1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WASHINGTON : Baraza la Senate mikononi mwa Demokrat

10 Novemba 2006
https://p.dw.com/p/CCuJ

Mbunge wa chama cha Republican wa jimbo la Virginia George Allen amekiri kushindwa na mpinzani wake wa chama cha Demokrat Jim Webb katika uchaguzi wa bunge wa kipindi cha kati uliofanyika nchini Marekani hapo Jumanne.

Kwa matokeo hayo chama cha Demokrat kimefanikiwa kunyakuwa kiti cha mwisho ilichokuwa ikihitaji kuweza kufikisha viti 51 ambao ni wingi wa viti katika baraza la Senate kulidhibiti baraza hilo wakati bunge la Marekani litakapoanza kikao chake hapo mwezi wa Januari mwakani.

Udhibiti wa baraza la Senate na kamati zake utakipa chama cha Demokrat haki ya kuitisha vikao na kuidhinisha nyadhifa zinazotolewa na Rais ikiwa ni pamoja na zile za Mahkama Kuu. Ushindi wa Demokrat katika uchaguzi huo wa bunge la Marekani unawapa fursa mpya za kusaidia kuunda sera za taifa na kubeba mzigo wa kutimiza matarajio ya wapiga kura.

Akizungumza nje ya jengo la bunge la Marekani mjini Washington Seneta Harry Reid wa chama cha Demokrat ambaye anatarajiwa kuwa kiongozi wa baraza hilo mwakani amesema wakati wa mabadiliko umewadia kwa nchi hiyo kutamka kwa sauti kubwa ilio dhahiri.

Ushindi wa baraza la Senate kwa chama hicho cha Demokrat unatanguliwa na ule wa baraza la wawakilishi ililolitwaa na mapema.

Mada kuu ya uchaguzi huo ilikuwa ni vita vya Iraq.

Rais George W. Bush wa Marekani amesema hapo jana yuko tayari kupokea ushauri kutoka kwa wabumge wa chama cha Demokrat juu ya namna ya kushinda vita nchini Iraq.Hata hivyo amesema hayuko tayari kusalimu amri kutokana na lengo lake la kupata ushindi nchini Iraq ambao umeufafanuwa kuwa ni Iraq ambayo itaweza kujihami na kujiendesha yenyewe.

Rais huyo wa Marekani ameendelea kukataa wito wa kutangaza ratiba ya kuvirudisha nyumbani vikosi vya Marekani.