Wanasheria washambuliwa na majaji kuzuiliwa kutoka nje | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 05.11.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Wanasheria washambuliwa na majaji kuzuiliwa kutoka nje

Maelfu ya polisi wamepambana na wanasheria wanaoandamana kupinga hatua ya Rais Pervez Musharraf ya kutangaza hali ya hatari.Wakati huohuo majeshi ya usalama yanatia juhudi kudhibiti mahakama mjini Lahore huku majaji kadhaa kuzuiwa kutoka majumbani mwao baada ya kukataa kuahidi kutii amri baada ya tukio hilo la mwishoni mwa wiki.

Waandamanaji mjini Lahore

Waandamanaji mjini Lahore

Rais Musharraf alitangaza hali ya hatari mwishoni mwa juma lililopita kwa madai ya ongezeko la ghasia na vurumai nchini humo.Polisi walifyatua gesi ya machozi na kupambana na wanasheria hao wanaopinga hali ya hatari.Yapata watu 350 wanazuiliwa.Takriban wanasheria alfu 2 walikusanyika katika mahakama kuu mjini Lahore na kuvamia na mamia ya polisi baada ya kukiuka agizo la kutoandamana.

Polisi hao walifyatua gesi ya machozi walipojaribu kuelekea barabarani nao waandamanaji wakalipiza kisasi kwa kurusha mawe na kuwapiga kwa matawi.Ghasia zinaropotiwa kutokea mjini Karachi na Multan ambako wanasheria katika miji mikubwa wanajaribu kuandamana kupinga hatua ya Rais Musharraf.

''Maslahi ya Pakistan ndio yako mstari wa mbele ila fikra za wengine hazina nafasi. chochote ninachokifanya ni kwa manufaa ya Pakistan.Wakosoaji wafahamu kwamba wasitarajie demokrasia kama wanavyoifahamu wao waliyojifunza katika kipindi cha miaka kadhaa.Sisi pia tunajifunza na nadhani tumepiga hatua.''

Hali ya hatari ilitangazwa mwishoni mwa juma lililopita huku Rais Musharraf akidai kuwa ghasia na visa vya uasi vimeongezeka nchini humo.Katiba ya nchi hiyo aidha imesimamishwa jambo linalolazimu uchaguzi kuahirishwa.Shaukat Aziz ni waziri mkuu wa Pakistan

''Kukiwa na hali ya hatari bunge linaweza kujipa muda zaidi..mpaka mwaka mmoja ndipo kufanya uchaguzi ujao.Hata hivyo hakuna uamuzi wowote uliotolewa kwa sasa.Tunatia juhudi zote kuhakikisha kuwa uchaguzi unafanyika na demokrasia inadumishwa.Kulingana na yaliyotokea huenda muda wa kufanya hilo ukabadilika ''

Rais Musharraf aliahidi kujiuzulu kama mkuu wa majeshi punde baada ya kuteuliwa tena.Kauli hiyo kwa sasa huenda isitimizwe kufuatia hali ya hatari kutangazwa kwa mujibu wa naibu waziri wa habari Tariq Azeem.Rais Musharraf aliyeingia madarakani mwaka 99’ baada ya kupindua uongozi wa wakati huo aliahidi mwezi Septemba kujiuzulu kama mkuu wa majeshi kabla kuapishwa tena baada ya uchaguzi wa rais wa mwezi Oktoba.Hilo lilitarajiwa kufanyika tarehe 15 mwezi huu wakati ambapo muhula wake unakamilika.Uamuzi wa mahakama kuu kuhusu uhalali wa ushindi huo bado unasubiriwa na kudhaniwa kuchangia hali hiyo ya hatari kutangazwa.Vyama vya upinzani vinapinga vikali hatua hiyo ya Rais Musharraf.Bi Benazir Bhutto Waziri mkuu wa zamani aliyekuwa uhamishoni kwa yapata miaka minane anashiriki katika uchaguzi unaosubiriwa

''Naelewa kwamba Jenerali Musharraf anasisitiza kuwa maslahi ya Pakistan yawe mstari wa mbele ila siamini kuwa uamuzi wa mtu mmoja utafanikisha hilo na ni makosa kwa Rais Musharraf kufanya uwamuzi wa binafsi.Hilo ni jambo ambalo raia wa Pakistan sharti waamue kwa pamoja.''

Kwa upande mwingine Marekani iliyo mwandani wa rais Musharraf inasitisha mazungumzo ya usalama na Pakistan na kutoa wito wa demokrasia kudumishwa haraka iwezekanavyo.Mazungumzo hayo ya siku mbili yalipangwa kuanza hapo kesho.Jamii ya kimataifa inashtumu vikali hatua ya Rais Musharraf ya kutangaza hali ya hatari.Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bi Condoleeza Rice hapo jana alieleza wasiwasi wake.

''Ni kwa manufaa ya nchi ya Pakistan na raia wake kurejelea mfumo unaotilia maanani katiba ili kuwezesha uchaguzi kufanyika na bunge jipya kuchaguliwa.Aidha wahusika wote wajizuie katika hali hii ngumu inayowakumba ''

Majaji kadhaa wanazuiliwa majumbani mwao baada ya kukataa kuahidi kushirikiana na serikali baada ya hali ya hatari kutangazwa.Baadhi ya walioweza kutoka nje walizuiliwa kuingia mahakamani.Polisi wanashika doria nje ya nyumba za majaji hao mjini Islamabad huku Rais Musharraf akitoa agizo la majaji hao kuapishwa tena au kutimuliwa.Wengi ya wanasheria hao wanakataa kuapishwa.

 • Tarehe 05.11.2007
 • Mwandishi Thelma Mwadzaya
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/C77F
 • Tarehe 05.11.2007
 • Mwandishi Thelma Mwadzaya
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/C77F

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com