1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wananchi wa Libanon waombwa kubakia shwari

13 Desemba 2007
https://p.dw.com/p/CazN

NEW YORK:

Shambulizi la bomu lililomuua jemadari wa ngazi ya juu nchini Libanon,siku ya Jumatano limelaaniwa na jumuiya ya kimataifa.Brigedia Jenerali Francois al-Hajj na watu 3 wengine waliuawa katika shambulizi hilo karibu na makao rasmi ya rais katika mji wa Baabda,mashariki mwa mji mkuu Beirut.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,Ban Ki Moon ametoa mwito kwa wananchi wa Lebanon kubakia shwari ili kuzuia mgogoro wa kisiasa nchini humo kuwa mkubwa zaidi.Wakati huo huo Kansela wa Ujerumani,Angela Merkel amesema,ni matumaini yake kuwa waliohusika na shambulizi hilo wataadhibiwa haraka.

Marehemu al-Hajj alitazamiwa kumrithi Jenerali Michel Suleiman kama mkuu wa majeshi,iwapo juma lijalo,Suleiman atachaguliwa kama rais mpya wa Libanon.Kufuatia shambulizi la Jumatano,hali ya mvutano imezidi kuwa mbaya katika nchi ambako viongozi wanaohasimiana,wanashindwa kuafikiana kuhusu uchaguzi wa rais mpya.