1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapiganaji wa Kiislamu waiteka miji kadhaa nchini humo.

Ponda, Eric Kalume14 Novemba 2008

Habari kutoka nchi ni Somalia zinasema kuwa wapiganaji wa kiislamu nchini humo wanaukaribia Mji mkuu wa Mogadishi baada ya kuteka miji mingine mitatu katika muda wa siku tatu zilizopita.

https://p.dw.com/p/FuyF
Wapiganaji wa Kiislamu nchini Somalia ambao wameiteka miji mitatu na sasa wanaukaribia mji mkuu wa Mogadishu.Picha: picture-alliance/dpa


Habari kutoka nchi ni Somalia zinasema kuwa wapiganaji wa kiislamu nchini humo wanaukaribia Mji mkuu wa Mogadishi baada ya kuteka miji mingine mitatu katika muda wa siku tatu zilizopita.





Wapiganaji hao wa kundi la Al Shabab sasa yaripotiwa wako umbali wa kilomita 15 tu kusini mwagharibi mwa Mji huo wa Mogadishu.




Kundi la Al- Shabab ambao ni mrengo wa kundi la waliokuwa wapiganaji wa mahakama za kislamu, waliotimuliwa mwaka wa 2006 na majeshi ya Ethiopia, wameimarisha mashambulizi yao dhidi ya serikali ya muungano nchini humo, na kuuteka mji wa Elasha, yapata umbali wa kilomita 2 kutoka kituo cha Sinkadheer, kinachosimamiwa na majeshi ya Ethiopia.


Mnamo siku ya Jumatano wapiganaji hao waliuteka mji wa Merka, ulioko umbali wa kilomita 90 kusini magharibi mwa Mji wa Mogadishu,ambao ni mji muhimu wa bandari unaotumiwa na Umoja wa Mataifa na shirika la chakula duniani, kusafirisha misaada ya kibinadamu.


Baada ya kuiteka miji hiyo mitatu, wapiganaji hao wametangaza kuzingatiwa kwa sharia za kiislamu katika miji yote wanayoisimamia, ingawa kamanda wa kundi hilo la wapiganaji Sheikh Abdi Muse amesema kuwa kamwe wapiganaji wake hawatatatiza shughuli za kusafirisha misaada ya kibinadamu hasa katika mji wa bandari wa Merka.


Zaidi ya theluthi moja ya idadi ya watu nchini Somalia wanategemea misaada ya kibinadamu kupitia mji huo wa Bandari wa Merka.


Hali hiyo imezidisha hofu ya kuzuka upya kwa mapigano baina ya majeshi ya Ethiopia na wapiganaji hao wa Al- Shabab, na tayari wakaazi wa maeneo hayo wameanza kutoroka.


Wapiganaji hao wamekataa mpango wa kusitisha mapigano na kugawana madaraka katika serikali ya muungano, mpango ulioongozwa na Umoja wa mataifa, hali inayotikisa zaidi uthabiti wa taifa hilo la upembe mwa Africa, ambalo halijakuwa na serikali thabiti kwa zaidi ya miaka 17.


Ukosefu wa uthabiti katika eneo hilo la upembe wa Africa pia umechangia kuongezeka kwa visa vya maharamia na kutishia shughuli za usafiri wa vyombo vya baharini katika pwani ya Somalia.


Chini ya mkataba huo, majeshi ya Ethiopia ambayo yamekuwa yakishika dora mjini Mogadishi na maeneo mengi nchini humo,yalitarajiwa kuondoka baadaye mwezi huu, lakini matukio ya hivi punde huenda muda huo ukaongezwa zaidi.


Majeshi ya Ethiopia yaliingia nchini Somalia mwaka wa 2006 kuisaidia serikali changa ya mpito nchini humo na hatimaye kuwatimua wapiganaji wa Kunsi la mahakama za Kiislamu.


Wapiganaji wa kundi la Shabab wanasema kuwa nia yao ni kuingia madarakani na kutangaza sharia za kiislamu kote nchini humo. Mwezi uliopita, mvulana mmoja aliyepatikana na kosa la zinaa aliuawa kwa kupigwa mawe kusini mwa Mji wa Kismayu.


Habari zaidi zasema kuwa kuwa maelfu ya wakaazi nchini humo wanakabiliwa na njaa kutokana na vita hivyo na ukame.

Shirika la msalaba mwekundu linasema kuwa zaidi ya watu elfu 435 wabnahitaji misaada ya dharura nchini humo.