1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapiganaji waukamata mji wa Mosul

10 Juni 2014

Polisi na wanajeshi nchini Iraq wamevikimbia vituo vyao katika mji wa kaskazini wa Mosul baada ya wapiganaji kukamata makao makuu ya serikali ya jimbo hilo pamoja na majengo mengine muhimu.

https://p.dw.com/p/1CFJX
Irakische Soldaten werden nach Mosul verlegt 08.06.2014
Wanajeshi wa IraqPicha: Haidar Hamdani/AFP/Getty Images

Hatua hiyo ya wapiganaji ni pigo kubwa kwa juhudi za serikali mjini Baghdad za kudhibiti mapambano yanayoongezeka nchini humo.

Afisa wa jimbo hilo pamoja na wakaazi wa eneo hilo wamesema leo kuwa wapiganaji walikamata jengo la serikali, ikiwa ni alama muhimu ya mamlaka ya taifa, jana Jumatatu , kufuatia siku kadhaa za mapigano katika mji huo ambao ni wa pili kwa ukubwa nchini humo, ambako pia ni ngome kuu ya kundi la zamani la al-Qaeda ulioko katika kile ambacho kwa muda mrefu ni eneo lenye machafuko nchini Iraq.

Irak Anschlag
Mashambulizi dhidi ya maoneo mbali mbali nchini IraqPicha: Reuters

Watu wenye silaha pia wamechoma moto vituo kadhaa vya polisi mjini humo, na kuwaacha huru wafungwa ambao walikuwa korokoroni.

Wapiganaji wanaaminika kuwa wanamahusiano na kundi la taifa la Kiislamu la Iraq na Sham , tawi lililotokana na kundi la al-Qaeda ambalo linahusika na mashambulizi mengi yaliyomwaga damu nchini Iraq na ni miongoni mwa waasi wanaofanya vitendo vya vya kikatili zaidi vinavyopambana kuuondoa utawala wa rais Bashar al Assad katika nchi jirani ya Syria.

Kundi hilo pia limejaribu kujiweka kama watetezi wa kundi kubwa la Wasunni walio wachache ambao wamekuwa hawaridhishwi na kile kinachotokea nchini humo.

Wakaazi wakimbia

Wakaazi kadha wa mji wa Mosul ambao wanahofu wameripoti kuona watu hao wenye silaha wakipandisha bendera nyeusi ikiwa na maandishi ya Kiislamu ambayo yanasemekana kuwa yametumiwa na kundi la ISIL, al-Qaeda na makundi mengine ya kijihad.

Irak Protest in Mosul
Maandamano katika mji wa MosulPicha: picture alliance/dpa

Wapiganaji hao wanaonekana kuwa wanaudhibiti katika maeneo kadha ya mji , wamesema kwa simu, wakizungumzuma kwa masharti ya kutotajwa majina kwa hofu ya kuadhibiwa.

Wafungwa wameachwa huru kutoka vituo vya polisi wameonekana wakikimbia mitaani katika sare zao za njano , wamesema.

Um Karam , mwajiriwa wa serikali ambaye anaishi kiasi ya kilometa mbili kutoka kutoka makao makuu ya jimbo hilo, amesema familia yake imeamua kukimbia kutoka mji huo mapema leo Jumanne baada ya kusikia juu ya kukamatwa kwa jengo la serikali.

Hofu imetanda

Hali ni ya mtafaruku ndani ya mji huo na hakuna mtu yeyote wa kutusaidia , "mama huyo ambaye ni mkristo mwenye watoto wawili amesema, akitumia jina la bandia akihofia usalama wake. "Tunahofu... hakuna polisi ama jeshi mjini Mosul."

Irak Wahlen Ministerpräsident Nuri al-Maliki in Bagdad Wahllokal
Rais Nouri al-Maliki wa IraqPicha: Reuters

Hatua hiyo ya wapiganaji inakuja wakati waziri mkuu wa Iraq anayekabiliana na matatizo kadhaa, Nouri al-Maliki , anahangaika kubaki madarakani kufuatia uchaguzi wa bunge mwishoni mwa Aprili ambao umempa viti vingi lakini hakuweza kupata wingi wa kutosha unaohitajika kuunda serikali mpya moja kwa moja.

Wasunni wengi wa Iraq wanahisi kuwa wametengwa chini ya uongozi wa al-Maliki katika muda wa miaka minane ya utawala wake na wanamuona kuwa anahusisha kwa karibu zaidi na washia wahafidhina na nchi jirani ya Iran ambayo ina nguvu.

Mosul uko kilometa 360 kaskazini magharibi ya Baghdad, katika jimbo la Ninevah.

Mwandishi : Sekione Kitojo / ape

Mhariri: Mohammed Abdul Rahman