1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanasiasa Ulaya waeleza matumaini kuhusu virusi vya corona

Yusra Buwayhid
14 Aprili 2020

Wanasiasa barani Ulaya waeleza matumaini huenda maambukizi ya virusi vya corona yakawa yamefikia kilele chake. Ufaransa itaendelea na hatua za tahadhari hadi Mei 11, huku Ujerumani ikitafakari kufungua tena shule.

https://p.dw.com/p/3ar2N
Frankreich | Corona-Pandemie | TV Ansprache Präsident Macron
Picha: picture-alliance/abaca/Balkis Press

Ufaransa imeongeza muda wa kuendelea kuchukua tahadhari za kudhibiti maamukizi ya virusi vya corona hadi Mei 11. Rais Emmanuel Macron amesema ifikapo tarehe hiyo shule zitaanza kufunguliwa. Jumatatu Ufaransa imeripoti vifo 574 vinavyotokana na maambukizi ya virusi hivyo, na kuifanya idadi jumla ya vifo kufikia watu15,000. Hata hivyo, idadi ya wagonjwa wa COVID-19 wanaohitaji uangalizi maalumu imepungua kwa siku ya tano mfululizo. Macron amesema kasi ya janga hilo inaanza kupungua na dalili za kudhihirisha hilo ziko wazi. "Mei 11 itakuwa mwanzo wa awamu mpya. Sheria zinaweza kubadilishwa kulingana na hali itakavyokuwa," aliongeza Macron.

Tangazo hilo la Macron limetolewa baada ya Shirika la Afya Ulimwenguni WHO kusema kwamba kuondoa vizuizi vilivyowekwa mapema sana kunaweza kuleta wimbi la pili la maambukizi, na kuonya kuwa chanjo tu ndio itazuia kabisa kuenea kwa ugonjwa wa COVID-19.

Serikali mbalimbali kote ulimwenguni ziko chini ya shinikizo la kuokoa uchumi wa dunia usije kuanguka kabisa kwa sababu ya kufungwa kwa biashara na watu kulazimika kubakia majumbani, lakini viongozi pia wanajaribu kuzuia wimbi la pili la ugonjwa huo.

Huko Uhispania, ambako zaidi ya watu 17,000 wamekufa, wajenzi na wafanyakazi wa viwandani waliruhusiwa kurudi kazini Jumatatu na polisi walikuwa wakiwakabidhi maski za kufunika uso kwenye vituo vya treni.

BG | Bau von temporären Coronavirus Kliniken | Spanien - Madrid
Vitanda vikitayarishwa mjini Madrid kupokea wagonjwa wa COVID-19 katika hospitali ya kijeshi.Picha: Reuters/Comunidad de Madrid

Na Italia itaanza jaribio la kufungua tena maduka ya vitabu pamoja na sehemu za kufua nguo siku ya Jumanne, ingawa imeshatangaza rasmi kuongeza muda wa kuendelea na hatua za tahadhari hadi Mei 3. Italia ni nchi ya pili iliyopigwa vibaya na janga la maambukizi ya virusi vya corona - inayoongoza ni Marekani - na idadi jumla ya vifo vilivyorekodiwa hadi Jumatatu ni 20,000. Hata hivyo idadi ya wagonjwa walio katika hali mbaya imepungua kwa siku ya 10 mfululizo.

Wakati huo huo nchini Uingereza watu waliokufa kutokana na ugonjwa wa COVID-19 wamefika hadi 11,329 Jumatatu. Uingereza ni nchi ya tano duniani yenye idadi kubwa ya vifo vinavyotokana na maambukizi ya virusi vya corona.

Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Dominic Raab ambaye amekuwa akikaimu nafasi ya uwaziri mkuu ya Boris Johnson amesema kuna dalili za matumaini zinazoonyesha Uingereza imeanza kufanikiwa kupambana na janga la maambukizi ya virusi vya corona. Lakini Raab pia amekiri itachukuwa muda kufikia hatua hiyo.

Bildergalerie der Reise Lonely Places
Jiji la Paris likiwa tupu wakati wa COVID-19Picha: picture-alliance/Photoshot/Tang Ji

Nchini Ujerumani taasisi kuu ya kisayansi Leopoldina imesema shule zinaweza polepole kuanza kufunguliwa huku tahadhari za kujikinga na virusi hivyo zikiendelea kuzingatiwa. Maduka na mikahawa pia inaweza kuanza kufunguliwa, iwapo sheria ya kuweka umbali kutoka mtu mmoja hadi mwengine itakuwa inatekelezwa. Taasisi hiyo pia imesema watu watalazimika kuvaa maski za kufunika mdomo na pua. Na ingawa ofisi za serikali zinaweza kufunguliwa, safari na hafla za mikusanyiko ya watu wengi zinapaswa kuruhusiwa polepole na kwa tahadhari kubwa.

Mapendekezo ya taasisi hiyo yatatiliwa manani wakati wa kufanya uamuzi Jumatano na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na wakuu wa majimbo 16 ya Ujerumani, kama kuna haja ya kuongeza muda wa kuendelea kutekeleza vizuizi vilivyowekwa katikati mwa mwezi Machi ambao unatarajiwa kumalizika Jumapili.

Lakini shirika la WHO limeendelea kuonya dhidi ya kuondoa vizuizi vilivyowekwa likisema hakuna suluhisho lingine zaidi ya chanjo ambayo inaweza kuchukuwa mwaka mzima hadi kupatikana.

Vyanzo: (AFP,DW)