1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapiganaji dhidi ya Gaddafi wapata hasara kubwa Sirte

28 Septemba 2011

Vikosi vinavyompinga Muammar Gaddafi vimepata hasara kubwa leo wakati vikielekea kwenye eneo la kiongozi huyo wa Libya aliepinduliwa katika mji alikozaliwa wa Sirte na pia wamepata kipigo katika mji wa Bani Walid.

https://p.dw.com/p/Ro6I

Kwa upande wa kisiasa, mjumbe wa Baraza la Taifa la Mpito nchini Libya amesema kuundwa kwa serikali ya mpito ambako tayari kumecheleweshwa kutokana na mizozo juu ya kuwagana madaraka, kumeahirishwa hadi hapo watakapoitia mkononi nchi nzima.

Katika ujumbe wa radio, Moamer Gaddafi amepongeza upinzani uliopo huko Bani Walid ambapo Baraza la Taifa la Mpito limesema wapiganaji wake wanne wameuwawa na 11 wamejeruhiwa katika mapambano makali na vikosi tiifu kwa Gaddafi.

Hasara kubwa zaidi imepatikana katika mji wa Sirte ambapo wapiganaji wa Baraza hilo la Taifa la Mpito wanapambana kuingia kati kati ya mji huo mkubwa ulioko katika bahari ya Mediterranean na mahala ambapo kuna nyumba ya Gaddafi na mahandaki ya kijeshi.

Wapiganaji wa serikali mpya Libya wakiushambulia mji wa Sirte
Wapiganaji wa serikali mpya Libya wakiushambulia mji wa SirtePicha: dapd

Mapigano hayo ambayo yaliendelea hadi usiku hapo jana yalijikita karibu na hoteli ya Mahari, mashariki ya Sirte, wapiganaji waasi walipigana mtu na mtu na vikosi tiifu kwa Gaddafi na kupoteza wapiganaji 10. Hayo yameelezwa na kamanda mmoja wa Baraza la Taifa la Mpito kwa sharti la kutotajwa jina kutokana na unyeti wa habari hizo. Kwa mujibu wa kamanda huyo wapiganaji wao na wale vichwa ngumu wa Gaddafi wamekuwa kwenye mapambano ya barabarani na kushambuliana kwa kutumia bunduki za Kalashnikovs na maguruneti yanayovurumishwa na roketi.

Wapiganaji wa serikali mpya ya Libya mapema jana waliiteka bandari ya Sirte, huo ukiwa ni ushindi muhimu katika mpambano ya kuuteka mji huo alikozaliwa Gaddafi.

Hata hivyo, wanatarajia kuwepo kwa mapigano makali ya kulidhibiti eneo yalioko makaazi ya Gaddafi, kitovu cha upinzani uliobakia ambapo inafikiriwa kuwa baadhi ya familia ya Gaddafi imejificha.

Mpiganaji wa waasi, Fateh Marimri, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba wapiganaji wa Gaddafi wamekuwa wakitumia silaha nzito, wanapigana wakiwa wamevalia nguo za kiraia na kwamba kuna mamluki wa Kiafrika kila mahala huko Sirte.

Kiongozi wa zamani wa Libya Muammar Gaddafi na mke wake Safiya
Kiongozi wa zamani wa Libya Muammar Gaddafi na mke wake SafiyaPicha: AP

Maelfu ya raia wenye hofu wamekuwa wakiukimbia mji wa Sirte ulioko kama kilomita 360 mashariki mwa mji mkuu wa Tripoli wakati vikosi vya utawala mpya vikiusogelea mji huo kutoka upande wa mashariki, kusini na magharibi. Baadhi ya watu wanasema kwamba vikosi vya Gaddafi vimekuwa vikijaribu kuwazuwia watu wasiukimbie mji huo.

Katika ujumbe wa radio, Gaddafi amesema bado anapambana na yuko tayari kufa shahidi. Amesema mashujaa wamepigana na kufa mashahidi na kwamba wao pia wanasubiri kufa mashahidi.

Habari zaidi zinasema kwamba inaaminika Gaddafi amejificha karibu na mji wa magharibi wa Libya wa Ghadamis ulioko karibu na mpaka wa Algeria akiwa chini ya ulinzi wa kabila la Touareg.

Mwandishi : Mohamed Dahman/ AFP

Mhariri: Miraji Othman