1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanawake 6 wenye ulemavu wa ngozi kuukwea Mlima Kilimanjaro

28 Septemba 2018

Wanawake hao kutoka nchi kadhaa za Kiafrika ambao wameushinda unyanyapaa, unyanyasaji, kubakwa na kushambuliwa kwa mapanga wanatarajiwa kuukwea mlima huo kuondoa dhana iliyoko kuhusu watu wa jamii yao.

https://p.dw.com/p/35ep0
Kilimandscharo Tansania
Picha: Roberto Schmidt/AFP/Getty Images

Wanawake hao wenye umri wa kati ya miaka 26 na 35 kutoka kenya, Nigeria, Afrika Kusini, Zimbabwe na Senegal shughuli hiyo ya siku saba ni ya kuwasherehekea watu wote wenye ulemavu wa ngozi. Mwanaharakati mmoja nchini Kenya na mmoja wa waanzilishi wa safari hiyo kwa jina 'Climb for Albinism' maana yake 'Kupanda Mlima kwa ajili ya Walemavu wa Ngozi' Jane Waithera amesema wamechoka kila mara kuambiwa kuwa hawawezi, wamelaaniwa na kwamba hawafai kuwa katika jamii.

Watu wenye ulemavu wa ngozi mara nyingi hutengwa na kushambuliwa katika bara la Afrika kutokana na kutokuwepo elimu sahihi kuhusu tatizo hilo la ngozi. Katika baadhi ya mataifa, wanawindwa kwa viungo vyao ambavyo hupelekwa kwa waganga wa kienyeji na watu wanaoamini vinaweza kuwapa utajiri au mafanikio.

Wanawake wenye ulemavu wa ngozi huwa katika hatari ya kubakwa kutokana na dhana potofu kwamba kushiriki ngono nao husaidia kuponya maradhi ya UKIMWI. Kuongezeka kwa mauaji dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi ambao viungo vyao hutumika kwa masuala ya kishirikina nchini Tanzania, Malawi na Burundi katika miaka ya hivi punde, kumesababisha Umoja wa Mataifa kumteua mtaalam maalum kuwalinda watu hao.

USA Prothesen für Kinder mit Albinismus aus Tansania
Pendo Noni,16, raia wa Tanzania aliyekatwa mkono mmoja, akiutizama mkono wake wa bandia.Picha: Reuters/C. Allegri

Baadhi ya wanawake hao wanasema hawakutambua hali yao ya ulemavu wa ngozi hadi walipobalekhe, na kupata wakati mgumu shuleni kutokana na matatizo ya kuona na kutoelewa sababu za kutokubaliwa kucheza nje kwani ngozi yao inaathirika wanapokuwa kwenye jua.

Mmoja wa wanawake hao kwa jina Staford anasema miaka kumi iliyopita, alikatwa mikono na wanaume watatu alipokuwa amelala na mwanawe wa kiume. Lakini alipata ufadhili na kuwekewa mikono bandia pamoja na mashine maalum ambayo aliitumia kuanzisha biashara ya kushona. Kwa sasa ni mwanaharakati anayefahamika nchini Tanzania.

Walianza majaribio kwa kuukwea Mlima Kenya

USA Prothesen für Kinder mit Albinismus aus Tansania
Picha: Reuters/C. Allegri

Wengine wamesimulia kuhusu jinsi walivyotelekezwa na wazazi wao walipozaliwa, au walivyobaguliwa shuleni, na hata kubakwa na kunyanyaswa kwa sababu ya ulemavu wao. Kuukwea Mlima Kilimanjaro hata hivyo huenda isiwe kazi rahisi kwao. Mnamo mwezi Mei mwaka huu, walifanya majaribio kwa kuukwea Mlima Kenya lakini wawili miongoni mwao walishindwa.

Wanawake hao sita watakaoukwea Mlima Kilimanjaro wamepewa miwani za jua na mafuta maalum ya kuyalinda macho yao na ngozi. Wana kundi la zaidi ya watu hamsini, daktari, wapokezi, walinzi pamoja na watunzi wa filamu. Wataanza safari yao tarehe Mosi Oktoba mwaka huu na kuendelea kuukwea mlima huo kila siku kwa kati ya saa nne na tano. Wanatarajia kufika kileleni Oktoba tarehe saba.

Mwandishi: Sophia Chinyezi/RTRE

Mhariri: Mohammed Khelef