1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapenda mageuzi wavinjari nchini Syria

8 Julai 2011

Katika wakati ambapo wanaharakati wa vuguvugu la mageuzi ya kidemokrasi wanapanga kuteremka tena majiani leo,Syria inaituhumu Marekani kuchochea uasi

https://p.dw.com/p/11rPL
Maandamano dhidi ya rais Bashar al AssadPicha: dapd

Wanaharakati wa vuguvugu la wapenda demokrasia nchini Syria wanajiandaa kwa maandamano mengine hii leo- kauli mbiu ikiwa "La hatutaki majadiliano"Mamia ya wakaazi wa Hama wanaupa kisogo mji huo ambako raia 25 waliuliwa na vikosi vya usalama, huku serikali ya mjini Damascus ikiituhumu Marekani kujihusisha na vugu vugu la wapenda demokrasia.

Kama kila siku kama ya leo, baada ya sala ya ijumaa, wanaharakati wa miji tofauti ya Syria, na hasa Hama, wanapanga kuteremka majiani kwa wingi, wakipania kuliko wakati wowote mwengine kuzidisha makali ya vuguvugu lao lililoanza March 15 iliyopita,licha ya hatua kali za jeshi zilizogharimu maisha ya zaidi ya raia 1300 hadi sasa. "Hatutaki majadiliano" ndio kauli mbiu ya maandamano ya leo, ambapo wanaharakati wanaodai demokrasia wanahisi hakuna haja ya kuzungumza ikiwa vikosi vya usalama havitaondolewa majiani, na kama utawala hautaacha kutumia nguvu dhidi ya raia.

Balozi wa Marekani mjini Damascuas, Robert Ford, amekwenda Hama -kitovu cha maandamano dhidi ya serikali ya rais Bashar al Assad. Kwa mujibu wa afisa mmoja wa ngazi ya juu wa Marekani, balozi Robert Ford, anapanga kusalia huko kufuatilizia maandamano hayo na kujaribu "kuanzisha maingiliano" pamoja na upande wa upinzani.

Syrien Präsident Bashar Assad 24.04.2011
Rais Bashar al Assad wa SyriaPicha: picture-alliance/dpa

Serikali ya mjini Damascus, lakini, inaiangalia kwa jicho jengine kabisa ziara hiyo. Wizara ya mambo ya nchi za nje ya Syria imesema katika taarifa yake, na hapa tunanukuu: "Kuwepo balozi wa Marekani huko Hama bila ya ruhusa ni ushahidi bayana wa kuhusika Marekani na hali ya sasa na azma yao ya kutaka kuzidisha mivutano."Mwisho wa kunukuu.

Kutokana na kuzidi matumizi ya nguvu dhidi ya waandamanaji, katibu mkuu wa Umoja wa mataifa, Ban Ki-Moon, ametoa mwito "mauwaji yakome " , huku waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ufaransa, Alain Juppé, akilalamika na kusema "si jambo linalokubalika kuona baraza la Usalama linashindwa kulaani ukandamizaji kutokana na upinzani wa Moscow."

Viongozi wanajaribu kuuvunja nguvu uasi huko Hama, mji ulioko kilomita 210 kaskazini ya mji mkuu Damascus, na ambako raia 25 wameuliwa tangu jumanne na vikosi vya usalama.

Jumla ya watu elfu moja wameuhama mji huo na kukimbilia al-Selmiya.

Mkuu wa shirika la haki za binaadam la Syria, Ammar Qorabi, amethibitisha habari hizo na kusema watu wanakimbia mauwaji na watu kukamatwa ovyo.

Syrien Demonstration Facebook
Wanajeshi wa SyriaPicha: picture-alliance/dpa

Wakati huo huo, vikosi vya usalama vya Syria vimeingia katika kitongoji cha Harasta, kaskazini mwa mji mkuu Damascus. Askari polisi na wanajeshi wameingia majumbani na kuwakamata watu mtindo mmoja. Shirika la haki za binaadam la Syria linasema vikosi vya usalama viliingia pia hospitali kuwasaka na kuwakamata wapinzani.

Mwandishi:Hamidou Oummilkhheir/AFP/Reuters

Mhariri: Miraji Othman