Washukiwa wa ujambazi wauawa Mombasa | Matukio ya Afrika | DW | 01.10.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Washukiwa wa ujambazi wauawa Mombasa

Washukiwa watatu wa ujambazi wameuwawa kwa kupigwa risasi katika makabiliano na maafisa wa ulinzi katika eneo bunge la Likoni, kaunti ya Mombasa

Tukio hilo limetokea karibu na bustani la Mama Ngina ambapo rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, anatarajiwa kwa mara ya kwanza mwezi huu kuongoza sherehe za kitaifa akiwa mjini Mombasa.

Kikosi kilichojumuisha maafisa wa usalama wa idara mbalimbali za ulinzi kimewavizia washukiwa hao katika msako uliokuwa unaendeshwa toka jana usiku. Huku akikwepa kuthibitisha iwapo washukiwa hao ni magaidi, kaimu mratibu wa idara ya upepelezi wa jinai eneo la Pwani ya Kenya Paul Letin amesema washukiwa hao walikuwa wanapanga njama za kufanya mashambulizi dhidi ya wananchi.

Letin amesema msako huo unaendelea ili kuwanasa wengine waliotoroka katika msako mwengine tofauti uliofanyika katika mtaa wa Bomani. Mkuu wa kitengo cha upepelezi katika kaunti ndogo ya Likoni Francis Kazungu amesema katika msako huo wameweza kunasa risasi, bunduki na silaha mbali mbali ikiwemo mapanga.

Watetezi wa haki za binadamu walaani mauaji ya watuhumiwa wa ujambazi

Mkuu wa kitengo cha dharura kutoka shirika la utetezi wa haki za binadamu la Muhuri, Francis Auma, ameshutumu kitendo hicho kwa kueleza kwamba idara ya ulinzi imekithiri katika kuwaua washukiwa eneo la Likoni badala ya kuwakamata na kuwafungulia mashtaka.

Mauaji hayo yanajiri wiki moja baada ya mshukiwa mwengine wauhalifu kupigwa risasi na maafisa wa polisi. Mtaa wa Majengo Mapya na bustani ya Mamangina ni kilomita zisizozidi mbili na sehemu hizo zinatenganishwa na mkondo mwembamba wa bahari unaoingia bandarini Mombasa.

Katika hatua nyingine, Rais Uhuru Kenyatta ataongoza sherehe za mashujaa tarehe ishirini mwezi huu katika bustani hiyo ambayo kwa sasa inaendelea kufanyiwa marekabisho chini ya ulinzi mkali wa jeshi la wanamaji na vikosi vingine vya ulinzi. Sherehe ya Mashujaa inaadhimishwa kila mwaka kuwakumbuka waliopigania uhuru wa taifa la Kenya. 

 

 

DW inapendekeza