Wandani wa jadi wamepapuana? | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 29.05.2009
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Timu Yetu

Wandani wa jadi wamepapuana?

Rais wa Marekani Barack Obama katika jitahada za kusuluhisha mzozo wa Mashariki ya Kati, mara nyingine tena aliishinikiza Israel, lakini alikataa kupanga muda maalum wa kutekelezwa juhudi hizo za amani.

Rais Barack Obama na Rais wa Palestina Mahmoud Abbas katika Ikulu ya White House

Rais Barack Obama na Rais wa Palestina Mahmoud Abbas katika Ikulu ya White House

Siku ya Alkhamisi,Rais Obama alipokutana na Rais wa Wapalestina Mahmoud Abbas mjini Washington kwa mara ya kwanza tangu kuingia madarakani, alitoa mwito kwa Israel kusitisha ujenzi wa makaazi ya Walowezi wa Kiyahudi katika Ukingo wa Magharibi. Akakumbusha kuwa alipokutana na Netanyahu juma lililopita,alieleza waziwazi haja ya kusitisha ujenzi huo. Mara nyingine tena alisema, ni matumaini yake kuwa kutapatikana suluhisho la mataifa mawili ili kumaliza mzozo wa Waisraeli na Wapalestina. Siku ya Jumatano Israel ilipuuza mwito wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Hillary Clinton kuitaka Israel isitishe ujenzi wa makaazi ya walowezi wa Kiyahudi katika maeneo yaliyokaliwa.

Israelischer Außenposten Migron in der West Bank nahen Ramallah

Kambi ya Migron iliyo karibu na Ukingo wa Magharibi

Obama alipoulizwa iwapo Israel itashinikizwa kama itangángánia msimamo wake wa kupinga kuundwa kwa taifa la Palestina, alisema yeye anaamini kuwa ni muhimu kutaraji mema na sio kinyume chake. Akaongezea "Nina hakika kwamba Israel ikizingatia maslahi ya mkakati wake wa muda mrefu basi itatambua kuwa suluhisho la mataifa mawili ni kwa maslahi ya Waisraeli na Wapalestina."


Licha ya msimamo tofauti wa Israel, Obama alijaribu kuzuia malumbano zaidi. Alisema Israel ni mshirika wa dhati wa Marekani na ni kwa maslahi yao kuhakikisha ulinzi na usalama wake. Hapo akatoa mwito kwa Rais wa Wapalestina Mahmoud Abbas kushughulikia zaidi usalama katika Ukingo wa Magharibi na kuchukua hatua za kuzuia uchochezi wa hisia za chuki dhidi ya Waisraeli katika shule na misikiti. Wakati huo huo akamsifu Abbas kwa hatua alizochukua hadi sasa kuendeleza usalama na pia msimamo wake wa kuunga mkono taifa la Israel katika majadiliano yake na kundi la Kipalestina la Hamas.


Kwa upande wake Rais wa Wapalestina Mahmoud Abbas alisisitiza kuwa wao wamejizatiti kutimiza majukumu yao yote, kuambatana na Mpango wa Amani wa Mashariki ya Kati Road Map.


Mkutano huo pamoja na kiongozi wa Kipalestina umempa Obama fursa nyingine katika juhudi zake za kutaka kuufufua mchakato wa amani wa Mashariki ya Kati uliokwama. Juma lijalo mjini Riyadh,Rais Obama atakutana na Mfalme Abdullah bin Abdelaziz wa Saudi Arabia na mjini Cairo atatoa hotuba yake kwa Waislamu duniani. Hotuba hiyo inangojewa kwa hamu tangu muda mrefu.


Mwandishi:Prema Martin /ZPR

Mhariri:Othman Miraji

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com