1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanigeria wana matumaini ya kura yao

11 Aprili 2011

Baada ya wiki nzima ya kuahirisha uchaguzi tena na tena, hatimaye Wanigeria walikwenda kwenye visanduku vya kura hapo Jumamosi (09.04.2011) kuwachagua wabunge na maseneta wao. Mamia ya waangalizi wanashiriki.

https://p.dw.com/p/10rEf
Wapiga kura wakijipanga kwenye jimbo la Kano
Wapiga kura wakijipanga kwenye jimbo la KanoPicha: DW

Kijiji cha Sarbi kiko umbali wa mwendo wa saa moja kwa gari kutoka mji mkuu wa jimbo la Kaskazini la Kano. Nyuma kidogo ya mpindo wa Minjibir ndipo inapoishia barabara ya lami na kuanza mwendo mwengine wa nusu saa katika barabara ya mchanga.

Kulia na kushoto, ni uwanda wa ardhi iliyokauka, kiasi ya kwamba hata yale miti ya kijani na vichaka vimegeuka rangi kwa vumbi. Hapa na pale mbuzi wanaonekana wakinyofoa majani. Bado msimu wa kiangazi unalikumba eneo hili la Kaskazini mwa Nigeria.

Kijijini Sarbi, maafisa wa kura wameweka kituo chao kwenye skuli ya msingi, ambapo tayari watu wamejipanga katika mstari tangu mapema kwa ajili ya kutambuliwa.

Lakini hadi saa nne na nusu asubuhi, kuna majina machache tu ya wapiga kura yaliyoweza kuonekana kwenye daftari la wapiga kura.

Afisa wa kituo cha kura, Kano, Nigeria
Afisa wa kituo cha kura, Kano, NigeriaPicha: DW

Kwenye varanda, katika viti viwili wamekaa vijana wawili wa kiume na mwanamke mmoja, ambao kwa mavazi yao ya kimagharibi hawaonekeani kutokea eneo hili.

Kawaida maafisa wa kura huwa ni wanafunzi waliomaliza masomo na ambao sasa wanatumikia mwaka wao mmoja wa kujitolea. Nje, kuna wapiga kura wanaume na wanawake waliosimama au kukaa chini ya miti.

Hali ni ya kawaida. Polisi wawili wanarandaranda na silaha zao. Hata Aisha Ado Abdullhi anaonekana kuridhika. Leo yeye ni mwangalizi kwenye kituo hichi.

"Tunapaswa kuwapo hapa kabla ya kuwasili kwa maafisa wa Tume ya Uchaguzi saa moja asubuhi. Lakini leo tuna bahati kwamba maafisa wa Tume ya Uchaguzi wamefika mapema kiasi ya saa kumi na mbili, kwa hivyo tuliwakuta hapa. Walianza kazi kwa wakati kabisa, saa mbili asubuhi." Anasema Aisha.

Taasisi ya uangalizi ya NBA ni sehemu ya mradi ujuilikanao kama SWIFT Count. Kupitia kwa taasisi hii, jumuiya kadhaa zisizo za kiserikali nchi nzima zinashiriki kuangalia uchaguzi, kuona ikiwa unafanyika kwa haki na kwa sheria.

Aisha Ado Abdullahi, mwangalizi wa uchaguzi
Aisha Ado Abdullahi, mwangalizi wa uchaguziPicha: DW

Aisha Ado Abdullahi, mwanamke wa miaka 31 kutokea Kano, anatumia siku yake nzima leo akifanya kazi hiyo ya SWIFT Count kwenye kituo hiki cha kura.

"Tunapaswa kuangalia tu na sio kuingilia shughuli yao yoyote. Tunatakiwa tukae kuangalia hatua zote kuanza mwanzo hadi mwisho, hadi upigaji kura umemalizika na matokeo kubandikwa ukutani." Anasema Aisha.

Kubandika matokeo moja kwa moja kwenye vituo vya kura ni sheria mpya katika uchaguzi huu, ambapo sasa INEC inayoongozwa na Profesa Attahiru Jega inajikuta haina nafasi ya kuyavuruga matokeo haya kwenye makao makuu.

Wapiga kura pia wana imani kubwa na Profesa Jega, wakitarajia kuwa mara hii sauti yao itasikikana na wanasiasa watakaowachagua watawasilisha maslahi yao. Mmoja wao, ambaye ni mkulima, anasema anataka kuona kuwa kura yake inabadilisha mambo kwenye nchi yake.

"Tunataka usalama na hilo ndilo jukumu kubwa la nchi nzima. Serikali zilizopita zimeiba tu pesa za nchi hii. Tunataka pesa hizo zirudi kwa ajili ya skuli. Jeshi linahitaji uchunguzi, ili waweze kujifunza." Anasema mkulima huyo.

"Tunataka maendeleo. Maji salama, umeme, barabara." Anasema mwengine, ambaye ni msichana.

Skuli bora na mbolea kwa ajili ya mashamba yao, ndio matarajio pia ya wanakijiji wengine. Kwa ujumla, watu wamejitokeza kwa wingi zaidi kwenye vijiji vya eneo hili, kuliko ilivyokuwa miaka minne nyuma. Watu wanaonekana sasa wanauamini mchakato wa zoezi la kura.

Mwandishi: Thomas Mösch/ZPR
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Josephat Charo