1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wasifu wa Kansela Angela Merkel

Saumu Ramadhani Yusuf10 Septemba 2013

Miongoni mwa sifa kuu za Kansela Angela Merkel (CDU) ni kutokuwa kwake mtu wa papara katika kutoa maamuzi hasa katika masuala tete na mara zote hukaa kimya na mwishowe kauli yake itaungwa mkono na walio wengi.

https://p.dw.com/p/19d27
Picha: Reuters

Mtu hawezi kusema kwamba Angela Merkel ametawala katika wakati wenye utulivu. Mwezi Juni alipokwenda St .Petersberg Urusi nusra akabiliwe na mashambulizi ya kisiasa.

Rais wa Urusi Vladmir Putin alitaka kuifuta ratiba ya awali ya kuhudhuria maonyesho ya Sanamu la Shaba katika makumbusho ya St. Petersburg pamoja na Merkel na kutaka Merkel asihutubie katika shughuli hiyo.

Lakini Merkel alitishia kukatiza ziara yake nchini Urusi hatua iliyomfanya Putin kuubadili msimamo wake. Hatua hiyo ilikuwa ni ushindi wa Merkel uliodhihirisha uwezo wake katika mchezo wa bahati nasibu. Bila ya shaka, kilichosababisha mafanikio hayo ni ile sera yake ya kukaa kimya, kutazama na kuchukuwa hatua dakika za mwisho.

Dosari ya NSA

Lakini sera hiyo imetowa matokeo tofauti lilipokuja sakata la Shirika la Ujasusi la Marekani (NSA) likitajwa kunasa kwa siri mawasiliano ya wananchi wa Ulaya, ikiwemo Ujerumani. Sakata hilo lilitia doa sera ya nje na ya ndani ya Kansela Merkel.

Kansela Angela Merkel katika picha hii ya tarehe 25 Julai 2012 akiwasili kwenye Tamasha la Bayreuth.
Kansela Angela Merkel katika picha hii ya tarehe 25 Julai 2012 akiwasili kwenye Tamasha la Bayreuth.Picha: picture-alliance/dpa

Kiroja cha mambo ni kwamba Marekani ni rafiki mkubwa wa Ujerumani, sasa ni vipi Marekani inawachunguza wandani wake na ilhali kila mmoja ana siri zake? Juu ya hilo, ni vipi mashirika ya kijasusi ya Ujerumani yahusike katika sakata hili kwa kutoa msaada mkubwa kwa NSA?

Merkel alikaa kimya muda wote hadi hapo baadaye alipoamua kutoa sauti yake. Mwanahistoria Edgar Wolfrum anasema Merkel ni "mtu anayepima kwa umakini mkubwa masuala tete kabla ya kuyatolea kauli."

Mwanahistoria huyo anasema Merkel sio mtu wa papara katika kutoa maamuzi hasa katika masuala tete na mara zote hukaa kimya na mwishowe kauli yake itaungwa mkono na walio wengi. Ana kipaji na, kwa hivyo, katika siasa anachukuwa tahadhari na wakati huohuo kutowa onyo.

Mtatuzi wa migogoro


Tangu mwaka 2008 Kansela Angela Merkel amekuwa akiangaliwa kimsingi kama kiongozi mzuri katika kukabiliana na migogoro. Katika suala la Ugiriki, alisaidia kuikowa sarafu ya euro, lakini kwa Wagiriki wenyewe Merkel hana nafasi ya kuupitisha uso wake.

Ziara ya Kansela Merkel nchini Kenya mwezi Julai 2011.
Ziara ya Kansela Merkel nchini Kenya mwezi Julai 2011.Picha: picture-alliance/dpa

Huko hakuna anayetaka kuzungumza kuhusu Merkel na, kwa hakika, sio tu Ugiriki lakini katika eneo zima la Ulaya ya Kusini.

Ingawa ukweli wa mambo unabaki kuwa Merkel ameibuka kuwa shujaa kimataifa katika suala hilo la kuikowa sarafau ya euro.

Kwa hakika mtu atalazimika kuijuwa mizizi ya Merkel ndipo atakapoweza kumuelewa yeye kama alivyo. Haijapata kutokea katika historia ya Ujerumani baada ya mwaka 1945 kutokea mwanasiasa aliyewekewa matumani kidogo kama ilivyotokea kwa binti huyo wa mchungaji kutoka Mashariki.

Mara ya kwanza alipoonekana katika televisheni alikuwa hana mvuto wowote. Lakini kilichokuwa dhahiri ni kwamba Merkel alikidhibiti chama na serikali yake na yote yalitokana na sababu zake.

Sababu zenyewe ni hizi

Ni mtu wa kuchukuwa tahadhari anapokabiliana na wengine.kwamfano wakati wa utoto wake alikuwa asiyejalishwa na wafanyakazi vijana pamoja na jimbo lake lililokuwa masikini. Merkel hakuwa na mpinzani katika iliyokuwa Ujerumani Mashariki (GDR).

Kansela Merkel na baadhi ya wajumbe wa baraza la mawaziri.
Kansela Merkel na baadhi ya wajumbe wa baraza la mawaziri.Picha: picture-alliance/dpa

Angela Merkel ni msikivu, na tofauti na ilivyokuwa kwa vijana wenzake wakati huo alikuwa na uwezo mkubwa katika kuzungumza. Kurt Lauk rafiki yake katika chama anasema anapata tabu katika kumuelewa kiongozi wake wa chama.

Anasema Merkel anasikiliza sana, anaridhia, na ni muelewa na siku zote maamuzi yake ya mwisho sio ya moja kwa moja, yaani hatowi jawabu la moja kwa moja.

Merkel aliingia katika siasa na kuwa kama msemaji wa waziri mkuu wa mwisho katika iliyokuwa Ujerumani Mashariki, Lothar de Maiziere, wakati huo akiwa na umri wa miaka 35. Ni mchapa kazi katika chama chama cha CDU.

Chini ya Kansela Helmut Kohl mwaka 1994 alikuwa waziri wa mazingira na usalama wa nyuklia, wizara muhimu kabisa kwa mtu anayeshikilia shahada ya uzamifu katika fizikia.

Baada ya kushindwa Helmut Kohl katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1998, chama cha CDU kilipata mshtuko mkubwa lakini sio kwa Merkel, ambaye aliitumia nafasi yake barabara na mwaka 2000 akachaguliwa kuwa mwenyekiti wa chama hicho.

Mwaka 2005 katika uchaguzi mkuu akatokeza kuwa mgombea mkuu wa chama hicho wa Ukansela. Merkel alipata ushindi lakini ilimbidi kuunda serikali ya pamoja na chama cha SPD. Merkel anakiongoza chama hicho cha CDU kwa mwaka wa 13 sasa na amekuwa kansela kwa miaka 8.

Mwandishi: Völker Wagener
Tafsiri: Saumu Yusuf
Mhariri: Mohammed Khelef