1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapigania uhuru wa Mau Mau kuenndelea kudai fidia kwa Uingereza

Mohamed Dahman25 Mei 2007

Mashujaa wa kupigania uhuru wa Kenya Mau Mau wameapa kuendeleza mapambano ya kudai fidia kutoka kwa serikali ya Uingereza kwa dhuluma walizotendewa wakati wa utawala wa ukoloni katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki baada ya Uingereza kutupilia mbali madai yao ya fidia.

https://p.dw.com/p/CHDn
Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Jomo Kenyatta mjini Nairobi Kenya.
Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Jomo Kenyatta mjini Nairobi Kenya.Picha: picture-alliance / Helga Lade Fo

Kwa Mau Mau kipindi hicho cha kale bado si historia.

Hatutonyamazishwa amesema hayo Gitu wa Kahengeri mwanachama wa Chama cha Wapiganaji wa Vita vya Mau Mau wakati alipozungumza na waandishi wa habari katika mji mkuu wa Kenya Nairobi ambapo amesema wameazimia kuendelea kufunguwa kesi katika mahkama za Uingereza sio kwa ajili ya fedha bali kuonyesha kwamba haki za binaadamu hazipaswi kuvunjwa.

Wakisaidiwa na Tume ya Haki za Binaadamu ya Kenya wakongwe hao wa vita waliwasilisha dai lao rasmi la kutaka kulipwa fidia hapo mwezi wa Oktoba mwaka 2006.

Inakadiriwa kwamba wapiganaji 13,000 wa Mau Mau wamekufa kutokana na kuandamwa kulikotokea baada chama chao kuanzisha uasi dhidi ya wakoloni katika miaka ya 1950 wakati watu wengine zaidi 80,000 waliouhusishwa na uasi huo inaaminika kuwa walizuiliwa kwenye makambi.Takriban wanachama wengi wa Mau Mau walikuwa ni wa kabila la Kikuyu ambalo ni kabila kubwa kabisa nchini Kenya.

Dhuluma walizotendewa chama hicho na wale wanaodaiwa kuwaunga mkono ni pamoja na zile za ngono zilizofanywa na wanajeshi wa Kiafrika waliokuwa wakitumikia utawala wa kikoloni.

Uingereza ilitowa jibu la madai yao ya fidia hapo mwezi uliopita.

Imesema hawawezi kukubali kwamba Ofisi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Jumuiya ya Madola na idara nyengine yoyote ile ya wizara ya mambo ya nje ya Uingereza kuwajibika kisheria kwa aina yoyote ile kuhusiana na madai yao.

Mau Mau ilipigwa marufuku wakati wa utawala wa ukoloni na iliendelea kupigwa marufuku baada ya uhuru wa nchi hiyo hapo mwaka 1963 na amri hiyo ya kupigwa marufuku kwake iliondolea tu miongo minne baadae kufuatia kiongozi wa sasa wa Kenya Mwai Kibaki kushika madaraka na kukiwezesha chama hicho cha Mau Mau kuundwa.

Kaimu Mkurugenzi mtendaji wa Tume ya Haki za Binaadamu nchini Kenya Mwambi Mwasarru ameuliza vipi wanusurika wa Mau Mau wangeliweza kukutana kuzungumzia mashaka yao wakati chama chao kilikuwa kikihesabiwa kuwa sio halali?

Jimmy Rugunya akikumbuka dhila hizo anasema waliteseka kweli chini ya mikono ya mabwana wao wa kikoloni na kupelekwa kwenye makambi ya mahabusu walikoteswa kukaribia kufa ambapo wazungu hwazibiginya sehemu zao za siri kwa kutumia koleo.

Katibu Mkuu wa Chama cha Wapiganaji wa Mau Mau Augustine Kamunde amekaririwa akisema kwamba alikuwa na watu 120 waliokuwa chini yake na 111 waliuliwa kwa kupigwa risasi na tisa akiwemo yeye mwenyewe walikimbia ambapo wazungu walichukuwa ardhi yao baada ya wao kutokomea misituni.

Amesema wanawake walibakwa na kutumbukizwa vitu kwenye sehemu za siri wakati watoto wao wakiaangalia unyama huo ukitendeka.

Timu ya wataalamu wa kisheria kutoka Tume ya Haki za Binaadamu ya Kenya inatazamiwa kukusanya ushahidi zaidi juu ya kesi hiyo huko London wakati ikitarajiwa kuwasilishwa mahkamani hapo mwezi wa Novemba.