1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mchakato wa amani ya Sudan Kusini kuendelea

2 Juni 2015

Wanasiasa watano wa upinzani waliotuhumiwa kupanga mapinduzi yaliyoshindwa mwaka wa 2013 nchini Sudan Kusini wamerejea nyumbani kutoka Kenya kufuatia mazungumzo yaliyofanywa chini ya upatanishi wa viongozi wa Afrika

https://p.dw.com/p/1FaWb
Riek Machar und Salva Kiir
Picha: Ashraf Shalzy/AFP/Getty Images

Kurejea kwao kumeongeza matumaini ya kupatikana amani licha ya kuripotiwa mapigano mapya karibu na visima vya mafuta vya nchi hiyo.

Wapinzani hao walionekana kuwa washirika wa kiongozi wa waasi Riek Machar wakati mapigano yalipozuka miongoni mwa majeshi ya serikali katika mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba mnamo Desemba 2013. Serikali ilidai njama ya kumpindua Rais Salva Kiir ilizimwa, na kuwazuilia washirika kadhaa wa Machar wakati machafuko yakisambaa kote nchini humo.

Chini ya upatanishi wa jumuiya ya ushirikiano wa nchi za mashariki na pembe ya Afrika IGAD, baadhi ya wapinzani hao waliachiliwa huru na kuhamishiwa Kenya. Na sasa wale waliorudi nyumbani jana pamoja ni Deng Alor Kuol, John Luk Jok, Kosti Manibe Ngai, Cirino Hiteng na Madut Biar. Wote ni mawaziri wa zamani waliohudumu katika serikali ya Kiir.

Südsudan Soldaten Rückeroberung Blue Nile Raffinerie
Mapigano bado yanaripotiwa kwenye visima vya mafutaPicha: picture-alliance/AA

Naibu rais wa Afrika Kusini Cyrile Ramaphosa, ni miongoni mwa viongozi wa Afrika walioandamana na wapinzani hao kwenda Juba na akawaambia waandishi wa habari kuwa kurejea kwao kunaashiria “siku kubwa ya amani nchini Sudan Kusini“. Kuol amesema wapinzano hao wamerejea nyumbani ili kushiriki mazungumzo ya kukiunganisha chama tawala na kumaliza vita katika taifa hilo.

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta anasema viongozi wa IGAD wataleta nguvu mpya kuzipa msukumo juhudi zilizokwama za kutaka kuukomesha mzozo wa Sudan Kusini ambao umedumu kwa miezi kumi na saba. "Mchakato wa IGAD utaanza tena mnamo Juni saba, ili kujaribu kuleta amani na utulivu kwa ndugu zetu wa Sudan kusini. Na tunapoanzisha mchakato huu, na nasema wazi huu sio uhitimisho, bali kuongezwa nguvu, kuwekwa pamoja michakato miwili ambayo imeendelea sambamba ikiwa na matumaini ya kuhakikisha kuwa Wasudan Kusini wanaweza kunufaika, wanaweza kufurahia uhuru, na mafanikio ambayo wangeyapata tokea mwanzo".

Wakati huo huo, Sudan Kusini imeamua kumtimua mratibu wa misaada wa Umoja wa Mataifa Toby Lanzer wiki chache tu kabla ya kuondoka ili kupewa majukumu mengine.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon alilaani hatua hiyo na kutoa wito kwa serikali kuubatilisha maramoja uamuzi huo dhidi ya Lanzer, raia wa Uingereza ambaye pia alihudumu kama naibu wa balozi wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini. Lanzer alikuwa anakaribia kukamilisha muhula wake na Eugine Owusu wa Ghana tayari alikuwa ameteuliwa kuchukua nafasi yake.

Hakuna sababu iliyotolewa kwa kutimuliwa kwake, lakini maafisa wa Umoja wa Mataifa wamedokeza kuwa ukosoaji unaofanywa dhidi ya serikali na waasi kuhusiana na kuongezeka kwa mapigano huenda uliikasirisha serikali ya Kiir.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Iddi Ssessanga