1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanandoa Uingereza washambuliwa na sumu ya Novichok

Lilian Mtono
5 Julai 2018

Polisi Jijini London, Uingereza imethibitisha kwamba raia wawili waliokutwa wakiwa katika hali mbaya, kwenye mji wa Amesbury wameathirika na sumu ya kuua mishipa ya fahamu aina ya Novichok.

https://p.dw.com/p/30rr1
Großbritannien Vergiftungen in Wiltshire
Picha: picture-alliance/empics/Y. Mok

Polisi Jijini London, Uingereza imethibitisha kwamba raia wawili waliokutwa wakiwa katika hali mbaya, kwenye mji wa Amesbury wameathirika na sumu ya kuua mishipa ya fahamu aina ya Novichok. Ufichuzi huo unafuatia uchunguzi uliofanywa na maabara ya kijeshi ya Porton Down.

Matokeo hayo ya kimaabara yaliyotolewa jana jioni, yalithibitishwa na kamishna msaidizi wa polisi, kitengo cha kupambana na ugaidi, Neil Basu, kupitia taarifa iliyotolewa kwenye ukurasa wa twitter. Amesema wagonjwa hao ambao ni wanandoa, bado wamelazwa hospitalini wakiwa katika hali mbaya.

Alirejelea sehemu ya uchunguzi wa shambulizi hili la karibuni, na kama linahusian na lile lililofanywa dhidi ya jasusi wa zamani wa Urusi Sergei Skripal, na binti yake Yulia mjini Salisbury mnamo mwezi Machi, na kuibua vita vya kidiplomasia baada ya Uingereza kuituhumu Urusi kwa shambulizi hilo, huku Urusi ikikana. Amesbury iko umbali wa kilomita 10 kutoka Salisbury.

Naibu kamishina Basu amesema, baada ya uchunguzi wa awali, ilidhaniwa kwamba wagonjwa hao wawili waliugua baada ya kutumia dawa  zilizoharibika. 

Großbritannien Vergiftungen in Wiltshire
Baadhi ya maeneo ambayo wanandoa hao walitembelea yamefungwa na polisi kwa uchunguzi wa kisa hicho.Picha: Reuters/J. Nicholls

Hata hivyo hospitali ambako walilazwa wagonjwa hao, ililazimika kutuma sampuli zao kwenye maabara ya kijeshi ya Porton Down kwa uchunguzi zaidi, kufuatia dalili zilizotia wasiwasi mnamo siku ya Jumatatu, na ndipo hatimaye polisi ilithibitisha waliathiriwa na sumu ya Novichok, sawa na ile iliyotumika kwenye shambulizi dhidi ya Skripal na bintiye Yulia.

Kulingana na Basu, kikosi cha wachunguzi 100 kutoka mtandao wa kipolisi wa kupambana na ugaidi na polisi ya London inayoongoza katika masuala ya kupambana na ugaidi walikuwa wanashirikiana kuchunguza tukio hilo.

Naibu mkuu wa polisi wa Wiltshire Paul Mills amewaambia waandishi wa habari kwamba wagonjwa hao wote wawili ambao wanaendelea kupata matibabu ni raia wa Uingereza, na polisi imeyafunga baadhi ya maeneo ambayo wenza hao waliyatembelea kabla ya kukutwa wakiwa hawajitambui, ambayo ni pamoja na duka na kanisa.

Msemaji wa kitengo cha huduma za afya kwa umma nchini humo amesema kwenye taarifa yake kupitia jeshi la polisi kwamba hakukua na hatari yoyote ya kiafya kwa umma kufuatia tukio hilo.

Waziri wa mambo ya ndani wa Uingereza Sajid Javid alisema ataongoza kikao cha dharura cha baraza la mawaziri hii leo na taarifa nyingine zilisema atatoa taarifa bungeni juu ya kisa hicho, huku msemaji wa waziri mkuu Theresa May akisema, May amekuwa akiarifiwa kila mara kuhusu suala hilo.

Mwandishi: Lilian Mtono/DPAE/AFPE/DW

Mhariri: Caro Robi