Wanigeria wa mji wa Jos kufunga kwa siku tatu | Matukio ya Kisiasa | DW | 11.03.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Wanigeria wa mji wa Jos kufunga kwa siku tatu

Lengo ni kumuomba Mungu msamaha kutokana na mauaji

Wanawake wakiangua kilio baada ya kuona maiti huko Dogo Nahwa, Nigeria

Wanawake wakiangua kilio baada ya kuona maiti huko Dogo Nahwa, Nigeria

Wananchi wa Nigeria katika mji wa Jos kulikotokea mauaji ya watu zaidi ya 100 mwishoni mwa wiki, leo wameanza ibada ya siku tatu ya kufunga kwa ajili ya kumuomba mwenyezi Mungu msamaha pamoja na amani katika eneo hilo. Gavana wa jimbo hilo la Plateau ambako wakristo waliuwawa, Jonah Jang ametangaza hatua hiyo kwa lengo la kuwaleta pamoja wakaazi wa vijiji vilivyokumbwa na mkasa huo kumuomba Mungu.

Gavana wa jimbo la Plateau Jonah Jang amewatolea mwito wakaati wote wa eneo hilo kuanza hii leo kipindi cha funga ya siku tatu kwa ajili ya kumtaka msahama mola kwa madhambi yaliyotendeka mwishoni mwa wiki ambapo zaidi ya watu 100 waliuwawa kwa kukatwa katwa kwa mapanga na waislamu kutoka kabila la Fulani ambao kwa muda mrefu wamekuwa na uhasama na wakristo katika eneo hilo. Akitoa mwito huo kwa wakaazi gavana huyo ambaye ni kutoka kabila la Berom amesema kwamba Mwenyezimungu ni mtenda haki kila wakati na hivyo anaamini kilichotendekea kimetendeka kwa mapenzi yake na kwa sababu zake hivyo basi hawana budi kumshukuru na kumuomba mema.

Tukio hilo la kusikitisha limezusha hisia za uchungu takriban kila mahala kwani pamoja na waliouwawa ni watoto wachanga ambao hawana hatia. Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Benedicti wa 16 hapo jana alitoa matamshi ya kuyalaani maauaji hayo nchini Nigeria na kusema kwamba ni kitendo cha ukatili ambacho kinasikitisha sana. Mamia ya watu waliotoroka majumbani kwao wamepiga kambi katika vituo vya polisi mmoja wao akiwa ni Sam Alamda.

''Walikuwa wakifyatua risasi kutoka wakati huo niliingia na uwoga nikaanza kukimbia kuwafuata watu wanaokuja hapa. Milio ya risasi ikaongezeka kwa muda wa dakika 30''

Polisi nchini humo imesema kwamba watu 49 watashtakiwa kwa kuhusuka katika mauaji hayo. Duru za polisi zimearifu kwamba watu 109 waliuwawa Jumapili ingawa taarifa zilizotolewa awali na maafisa hao ni kwamba zaidi ya watu 500 waliuwawa katika tukio hilo la chinja chinja lililofanywa na waislamu wa kabila la Fulani kwenye vijiji vitatu vinavyokaliwa na idadi kubwa ya watu wa kabila la Berom ambao ni wakristo karibu na mji wa Jos mji mkuu wa jimbo la Plateau. Akizungumzia kinachoonekana kwa sasa katika eneo hilo muhubiri Mack Litbo aliyetembelea eneo hilo anasema-

''Tumekuja kujionea kilichotokea kama mnavyoona nyumba nyingi zimechomwa na kuna watu wengi walioachwa bila makaazi''

Kamati ya kimataifa ya shirika la msalaba mwekundu imesema kwamba kiasi cha wanigeria 8000 wameyatoroka makaazi yao karibu na mji wa Jos baada ya kuzuka ghasia hizo. Wakaazi wa eneo hilo wamesema kwamba mauaji hayo ni sehemu ya mvutano kati ya kabila la Fulani ambao ni wafugaji na kabila la watu wa Berom ambao ni wakulima ambayo yamekuwa yakichochewa na visa vya wizi wa mifugo.

Wimbi hilo la mauaji yaliyochukua muda wa saa tatu ndilo la hivi karibuni la mauaji ya kidini kuwahi kulikumba eneo hilo la Jos tangu mapigano ya mwezi Januari kati ya wakristo na waislamu ambapo mamia ya watu waliuwawa.

Mwandishi Saumu Mwasimba/AFPE

Mhariri Josephat Charo

 • Tarehe 11.03.2010
 • Mwandishi Saumu Mwasimba
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/MPb8
 • Tarehe 11.03.2010
 • Mwandishi Saumu Mwasimba
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/MPb8
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com