Wapiganaji 65 wauawa Yemen | Matukio ya Kisiasa | DW | 02.09.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Wapiganaji 65 wauawa Yemen

Wapiganaji 65 wameuawa katika mapigano, baada ya waasi wa Houthi wa Yemen kuanzisha mashambulizi kwenye jimbo la Marib, ngome ya mwisho ya serikali kaskazini mwa nchi hiyo ambalo lina utajiri wa mafuta. 

Afisa wa polisi amesema leo kuwa waasi wanaoungwa mkono na Iran wameyashambulia maeneo yanaoungwa mkono na serikali kusini mwa mji huo wa kimkakati, na kusonga mbele, licha ya kupoteza wapiganaji kadhaa katika mashambulizi ya anga ya majeshi ya muungano.

Hilo lilikuwa shambulizi la kwanza kubwa kufanywa na waasi wa Houthi kwenye jimbo la Marib, tangu mwezi Juni wakati wapiganaji 111 wa pande zote mbili walipouawa katika mapigano yaliyodumu kwa siku tatu.

Wengine 50 wajeruhiwa

Afisa wa jeshi la serikali amesema wanajeshi 22 wanaoungwa mkono na serikali wameuawa na wengine 50 wamejeruhiwa, huku wapiganaji wa Houthi nao wakiuawa ndani ya saa 48 zilizopita. Idadi hiyo imethibitishwa na duru nyingine za kijeshi na kitabibu.

Mapigano hayo yameibuka tena baada ya mashambulizi ya makombora dhidi ya kambi kubwa ya kikosi cha anga ya Yemen, kusini mwa nchi hiyo na kuwaua takriban wapiganaji 30 wanaoungwa mkono na serikali siku ya Jumapili katika shambulizi baya kushuhudiwa tangu mwezi Desemba.

Jemen | Viele Tote bei Raketenangriff auf Luftwaffenstützpunkt Al-Anad

Gari la kubeba wagonjwa likiwaondoa majeruhi kwenye kambi ya anga ya Al-Anad

Watu wengine 64 walijeruhiwa katika shambulizi hilo lililotokea kwenye kambi ya Al-Anad kwenye jimbo la Lahj. Hakuna kundi lolote ambalo limekiri kuhusika na shambulizi hilo.

Shambulizi hilo pia limefanyika siku chache baada ya mjumbe mpya wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Yemen, Hans Grundberg kuanza majukumu yake.

Mashambulizi yameongezwa hivi karibuni

Waasi hao wameongeza mashambulizi kutaka kuiteka Marib katika miezi ya hivi karibuni, ambako mamia ya wapiganaji kutoka pande zote mbili wameuawa.

Huku Umoja wa Mataifa na Marekani zikishinikiza mchakato wa kumaliza vita, waasi wa Houthi wanataka kufunguliwa tena kwa uwanja wa ndege wa Sanaa, ambao umefungwa kutokana na kizuizi cha Saudi Arabia tangu mwaka 2016, kabla ya kufikiwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano au mazungumzo yoyote yale.

Serikali ya Yemen inayotambuliwa kimataifa na kuungwa mkono na muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia, na waasi wa Houthi wamekuwa katika vita tangu mwaka 2014, wakati wanamgambo walipochukua udhibiti wa mji mkuu, Sanaa na maeneo mengi ya kaskazini, hatua iliyoilazimisha serikali ya Abed Rabbo Mansour Hadi kukimbia.

Wakati huo huo, kituo cha Habari cha Houthi kimesema kuwa majeshi hayo ya muungano yameanzisha mashambulizi kadhaa ya anga kwenye miji ya Marib, ikiwemo Rahbah, Sirwah na Madghel, kwa lengo la kuvisaidia vikosi vinavyoungwa mkono na serikali.

(AP, AFP)