1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanawake Afrika wapiga hatua

Mohamed Dahman
8 Machi 2017

Machi 8 ni Siku ya Wanawake Duniani. Afrika wamepiga hatua kubwa ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kushiriki kwa wingi katika mabunge kuliko hata Uingereza na Marekani lakini bado wanakabiliwa na changamoto.

https://p.dw.com/p/2YojC
Maandamano ya wanawake
Picha: Getty Images/AFP/A. Joe

Wanakabiliwa na changamoto za kukatisha tamaa za kuwepo kiwango kikubwa cha dhila za ngono,vifo vya uzazi na maambukizi ya virusi vya HIV,hayo yanabainishwa na ripoti iliyotolewa na Umoja wa Mataifa.

Ripoti hiyo inasema barani kote Afrika katiba,sheria na sera zina enzi kanuni ya usawa na kupinga ubaguzi katika haki za kiuchumi,kijamii na kitamaduni kwa wanawake.

Hata hivyo mapengo yaliyoko katika sheria na sera halikadhalika ukosefu wa utekelezaji na usimamizi unaimarisha ubaguzi dhidi ya wanawake. Kwa mfano ripoti hiyo inazitaja  nchi za Burundi, Guinea, Congo,Kenya,Mali, Sudan na Tanzania zote "zina kanuni za kifamilia na za kibinafsi ambazo zinawabagua wanawake katika masuala ya ndoa" na ni nchi tano tu za Afrika zina marufuku ya uhakika kushusu ndoa za wasichana wenye ulio chini ya miaka 18.

Ripoti hiyo iliyotolewa na ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia masuala ya haki za binadamu kabla ya kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake ambayo ni leo mchunguzi maalum wa  haki za wanawake wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika ametoa mapendekezo kadhaa kukuza usawa wa kijinsia.

Upinzani dhidi ya haki za wanawake

Mkuu wa haki za binaadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra'aad al-Husein ameonya katika ujumbe alioutoa hapo jana na hapa nanukuu " katika nchi nyingi hivi sasa tunashuhudia upinzani dhidi ya haki za wanawake,upinzani ambao unatuzuia sote "mwisho wa kunukuu.

Mkuu wa haki za binaadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra'aad al Hussein.
Mkuu wa haki za binaadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra'aad al HusseinPicha: Reuters/P. Albouy

Ametaja kurudi nyuma kwa sheria hivi karibuni katika sehemu nyingi duniani zenye lengo la kudhibiti na kupunguza maamuzi ya wanawake kuhusiana na miili yao na maisha yao kunakochochewa na mtazamo kwamba dhima ya mwanamke inapaswa kuwa ndogo ya kuzaa na kutunza familia.

Akitaja mfano wa Burundi Zeid amesema sheria dhidi ya ukatili wa wanawake imepiga hatua kwa njia nyingi kwa kule kuufanya ubakaji jeshini kuwa kosa la jinai na kupiga marufuku vitendo vyenye kudhuru hata hivyo sheria hiyo pia inawabebesha lawama wanawake wanaokabiliwa na ukatili chini ya misingi ya kijinsia kwa nguo wavaazo kukosa heshima au kwa kuwa na tabia mbaya isiokuwa na maadili.

Kwa upande mzuri ripoti hiyo juu ya "Haki za Wanawake Afrika" imesema kwamba kiuchumi kuna harakati kubwa za wanawake barani Afrika hususan wakiwa kama wakulima ,wafanyakazi na wajasiriamali kuliko mahala popote pale pengine duniani.

Mwandishi: Mohamed Dahman/AP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman