Wanigeria wapiga kura kumchagua rais | Matukio ya Afrika | DW | 28.03.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

Wanigeria wapiga kura kumchagua rais

Taifa lenye wakaazi wengi barani Afrika, Nigeria, linapiga kura Jumamosi(28.03.2015)kumchagua rais mpya, katika uchaguzi ambao una mvutano mkubwa kuwahi kuonekana tangu nchi hiyo kupata uhuru.

Nigeria - nominierter Präsidentschaftskandidat Muhammadu Buhari und Goodluck Jonathan

Wagombea wakuu katika uchaguzi wa Nigeria, Mohammadu Buhari na Goodluck Jonathan(kulia)

Kuanzia mji mkubwa kabisa wa Lagos katika eneo la Wakristo upande wa kusini mwa nchi hiyo hadi katika miji upande wa kaskazini ambako kunapatikana Waislamu wengi, vituo vya kupigia kura vilitarajiwa kufunguliwa mapema asubuhi, ambapo kiasi ya Wanigeria milioni 68.8 kati ya wakaazi milioni 173 wamejiandikisha kupiga kura.

Nigeria Bildergalerie Staatspräsidenten Muhammadu Buhari

Muhammadu Buhari

Rais Goodluck Jonathan amewasili kwa helikopta katika mji alikozaliwa wa Utuoke kusini mwa jimbo la Bayelsa usiku wa jana Ijumaa, kwa matumaini ya kupata muhula wa pili wa uongozi licha ya ukosoaji mkubwa katika rekodi yake.

Mpizani wake mkubwa , mtu aliyejitangaza kupambana na ufisadi katika serikali Muhammadu Buhari , alikuwa mjini Daura, katika jimbo la kaskazini la Katsina, akilenga kurejea kwa njia ya kidemokrasia madarakani baada ya kuwapo madarakani kwa muda kama mtawala wa kijeshi katika miaka ya 1980.

Mjini Daura, fagio, nembo ya chama cha Buhari cha All Progressives Congress APC, imetundikwa mitaani, katika mji wa Utuoke, mabango yenye mwanvuli na picha ya rais wa sasa Jonathan wa chama cha Peoples Democratic Party PDP yanaonekana mitaani.

Nigeria Bildergalerie Staatspräsidenten Goodluck Jonathan

Rais Goodluck Jonathan

Hamasa kimataifa

Wachunguzi , kuanzia Umoja wa Ulaya na Umoja wa Mataifa hadi Umoja wa Afrika na Marekani wako nchini humo -- ishara ya hamasa ya kimataifa lakini pia kuhakikisha mpambano huru, wa haki na wa uwazi.

Matokeo ya uchaguzi wa rais na bunge unaofanyika kwa wakati mmoja yanatarajiwa kupatikana katika muda wa saa 48 baada ya vituo vya kupigia kura kufungwa, kwa mujibu wa tume ya taifa ya uchaguzi.

Nigeria Wahl 2015 Straßenszene

Mabango mitaani

Chaguzi zilizopita zimechafuliwa na wizi wa kura lakini kuna matumaini kwamba matumizi kwa mara ya kwanza kabisa cha teknolojia ya chombo kinachoshikwa mkononi kinachosoma kadi ya utambulisho ya mpiga kura kwa njia ya "biometriki " itapunguza udanganyifu.

Chama cha PDP cha Jonathan kimekuwa madarakani tangu Nigeria irejee katika utawala wa kiraia mwaka 1999 lakini matokeo hayana uhakika mara hii, wakati upinzani ukiwa katika nafasi imara zaidi kuliko wakati mwingine.

Kushindwa kwa rais hadi hivi karibuni kupambana na kundi la Boko Haram ni hali iliyochukua nafasi kubwa katika uongozi wake na licha ya kuwa Nigeria imekuwa taifa lenye uchumi mkubwa barani Afrika katika wakati wake, matatizo ya biashara ya mafuta dunia yameiathiri nchi yake pakubwa.

Wahlkampf in Nigeria 2015 Goodluck Jonathan

Goodluck Jonathan akifanya kampeni

"Siwezi kukumbuka uchaguzi ambao ni muhimu kuliko huu katika historia ya taifa letu," rais amesema siku ya Alhamis. Chidi Odinkalu , mwenyekiti wa tume ya taifa ya haki za binadamu nchini Nigeria , amesema licha ya kwamba kampeni za uchaguzi hazikuwa nzuri sana, kuna ishara za kutia moyo kuelekea demokrasia.

Hakuna uhakika nani mshindi

"Huwezi kukaa chini hivi sasa na kusema Buhari atashinda, ama rais Jonathan atashinda," ameliambia shirika la habari la AFP. "Itabidi tusubiri na kuona na kuingiwa na hali ya shauku kubwa....na hilo nadhani ni jambo zuri."

Usalama umeimarishwa kote nchini Nigeria , hususan katika eneo lililoathirika zaidi la kaskazini mashariki, ambako miaka sita ya ghasia za kundi la Boko Haram imesababisha watu 13,000 kuuwawa na wengine milioni 1.5 hawana makaazi.

Nigeria, Niger na Chad, zikisaidiwa na Cameroon, hivi karibuni zimedai kupata ushindi mara kadhaa, na kukamata tena maeneo yaliyokuwa yakishikiliwa na waasi.

Wahlkampf in Nigeria 2015

Mabango ya uchaguzi

Siku ya Ijumaa (27.03.2015) jeshi la Nigeria lilidai kuukamata tena mji wa Gwoza , katika jimbo la Borno, ambao kiongozi wa Boko Haram Abubakar Shekau alitangaza taifa la Kikhalifa mwaka jana na ambao ulikuwa unatambulika kama ngome ya kundi hilo.

Baadhi ya wakosoaji wamehisi hamasa za kisiasa katika tangazo hilo, pamoja na kuahirishwa kwa uchaguzi kwa wiki sita kuazia Februari 14 kutokana na misingi ya kiusalama.

Bado kuna hofu kwamba Boko Haram watafanya mashambulizi ya kujitoa muhanga pamoja na mabomu, ikiwa ni pamoja na katika vituo vya uchaguzi , hali iliyosababisha kuchukuliwa hatua kali ya usalama.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe

Mhariri: Iddi Ssessanga

Matangazo

IJUE DW

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com