mkapa alikuwa mwanachama wa chama cha ukombozi wa Tanganyika, TANU, kilichoongozwa na mwasisi wa taifa hilo na shujaa wake, Mwalimu Julius Nyerere.

Benjamin Mkapa (kulia) akiwa ameketi pamoja na Rais John Magufuli (kushoto) Picha ya maktaba

Benjamin Mkapa (kulia) akiwa ameketi pamoja na Rais John Magufuli (kushoto) Picha ya maktaba

Lakini Mkapa hakuanza safari yake ya maisha kama mwanasiasa, bali kama msomi. Ndiyo maana hata aliporejea nyumbani mwaka 1962 kutokea masomoni Makerere, alishika nafasi ya utendaji kama afisa tawala wa wilaya ya Dodoma, makao makuu ya sasa ya Tanzania, nafasi aliyodumu nayo kwa mwaka mmoja tu kabla ya kuhamishiwa wizara ya mambo ya kigeni kama afisa wa huduma za nje, ambako nako kwa sababu ya kiu yake ya kusoma alipatumia kupata fursa ya kwenda Marekani kusomea shahada ya uzamili kwenye masuala ya siasa za kimataifa katika Chuo Kikuu cha Columbia.

Mkapa kama Mwandishi wa Habari

Hata aliporejea tena masomoni kutokea Marekani, Mkapa aliingia kwenye uandishi wa habari kwa miaka kadhaa, ambapo mwaka 1966 aliteuliwa kuwa mhariri msimamizi wa magazeti ya Uhuru na Mzalendo na baadaye matoleo ya Kiingereza ya Daily News na Sunday News, yote midomo ya serikali chini ya utawala wa Mwalimu Julius Nyerere, ambaye alimteuwa kuwa katibu wake kabla ya kumpa tena jukumu la kuwa mwanzilishi na mkurugenzi mkuu wa Shirika la Habari, SHIHATA.

Ni kuanzia hapo ndipo safari yake rasmi kisiasa ikawa imeanza, kwani alikuwa na jukumu la kuisimamia na kuisambaza siasa ya chama chake na misimamo ya serikali  kupitia tasnia ya habari akiongoza midomo mikuu ya utawala wa Mwalimu Nyerere.

Safari ya Mkapa Kisiasa

Kuanzia mwaka 1976 alianza kuhudumu kwenye nafasi kadhaa za kisiasa ikiwemo ya ubalozi wa nchi yake kwa Nigeria, waziri kwenye wizara za mambo ya kigeni kwa vipindi viwili tafauti, wizara ya habari na utamaduni, sayansi na teknolojia na elimu ya juu, na hapana shaka mbunge wa jimbo la Nanyumbu kwa nyakati tafauti kupitia chama chake cha Mapinduzi, ambacho kiliundwa mwaka 1977 kwa muungano wa TANU ya Tanganyika na ASP ya Zanzibar. Ubunge wa Nanyumbu alikuwa nao hadi alipoteuliwa kuwania urais wa Tanzania kwenye uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995, ambao aliibuka mshindi na kuongoza kwa mihula miwili ya miaka mitano mitano.

Benjamin Mkapa (kushoto) akiamkuana na mwanasiasa Edward Lowassa (kulia). Picha ya maktaba

Benjamin Mkapa (kushoto) akiamkuana na mwanasiasa Edward Lowassa (kulia). Picha ya maktaba

Utawala wa Mkapa unakumbukwa na wengi kwa kauli mbiu yake ya ukweli na uwazi, aliyoitumia kuombea kura akinadiwa majukwaani na shujaa wake, Mwalimu Nyerere, katika jitihada za kupambana na ufisadi na uzembe serikalini. Yeye ndiye muasisi wa Kamisheni ya Ufisadi, maarufu kama Tume ya Warioba, ambayo ilipelekea kuundwa kwa chombo cha kisheria kupambana na gonjwa hilo thakili kwenye tawala nyingi za Afrika kwa jina TAKUKURU, Taasisi ya Kupambana na Kuzuwia Rushwa.

Sera ya Ubinafsishaji mashirika ya umma

Atakumbukwa pia kwa sera yake ya ubinafsishaji mashirika ya umma, uwekezaji wa kigeni na ukuzaji wa uchumi, ambayo kwa wengi haikwenda kama ilivyotazamiwa na badala ya kuleta nafuu ya kimaisha, ikawa chanzo cha ukiukwaji mkubwa wa haki za wafanyakazi na ufisadi. Wakati anaondoka madarakani mwaka 2005, serikali yake ilikuwa inatuhumiwa kwa matumizi mabaya ya fedha za umma, ikiwemo ndege binafsi ya rais iliyogharimu zaidi ya paundi milioni 15, na pia kashfa ya rada ya kijeshi iliyokula paundi milioni 30 za Kiingereza.

Lakini kama mwenyewe alivyokiri kwenye kitabu chake alichokizinduwa mwaka jana, doa kubwa zaidi kwake lilikuwa ni mauaji ya Januari 2001 visiwani Zanzibar, ambayo yalifanywa na vyombo vya dola, yeye akiwa amiri jeshi mkuu wake. Kwake, hii ni alama mbaya anayokwenda nayo kaburini.

Mhariri: Gakuba, Daniel