1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapalestina wapambana na polisi wa Israel

Sylvia Mwehozi
21 Julai 2017

Rais Mahmoud Abbas wa Palestina ameitaka Marekani kuishinikiza Israel kuachana na hatua mpya za kiusalama ambazo zimechochea mvutano katika eneo takatifu la Jerusalem ambalo linazozaniwa.

https://p.dw.com/p/2gyul
Protest in Jerusalem
Picha: Picture alliance/AA/M. Alkharouf

Wapalestina wamepambana na polisi wa Israel kwenye leo hilo baada ya kumalizika swala ya Ijumaa huku ripoti zikisema Mpalestina mmoja ameuawa. 

Shirika la habari la Palestina, WAFA, limeripoti leo kuwa Abbas ametoa ombi hilo wakati wa mazungumzo ya simu na mshauri mwandamizi wa Ikulu ya Marekani, Jared Kushner. Abbas ameonya kuwa hali katika eneo hilo linalotambuliwa na Waislamu kama eneo tukufu na Wayahudi kama Mlima wa Hekalu, ni mbaya sana na huenda ikashindwa kudhibitiwa.

Israel verschärfte Sicherheitsvorkehrungen am Tempelberg in Jerusalem
Mitambo ya kutambua silaha za vyuma inayolalamikiwa na WapalestinaPicha: picture-alliance/dpa/M. Illean

Hayo yanajiri wakati ambapo Mpalestina mmoja ameuawa leo kwa kupigwa risasi kichwani mashariki mwa Jerusalem karibu na Mji Mkongwe. Wizara ya afya ya Palestina imesema kuwa mauaji hayo yametokea baada ya ghasia kuzuka katika kitongoji cha Ras al-Amud, ingawa haijamtaja anayehusika na mauaji hayo. Wizara hiyo inasema watu wapatao 20 wamekimbizwa hospitalini kutokana na majeraha ya risasi za mpira na kuvuta gesi ya kutowa machozi.

Kutokana na hatua mpya za kiusalama zilizowekwa na Israel, Wapalestina wameshindwa kuingia katika msikiti wa Al-Aqsa ambao unatumiwa na Wislamu na Wayahudi na hivyo kulazimika kuswali nje ya ukuta wa mji wa kale. Waumini wa kiume wa Kiislamu chini ya umri wa miaka 50 hawakuruhusiwa kuingia katika eneo hilo hii leo ambalo limekumbwa na mashambulizi ya mara kwa mara. Rafique Hayat ni muumini wa Kiislamu anayeishi Jerusalem anasema "eneo hili ni kwa ajili ya kumwabudu Mungu. Hawawezi kuwazuia Waisalamu kuingia na kuswali. Wanafanya kitu kilicho kinyume na Mungu."

Israel verschärfte Sicherheitsvorkehrungen am Tempelberg in Jerusalem
Waislamu wakiswali mtaani nje ya eneo takatifu lililowekwa vizuizi na polisi wa IsraelPicha: Getty Images/AFP/A. Gharabli

Wapalestina pia walifanya swala yao katika kizuizi cha kijeshi katika ukingo wa Magharibi unaopakana na Jerusalem. Baada ya swala kumalizika polisi waliusogelea umati uliokusanyika na kuanza kuwashambulia kwa gesi ya kutowa machozi na risasi za mpira.

Polisi ya Israel imesema hatua hiyo imechangiwa na Wapalestina hao kuwashambulia maafisa wake baada ya swala. Wapalestina wanapinga utaratibu mpya wa mitambo ya kutambua vitu vya chuma na vizuizi, ulioanzishwa na polisi wa Israel Jumapili iliyopita ili kuwakagua waumini wa Kiislamu wanaoingia katika eneo hilo baada ya kuuawa kwa maafisa wawili wa polisi wa Israel wiki iliyopita.

Israel imeongeza askari wa ziada katikati mwa hofu ya vurugu baada ya mapambanao ya kila siku ndani ya wiki hii. Zaidi ya Wapalestina 20 walijeruhiwa jana jioni baada ya kuwashambulia polisi kwa mawe na chupa za vioo katika eneo hilo.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/dpa

Mhariri: Mohammed Khelef