1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ugaidi

Admin.WagnerD6 Mei 2015

Watu wanne wamekatwa kutokana na kutuhumiwa kuwamo katika kundi la mrengo mkali wa kulia.Kwa mujibu wa mwendesha mashtaka mkuu wa Ujerumani, watu hao walikuwa wanapanga kuishambulia misikiti na hifadhi za wakimbizi

https://p.dw.com/p/1FKqO
Makundi ya siasa kali za mrengo mkali wa kulia nchini Ujerumani
Makundi ya siasa kali za mrengo wa kulia nchini UjerumaniPicha: Reuters/Wolfgang Rattay

Maafisa wa idara za usalama leo wamefanya misako nchini Ujerumani kote ambapo wametwaa mabomu na wamewakata watu wanne wa kundi la siasa kali za mrengo wa kulia. Kwa mujibu wa taarifa ya polisi waliokamatwa ni wanaume watatu na mwanamke mmoja wanaotuhumiwa kuwa viongozi wa kundi hilo la siasa kali za mrengo wa kulia.

Ofisi ya mwendesha mashtaka mkuu nchini Ujerumani imearifu kwamba maafisa wapatao 250 kutoka idara za usalama walifanya misako katika jimbo la Saxony na katika majimbo mengine manne ya Ujerumani.

Waendesha mashtaka wamedai kwamba watu hao wannne walihusika katika kulianzisha kundi linaloitwa "Old School Society". Waendesha mashtaka pia wamedai kwamba watu hao wanne walikuwa wanapanga kuishambulia misikiti,sehemu za watu wanaoomba hifadhi ya ukimbizi na pia walikuwa wanapanga kuwashambulia viongozi maarufu wa Waislamu wa madhehebu ya salafi nchini Ujerumani.

Taarifa imesema watu hao wenye umri wa kunzia miaka 22 hadi 56 wamewekwa ndani chini ya kifungu cha mashtaka ya ugaidi. Kulingana na uchunguzi wa hivi karibuni, lengo la watu hao lilikuwa kuvitumia vikundi vidogo vidogo kuwashambulia viongozi wa Waislamu wa madhehebu ya Salafi nchini Ujerumani kote.

Na ili kulitekeleza lengo lao ,watu hao wanne waliokamatwa walimiliki mabomu. Waendesha mashtaka wamesema bado wanajaribu kubainisha iwapo watu hao walikuwa na mipango kamili ya kufanya mashambulio. Wapi na lini watuhumiwa hao walitaka kufanya mashambulio,bado haijabainika. Lakini Polisi wameweza kukusanya ushahidi dhidi yao

Maalfu wanafuata itikadi kali za mrengo wa kulia nchini Ujerumani

Idadi ya watu wenye siasa za mrengo mkali wa kulia, wanaotuhumiwa kuwa hatari nchini Ujerumani, hadi hivi karibuni ilifikia 31,000. Na 10,000 miongoni mwao wanahesabika kuwa watu hatari sana.

Idara za usalama zimeripoti kwamba wapo watu 25,000 wenye siasa za mrengo mkali wa kulia nchini Ujerumani, miongoni mwao mafashisti mamboleo zaidi ya 5000. Baadhi yao wameshiriki katika kuzishambulia hifadhi za wakimbizi na raia wa kigeni . Kwa mujibu wa idara kuu ya ulinzi wa katiba, watu hao walitenda vitendo vya kihalifu zaidi ya 15,000 mnamo mwaka wa 2011 nchini Ujerumani kote.

Watuhumiwa wa ugaidi waliokamatwa leo wametambulika kuwa ni Andreas H, mwenye umri wa miaka 56. Wengine ni Markus W, Olaf na mdogo kabisa ni Denise Vanessa mwenye umri wa miaka 22.

Mwandishi:Mtullya abdu.

Mhariri:Iddi Ssessanga