Wasemavyo wahariri wa Ujerumani Jumanne hii | Magazetini | DW | 11.02.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Wasemavyo wahariri wa Ujerumani Jumanne hii

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wamezungumzia juu ya kashfa ya kodi inayomkabili Meya Wowereit wa mji wa Berlin, ushiriki zaidi wa Ujerumani nchini Somalia, na mwaka mmoja tangu kujiuzulu kwa papa Benedikt wa 16.

Wahariri wamezungumzia mwaka mmoja tangu alipojiuzulu Papa Benedict XVI.

Wahariri wamezungumzia mwaka mmoja tangu alipojiuzulu Papa Benedict XVI.

Mhariri wa gazeti la Nordwest anazungumzia sakata la meya wa jiji la Berlin na mwenyekiti wa bodi ya uwanja wa kimataifa wa ndege wa mji huo, Klaus Wowereit, kufunika uhalifu wa katibu mkuu anaedaiwa kukwepaji kodi. Mhariri huyo anasema:

Klaus Wowereit alilaazimika kujiuzulu uenyekiti wa bodi hiyo huko nyuma kutokana na ucheleweshaji wa ujenzi wa uwanja huo uliogharimu mamilioni ya fedha za walipakodi. Lakini alirejea katika nafasi hiyo baada ya miezi michache tu. Na leo analaumiwa kwa sababu ya kumfichia makosa yake katibu mkuu aliyekwepa kodi, lakini pia hakuna madhara kwa sababu hakuna mtu anaweza kuziba nafasi yake. Si wanachama wa SPD wala washirika wao katika serikali, CDU/CSU, walio na mtu mwenye sifa za kuchukuwa kazi hiyo. Badala yake sakata hilo limetangazwa kuisha. Hii ni aibu, kwa Wowereit, kwa vyama husika na kwa heshima ya demokrasia.

Mhariri wa gazeti la Märkische Oderzeitung ameandika juu wazo la serikali ya shirikisho la Ujerumani kupeleka wanajeshi nchini Somalia. Mhariri huyo anasema:

Hali ya usalama nchini Somalia imebadilika katika namna ambavyo Ujerumani haina budi kujitosa nchini humo, hasa kwa kuzingatia mahitaji yake yenyewe ya usalama. Hii ni kwa sababu migogoro inayozidi kukuwa mashariki mwa Asia, Afrika na Mashariki ya Kati, inazidi kuihusu Ulaya na Ujerumani pia, na kwa hivyo migogoro hiyo haiwezi kupuuzwa. Katika hili, sera ya Ujerumani ya kujizuwia inapaswa kujadiliwa upya, kama walivyopendekeza hivi karibuni, Rais Joachim Gauck, Waziri wa Mambo ya Kigeni Frank Walter Steinmeier, na hata Waziri wa Ulinzi Ursula von der Leyen.

Naye mhariri wa gazeti la Passauer Neue Presse ameandika juu ya mwaka mmoja tangu kujiuzulu kwa Papa Benedikt wa 16, akikumbushia mambo mema aliyoyatenda na jinsi anavyokumbukwa, akisema:

Watu wanapenda kusahau, kwamba Benedikt wa 16 aliweka msingi wa mambo mengi ambayo papa Francis anayatekeleza hivi sasa. Alikuwa papa huyo aliebadilisha kitambaa cha ufalme kwenye kanzu yake na kuamua kuva kilemba cha kawaida, na hivyo kumuonyesha zaidi kama askofu wa Roma. Hata kupitia dhana yake ya imani na hekima, na wito wake wa uelewa sahihi wa dhana ya kujitenga na mambo ya kidunia, Benedikt alikuwa akimfanyia kazi mrithi wake. Kwa hivyo urithi wa Benedikt umekuwa na ufanisi - si tu katika sheria kali alizoziweka kupambana na vitendo vya kuwanajisi watoto miongoni mwa mapadri.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga
Mhariri: Mohammed Khelef