1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi wafanikiwa kuwaondoa wapiganaji kutoka Ghazni

Admin.WagnerD15 Agosti 2018

Hatimaye Wanajeshi wa Afghanistan wamewaondoa wapiganaji wa Taliban katika mji wa Ghazni leo, huku wamiliki wa maduka na wakazi wakirejea katika mitaa ya mji huo kuendelea na shughuli zao,baada ya siku kadhaa za mapigano

https://p.dw.com/p/33CoR
Gefechte in Afghanistan
Wanajeshi wa Afghanistan wakishika doria mjini GhazniPicha: picture-alliance/AP Photo/M. A. Danishyar

Maafisa wa usalama wameonekana wakipiga doria katika mji huo huku mapigano yakiwa yamesitishwa. Lakini wakati wamiliki wa maduka wakiendelea kukarabati maduka yao ambayo yaliharibiwa kutokana na hali hiyo, kumetolewa tahadhari kwamba wapiganaji hao bado wako karibu, imesababisha wasiwasi kwamba mapigano huenda yatatokea tena.

Wanajeshi wa Afghanistan kwa ushirikiano na wale wa anga kutoka Marekani walifanya juhudi kuwaondoa wapiganaji kutoka Ghazni, tangu mapigano yalipoanza Alhamisi wiki iliyopita. Idara za usalama zimesisitiza kwamba mji huo ungali katika mikono ya serikali, huku hali kuhusu ni lini operesheni hiyo itakamilishwa ikiwa bado haijulikani.

Mkuu wa Polisi wa Ghazni Farid Mashal amesema kwamba wanajeshi wa nchi hiyo walijitolea kupigana dhidi ya maadui ili kuwalinda wananchi . ´´Kutokana na mapigano makali yaliyofanikishwa na wanajeshi wetu, idadi kubwa wapiganaji walijeruhiwa. Wanajeshi walipigana kwa kujitolea dhidi ya maadui zetu katika maeneo mbalimbali ya mji wa Ghazni na kuwalinda wanachi pamoja na nchi yetu.´´

Afghanistan Kämpfe in Ghazni
Mji wa Ghazni uliposhambuliwa na wapiganaji wa TalibanPicha: Getty Images/AFP/Z. Hashimi

Mapigano hayo ndiyo makubwa zaidi kutokea tangu tangazo la kusitishwa kwa vita lililotolewa mwezi Juni kuchangia mapigano kati ya wapiganaji wa Taliban na wanajeshi kukomeshwa, na kuwapa afueni raia wa Afghanistan. Hata hivyo Umoja wa Mataifa umeonya kwamba huenda kukashuhudiwa maafa makubwa ya binadamu kutokana na mapigano hayo.

Raia wa Afghanistan warejeshwa kwao kutoka Ujerumani

Hayo yakijiri, ndege iliyokuwa imewabeba wakimbizi 46 wa Afghanistan imetua mapema leo katika mji wa Kabul. Wakimbizi hao wamerejeshwa kwao baada ya kurudishwa  kutoka Ujerumani. Hatua hiyo ni ya kumi na tano tangu Desemba mwaka 2016 ya wakimbizi kurejeshwa makwao.Mwezi uliopita, mmoja wa wakimbizi ambaye ni raia wa Afghanistan alijiua alipowasili mjini Kabul,baada ya kufurushwa kutoka Ujerumani. Alikuwa ameishi nchini humo kwa miaka miaka minane kabla ya kurejeshwa kwao.

Hatua ya kuwarejesha raia hao kwao inajiri licha ya kuwapo kwa tishio la kiusalama nchini Afghanistan. Wapiganaji wa Taliban wamekataa kufanya mazungumzo na kuendelea kuishambulia serikali pamoja na wanajeshi.

Wakati huo huo kundi la kigaidi la Dola la Kiislamu  IS linaendelea kuongeza mashambulizi yake katika maeneo ya mijini. Kwa mujibu wa Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo, Luteni Jenerali Tariq Shah, watu takriban 130 wameuwawa katika siku kadhaa zilizopita kufuatia mapigano katika eneo la Ghazni.

Mwandishi: Sophia Chinyezi/DPAE/AFP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman