Wapalestina wakosa huduma za afya kufuatia mgomo wa wafanyakazi wa zaidi ya mwezi mzima | Masuala ya Jamii | DW | 19.10.2006
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Wapalestina wakosa huduma za afya kufuatia mgomo wa wafanyakazi wa zaidi ya mwezi mzima

Mgomo wa waganga na wauguzi unaoendelea katika maeneo ya Palestina, umeiathiri sekta ya afya kwa kusababisha ukosefu mkubwa wa huduma za afya kwa raia ambao tayari wanakabiliwa na matatizo kadhaa. Mgomo huo wa kudai malimbikizo ya mishahara, unabainisha matatizo yanaoikabili serikali yenye kuongozwa na chama cha Hamas ambayo imewekewa vikwazo vya fedha na nchi za magharibi.

Mtoto akitibiwa katika hospital ya Beit Lahiya-Gaza kabla ya mgomo wa wafanyakazi

Mtoto akitibiwa katika hospital ya Beit Lahiya-Gaza kabla ya mgomo wa wafanyakazi

Kisa kilichomfika mwanamama Rania Hih kurudishwa nyuma bila kuweza kumtibisha mwanae wa kiume aliyekuwa akipiga kelele za maumivu baada ya kuvunjika mkono, ni mfano tu wa usumbufu unaowakabili Wapalestina kupata huduma za afya. Watu kiasi ya nusu milioni hutegemea huduma za afya kwa hospitali ya serikali ya Alia Hospital katika Ukanda wa Gaza ambayo sasa ni kama tupu.

Madaktari na wauguzi wamo mgomoni tangu tarehe 2 mwezi uliopita pamoja na wafanyakazi wengine wa sekta mbali mbali wakidai malimbikizo ya mishahara.

Mgomo huo umekwamisha shughuli katika sekta muhimu kama afya na elimu. Hospitali za serikali zimekuwa zikitoa huduma za dharura tu.

Hospitali ya Hebron, ambayo ilikuwa ikiwapokea wagonjwa 250 kwa siku mnamo mwezi Agosti mwaka huu, sasa inawapokea watu 20 tu. Wakati huo huo idadi ya akinamama waliojifungua kwa siku katika hospitali hiyo ya Hebron ilishuka kutoka 23 hadi 4.

Inaafiriwa kwamba hali ni mbaya zaidi katika Ukingo wa magharibi mwa mto Jordan ambako vipimo katika maabara vimesitishwa. Uchunguzi wa mimba kwa akinamama wajawazito hufanyike tena au huduma kwa watoto wachanga kama chanjo hazitolewi. Wagonjwa wa kisukari na maradhi mengine yanayohitaji huduma za kila mara wanaangaika pia.

Kwenye mlango mkubwa wa hospitali, mara nyingi kumeandikwa ´´utapokelewa ikiwa ni dharura´´.

Hao ni pamoja na wagonjwa mahatuti au wale ambao wamekumbwa na ajali na kupoteza damu, au wamevunjika mifupa au wanaokabiliwa na maumivu makali tumboni. Wengine wanalazimika kurudi nyumbani bila matibabu.

Hata hivyo shirika la afya duniani WHO, linasema licha ya mfumo huo kuwekwa, hakuna utaratibu ulio wazi kuwatambua wagonjwa ambao wana haki ya kupokelewa na kutibiwa. Fathi Abu Moghli, afisa wa Shirika la WHO mjini Jerusalem, anasema kuna ripoti ambazo hazijathibitishwa kwamba kumekuwa na ubaguzi katika utoaji huduma hizo za dharura za afya kwa kuwapendelea watu tiifu kwa serikali na kuwanyima wapinzani.

Wengi wa wasiopata huduma hukimbilia katika hospitali za watu binafsi ambazo ni ghali au katika mashirika ya kujitegemea ya misaada ama NGO’s. Taarifa zinazungumzia matukio kadhaa ya watu wanaokufa kwa ukosefu wa huduma baada ya kurudishwa nyuma.

Kulitolewa lawama kwamba mgomo huo kwa namna moja una uhusiano na uhasama wa kisiasa kati ya viongozi wa Palestina. Kwamba wengi wa waliogoma ni wafuasi wa chama cha Fatah cha rais Mahmud Abbas wanaojaribu kuiwekea vizingiti serikali ya waziri mkuu Ismail Haniya.

Serikali hiyo iliwekewa vikwazo vya kifedha na nchi za magharibi kutokana na msimamo wake kutoitambua Israeli. Sehemu kubwa ya bajeti ya matumizi ilikuwa ikitolewa kama misaada. Lakini tangu kuingia madarakani chama cha Hamas kufuatia uchaguzi mwezi Machi mwaka huu, sehemu kubwa ya misaada ya kifedha ilibanwa na wafanyakazi wa serikali hawapokei mishahara kama kawaida na hivyo kusababisha mzozo mwingine wa kijamii.

 • Tarehe 19.10.2006
 • Mwandishi Gregoire Nijimbere
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHmK
 • Tarehe 19.10.2006
 • Mwandishi Gregoire Nijimbere
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHmK

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com