1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanyama aina ya Nyani wamalizika porini

Scholastica Mazula21 Mei 2008

Mamilioni ya Nyani wamekuwa wakiuawa kila mwaka ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya nyama pori.

https://p.dw.com/p/E3sW
Duma,ni miongoni mwa wanyama wanaopatikana katika misitu.Picha: picture-alliance/dpa

Kitendo hicho kinaweza kuleta madhara makubwa kwa misitu ya joto ambayo ni masikani ya Nyani hao barani Afrika, Asia na Amerika ya Kusini.

Hayo yamejitokeza katika Mkutano unaoendelea wa Uhaianuai-Uhusiano kutegemeana kati ya mimea na Viumbe hai, unaofanyika Mjini Bonn, Ujerumani.

Kwa mujibu wa Watafiti wa masuala ya Wanyamapori, kitendo cha kugeuzwa biashara kwa Nyani hao, kumeifanya nyama pori iuzwe kwa bei ya juu katika miji kama ya London ikiwa ni pamoja na vifaa vya kisasa vya uwindaji ambavyo vinawateketeza nyani na kuwagawa vipande vipande.

Kwa kiwango kikubwa Nyani husaidia kusambaza mbegu katika maeneo ya miti, pengine kwa sababu mbegu hizo zinarutubika zaidi baada ya kupita kwenye mfumo wa Nyani unaosaga chakula au kwa sababu zimeondolewa kwenye maganda yake magumu wakati Nyani akitafuta chakula.

Mkutano huo wa Uhaianuai imehudhuriwa pia na Kundi la Ujerumani lenye kutetea uhai wa wanyamapori linalowajumuisha watafiti tisini na mbili wa Kimataifa.

Wajumbe hao wanaojishughulisha na utoaji wa elimu ya Mahusiano ya Viumbe la Mazingira, Sayansi ya muundo wa mimea na elimu ya binadamu, wamehudhuria Mkutano huo kwa lengo la kutathimini athari zinazoweza kujitokeza kufuatia mauaji ya Nyani na kuwasilisha ripoti yao kwa wajumbe elfu tano waliohudhuria Mkutano huo wa wiki mbili.

Matokeo ya utafiti uliofanywa yanaonyesha kwamba hakuna sheria zozote zinazozuia uwindaji na katika maeneo mengine sheria zimekuwa hazifuatwi.

Mmoja wa wataala wa masuala ya kibayolojia kutoka Kundi la watu wanaotetea uhai wa wanyamapori, Sandra Altherr, amesema kwamba zamani nyama ya Nyani ilikuwa ikitumiwa na watu walioko kwenye maeneo hayo ya pori kwa ajili ya mahitaji yao ya chakula, lakini kwa sasa nyama ya Nyani imeonekana kuwa na faida kubwa kibiashara.

Anasema kinachosikitisha sana kwa sasa katika maeneo mengi ya Pori ambako kulikuwa na idadi kubwa ya Nyani, sasa hawaonekani na hata hao wawindaji hawawaoni tena katika makazi yao.

Bibi Altherr, anasema siku hizi wamefikia hatua ya kuua hata ngedere ambao wananyama kidogo sana.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanya hivi karibuni na Kundi la kutetea uhai wa Wanyama pori,unaonyesha kwamba katika maeneo yote ya Amerika ya Kusini kwenye misitu inayopata mvua yakutosha na ambako wanyama aina ya Nyani wamekuwa wakiangamizwa kumekuwa na uwezekano mdogo sana kwa wanyama hao kuishi.

Katika maeneo mengi ya Afrika na Brazil, Nyama ya Nyani imeonekana kuwa nzuri na kupendwa zaidi.

Idadi kubwa ya wahamiaji wakuwa wakiwachukua wanyamapori na kuwapeleka katika nchi za Ulaya Magharibi na Amerika ya Kaskazini ambako sasa pamoja na kwamba ni kinyume cha sheria lakini lengo nikuongeza biashara ya nyama ya Nyani.

Kundi la kutetea uhai wa wanyama linakadiria kwamba kiasi cha wanyama pori wa aina mbalimbali wakiwemo Nyani, milioni tano nukta nne wamekuwa wakitolewa kutoka kwenye misitu ya Amazoni nchini Brazil.