1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Washindi wa nishani ya Nobel kuanza kutangazwa leo

Liongo, Aboubakary Jumaa6 Oktoba 2008

Mchakato wa kuwapata washindi wa nishani ya Nobel katika sekta mbalimbali unaanza leo kwa kutangazwa mshindi wa tuzo hiyo kwa upande wa madawa.

https://p.dw.com/p/FUcF
Mshindi wa nishani ya Nobel upande wa fasihi, Doris Lessing mwenye umri wa miaka 88 mara baada ya kutangazwa mshindi mwakaPicha: AP

Mchakato huo unatarajiwa kumalizika tarehe 13 mwezi huu pale atakapotangazwa mshindi wa nishani hiyo ya Nobel kwa upande wa uchumi.Maeneo mengine yatakayotolewa nishani hiyo ni ya Amani, Mazingira, Fasihi na Sayansi.


Kamati za uteuzi wa washindi wa tuzo hiyo zimefanyakazi kubwa kuhakikisha kuwa hakuna taarifa zilizovuja juu ya majina ya washindi.Hata hivyo wafutualiaji wa nishani hiyo ya Nobel wamekuwa wakichambua wawaniaji


Wanasayansi wawili wa kike ambao tafiti zao katika maradhi ya kansa zimekuwa na mafanikio makubwa wanapewa nafasi kushinda tuzo hiyo yenye hadhi kubwa duniani.


Wanasayansi hao  Elizabeth Blackburn na Carol Greider wote kutoka Marekani tayari wamekwishashinda tuzo kadhaa kutokana na utafiti wao huo.


Toka kuanzishwa kwa tuzo hiyo ya Nobel upande wa madawa, mnamo mwaka 1901, ni wanawake saba tu waliyowahi kushinda, ambapo mara ya mwisho ilikuwa mwaka 2004 pale mwanasayansi wa kimarekani  Linda Buck aliposhinda lakini kwa kugawana tuzo hiyo na mwanasayansi wa kiume Richard Axel.


Kwa upande nishani ya amani,mwanaharakati wa haki za binaadamu wa China Hu Jia pamoja na mwanaharakati mwengine wa haki za binaadamu ambaye ni mwanasheria Lidiya Yusupova kutoka Chechenya wanapewa nafasi kubwa kuteuliwa kuwania tuzo hiyo.


Uteuzi wa mshindi wa tuzo hiyo ya Nobel upande amani atatangazwa Ijumaa ijayo  mjini Oslo Norway siku ambayo ni maadhimisho ya miaka 60 Umoja wa Mataifa ulipopitisha azmio la haki za binaadamu.


Pia yanatajwa majina kama  vile Ingrid Betancourt Mcolombia mwenye asili ya Ufaransa ambaye alikuwa mateka kwa miaka  sita unusu katika mikono ya wapiganaji wa kundi la FARC huko Colombia kuweza kushinda tuzo hiyo


Wengine wanaotajwa kuwa huenda wakashinda ni mwanaharakati wa demokrasia nchini Vietnam mtawa wa dini ya Kibuddha Thich Quang Do, pamoja na mpinzani wa utawala wa Cuba Oswaldo Paya.


Kwa upande wa  Fasihi, ambapo mshindi wake atatangazwa Alhamisi ijayo, mwanafasihi wa kifaransa Jean-Marie Gustave Le Clezio anapewa nafasi kubwa ya kushinda.Mwaka jana mwanafasihi wa kiingereza Doris Lessing ndiye aliyeshinda.


Tuzo za Nobel zilianzishwa mwaka 1901 na tajiri mmoja aliyekuwa na viwanda raia wa Sweeden Alfred Nobel.


Alfred Nobel aliandika wosia mnamo mwaka 1895 mwaka mmoja kabla ya kifo chake kuwa mapato ya mali yake kila mwaka yagawiwe kwa njia ya tuzo kwa wale ambao wamefanya mambo makubwa ya kujitolea kwa ajili ya wanaadamu.


Mshindi wa tuzo hiyo ya Nobel mwaka huu atapata kiasi cha euro millioni 1 na laki mbili ambazo iwapo washindi ni wa wawili au watatu basi hugawana.


Afrika ilishuhudia Profesa Wangari Maathai kutoka Kenya akishinda tuzo hiyo ya Nobel kwa upande wa mazingira mwaka 2004 na kuwa mwanamke pekee kutoka Afrika kushinda tuzo hiyo.