Wanasiasa Kenya waonywa kutowachochea raia kuhusu sensa | Matukio ya Afrika | DW | 28.08.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Wanasiasa Kenya waonywa kutowachochea raia kuhusu sensa

Mkuu wa usalama katika eneo la Rift Valley amewataka wanasiasa kukoma kabisa kuwachochea wananchi wasihesabiwe kwenye zoezi la sensa linaloendelea.

Kamishina wa eneo la  Rift valley amewaonya wanasiasa dhidi ya kuwachochea watu wasihesabiwe katika zoezi la sensa linaloendelea nchini Kenya. Mkuu huyo anawataka wanasiasa wakome kuwaambia watu warejee katika kaunti na maeneo bunge yao wenyeji.

Haya yanajiri huku viongozi wawili waliokamatwa katika eneo la Baringo wakisubiri kufunguliwa mashtaka hii leo kwa kuwachochea wakaazi dhidi ya sensa.

Ripoti za wanasiasa kuwachochea watu katika baadhi ya maeneo nchini zinatatiza zoezi la sensa linaloendelea nchini Kenya. Hii leo mwakilishi wa wadi ya Illchamus Joseph Leparsalach na chifu wa eneo la Salabani Francis Olekipirich wanafikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya uchochezi baada ya kukamatwa wikendi iliyopita huko Baringo. Moses Ole Mpaka mratibu wa kitengo kinachoshughulikia maswala ya jamii za wachache na zilizotengwa katika afisi ya naibu Rais anasema baadhi ya wanasiasa wanatumia zoezi hili kuwashawishi na kuwahamisha watu wahesabiwe katika maeneo yao.

Mkuu wa eneo la bonde la ufa George Natembeya amewaonya wanasiasa dhidi ya kuwachochea watu akisema. Akizungumza sababu zinazowafanya wanasiasa kuwahamisha watu, Natembeya amesema kila mtu atahesabiwa pale alipo na kwamba wanasiasa wakome kuwaambia watu warejee katika maeneo yao wenyeji kuhesabiwa huko.

 

Afisa wa kuhesabu watu Kenya akimuuliza maswali mkaazi mmoja wa Nairobi wakati wa zoezi la kuhesabu watu, sensa.

Afisa wa kuhesabu watu Kenya akimuuliza maswali mkaazi mmoja wa Nairobi wakati wa zoezi la kuhesabu watu, sensa.

Natembeya amewaonya wanasiasa na kuwaambia "Tabia duni zinalemaza taifa leo hata kwenye maswala ya siasa, tunapoteza muda mwingi tukifanya mambo yasiyofaa. Serikali inataka kujua idadi ya watu ndio iweze kumpangia kila mwananchi, haijalishi uko wapi. Kama eneo bunge lako limepangiwa kuondolewa, litaondolewa. Kwa sababu ukijihusisha na tabia hiyo ya kuwahamisha watu waje katika eneo lako la uwakilishi kuna uwezekano kuwa kuna mtu mwingine pia anawahamisha watu kutoka kwenye eneo lako la uwakilishi. Kwa hivyo tunajihusisha na shughuli zisizo na manufaa. Muhimu zaidi ni kwa viongozi kujitokeza kuwahimiza watu wajitokeze katika zoezi hili la sensa."

Kumekuwa na wasiwasi kati ya wakenya kuhusu muda waochukua maafisa wanaotekeleza zoezi la sensa, baadhi wakidai hawajafikiwa na kuhesabiwa. Natembeya anawasihi wakenya kuwa na subira akikariri kuwa zoezi la mwaka huu linahusisha taarifa nyingi kutoka kwa watu.

Vilevile akizungumza maswali yanayoulizwa kwenye sensa, kamishna wa kaunti ya Nakuru Erastus Mbui anawataka wakenya kutoyapuuza na badala yake kushirikiana na maafisa wa sensa kwa minajili ya mipangilio ya Taifa.

Zoezi la sensa nchini Kenya lilianza tarehe 24 mwezi huu na linatarajiwa kukamilika tarehe 31 mwezi huu.