1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Washukiwa watatu washitakiwa kwa ugaidi Brussels

Mohammed Khelef28 Machi 2016

Waendesha mashitaka nchini Ubelgiji wamewafungulia mashitaka ya ugaidi watuhumiwa watatu, huku polisi barani Ulaya wakiendelea na msako kufuatilia mashambulizi ya hapo Jumanne mjini Brussels kuuwa watu 35.

https://p.dw.com/p/1IKm1
Mtoto akiweka shada la maua katika eneo la waombolezaji mjini Brussels.
Mtoto akiweka shada la maua katika eneo la waombolezaji mjini Brussels.Picha: DW/B. Riegert

Kituo cha Migogoro cha Ubelgiji hivi leo kimetoa idadi mpya ya vifo vilivyotokana na miripuko ya mabomu katika kituo cha treni na uwanja wa ndege mjini Brussels, kikisema ni 35 wakiwemo washambuliaji watatu.

Ripoti za awali za kituo hicho zilikuwa zikisema jumla ya waliouawa walikuwa 31 pamoja na washambuliaji wenyewe, na 340 kutoka mataifa 19 kujeruhiwa, ambapo 101 bado wako hospitali na 62 kati yao wakiwa kwenye vyumba vya wagonjwa mahututi.

Sasa kinasema kimewatambua wahanga 28 wa mashambulizi hayo ya kujitoa muhanga, ambapo 15 waliuawa kwenye uwanja wa ndege, sita kati yao wakiwa raia wa Ubelgiji na waliobakia wa kigeni.

Katika wahanga 13 wa mashambulizi kwenye kituo cha treni, 10 walikuwa raia wa Ubelgiji, na watatu wa kigeni.

Miongoni mwa wageni waliouawa ni kutokea Uingereza, Italia, Uchina, Uholanzi, Ujerumani, Sweden na Marekani. Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imethibitisha vifo vya raia wengine wawili wa nchi hiyo, na hivyo kuifanya idadi ya Wamarekani waliouawa kwenye mashambulizi hao kufikia wanne.

Watatu wafunguliwa mashitaka

Katika hatua nyengine, waendesha mashitaka mjini Brussels wanasema wamewafungulia mashitaka watu wengine watatu kwa kujihusisha na kundi moja la kigaidi, sambamba na kumuachia mtu wa nne kati ya waliokuwa wanawashikilia.

Sehemu ya maombolezo mjini Brussels.
Sehemu ya maombolezo mjini Brussels.Picha: DW/B. Riegert

Taarifa ya ofisi ya mwendesha mashitaka mkuu inawataja watatu hao walioshitakiwa kuwa ni Yassine A., Mohamed B., na Aboubaker O.

Usiku wa kuamkia leo, polisi waliyavamia maeneo 13 mjini Brussels, ambapo waliwahoji watu tisa na kuwashikilia wanne kwa mahojiano zaidi.

Nako nchini Uholanzi, polisi walimkamata raia mmoja wa Ufaransa katika mji wa Rotterdam, baada ya kuombwa na wenzao wa Ufaransa. Inadaiwa mtu huyo alipanga mashambulizi nchini Ufaransa akiwa pamoja na Reda Kriket, mtuhumiwa mwengine wa ugaidi ambaye alitiwa nguvuni mjini Paris siku ya Alhamis.

Wakati huo huo, uwanja wa ndege wa Brussels unaanza hivi leo majaribio ya uwezo wake kwa kufungua sehemu moja ya huduma kwa abiria, ingawa maafisa wanasema ingali mapema kuamua muda hasa ambapo huduma zitaanza rasmi.

Mshambuliaji wa kujitoa muhanga aliiharibu vibaya sehemu kubwa ya eneo la kuondokea wageni kwenye uwanja wa ndege huo tarehe 22 mwezi huu.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/AP/Reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga