1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanamichezo wa Urusi katika hali ngumu

22 Julai 2016

Baada ya wanamichezo wa Urusi kushindwa katika juhudi zao za kutaka hatua ya kufungiwa kushiriki Olimpiki ibatilishwe, sasa hatima yao iko mikononi mwa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki – IOC

https://p.dw.com/p/1JUMD
Symbolbild Leichtathletik Russland Doping
Picha: picture-alliance/AP Photo

IOC inapaswa kufanya uamuzi wa kama iitimue timu nzima ya Urusi katika michezo hiyo inayoanza mjini Rio de Janeiro katika siku 14 zijazo.

Mahakama ya juu kabisa michezoni ilitupilia mbali ombi lililowasilishwa na wanamichezo 68 wa Urusi la kupinga hatua ya kupigwa marufuku iliyotangazwa na Shirika la Kimataifa la Riadha – IAAF kufuatia tuhuma za kukithiri utumiaji wa dawa za kuongeza misuli nguvu unaofadhiliwa na serikali. Maafisa wa michezo nchini Urusi wameilaani hukumu hiyo wakiitaja kuwa ya “kisiasa”. Vitaly Mutko ni waziri wa michezo wa Urusi "Nimechukizwa sana na tabia ya IAAF. Ningependa kusisitiza kuwa IAAF ilipatikana na hatia ya ufisadi na rais wake akachunguzwa na sasa yuko katika kifungo cha nyumbani nchini Ufaransa. Lakini watu waliounda, kuongoza na kuuficha mfumo wa kudhibiti matumizi ya dawa za kuongeza misuli nguvu wanaendelea na kazi – naibu mkurugenzi wa idara, Rais wa IAAF Sebastian Coe. Kutokana na uamuzi dhidi ya Urusi, wanajaribu kujiondolea lawama".

Schweiz IOC - PK in Lausanne - Präsident Thomas Bach
IOC itaamua hatima ya Urusi katika OlimpikiPicha: Reuters/D. Balibouse

Jopo hilo la majaji watatu katika Mahakama ya Usuluhishi wa migogoro michezoni – CAS lilitoa uamuzi kuwa Kamati ya Olimpiki ya Urusi “haina haki ya kuwapeleka wanamichezo wa Urusi kushiriki katika Michezo ya Olimpiki ya Rio 2016 ikizingaziwa kuwa hawana kibali cha kushiriki chini ya sheria za IAAF”. Katika kesi yao, Warusi walihoji kuwa sio haki kutoa marufuku ya jumla, wakisema inawaadhifu wanamichezo ambao hawajatuhumiwa kufanya makosa yoyote. Rais wa IAAF alisema marufuku hiyo ni muhimu kulinda hadhi ya mashindano ya Olimpiki.

Mutko amesema Urusi huenda ikawasilisha kesi hiyo katika Mahakama ya kesi za kiraia. Kaatibu Mkuu wa Mahakama ya Usuluhishi wa migogoro michezoni – CAS Matthieu Reeb amesema Warusi wana haki ya kukata rufaa katika mahakama hiyo maalum ya Uswisi ndani ya siku 30, lakini kwa misingi ya kiutaratibu na wala sio uhalali wa uamuzi wa CAS. Bodi Kuu ya IOC inatarajiwa kuandaa mkutano mwingine wa dharura kesho Jumapili ili kutathmini suala hilo la Urusi. Craig Reedie ni rais wa Shirika la Kimataifa la Kupambana na matumizi ya Dawa zilizopigwa marufuku michezoni - WADA

Urusi sio nchi pekee yenye tatizo hilo. Lakini sasa sidhani kama kuna nchi nyingine yenye tatizo la aina hiyo la dawa za kuongeza misuli nguvu linalopangwa na serikali. Huu ni mfano wa kushangaza wa udanganyifu. Ulidumu kwan miaka minne. Ulichafua mashindano ya riadha ya dunia, Michezo ya Olimpiki ya LONDON, michezo ya vuo vikuu duniani

China Leichtathletik-WM in Peking Ussain Bolt
Usain Bolt anasema hatua kali inapaswa kuchukuliwaPicha: Reuters/D. Martinez

Urusi sio nchi pekee yenye tatizo hilo. Lakini sasa sidhani kama kuna nchi nyingine yenye tatizo la aina hiyo la dawa za kuongeza misuli nguvu linalopangwa na serikali. Huu ni mfano wa kushangaza wa udanganyifu. Ulidumu kwan miaka minne. Ulichafua mashindano ya riadha ya dunia, Michezo ya Olimpiki ya LONDON, michezo ya vuo vikuu duniani

Kundi la mashirika 14 ya kitaifa ya kupambana na dawa za kuongeza misuli nguvu limetuma barua kwa Rais wa IOC Thomas Bach likimtaka atangaze marufuku kamili “ili kutetea mkataba wa Olimpiki na uadilifu wa Michezo ya Olimpiki ya Rio”. Miongoni mwa nchi zilizowakilishwa katika barua hiyo ni Marekani, Canada, Ujerumani, New Zealand na Austria.

Bolt na Farah waunga mkono hatua hiyo

Mwanariadha wa kasi zaidi ulimwenguni Mjamaica Usain Bolt anasema hatua iliyochukuliwa dhidi ya Urusi ni nzuri kwa maafisa wa riadha kutuma ujumbe mzito dhidi ya uovu huo. "Kwangu mimi, kama una ushahidi na unaweza kumnasa mtu, nahisi kuwa unapaswa kuchukua hatua na kama unahisi kuipiga marufuku timu nzima ndiyo hatua sahihi basi naunga mkono. kama nilivyosema, sheria ni sheria na matumizi ya dawa za kuongeza misuli nguvu yamekithiri. ukitaka kutuma ujumbe mzito basi ni vyema.

Naye Mwanariadha wa Uingereza, bingwa wa Olimpiki Mo Farah pia amezungumzia suala hilo akisema anataka tu kushindana na wanariadha safi. "Kama nilivyosema, hatutaki kuona kitu chochote kibaya katika mchezo wetu. mimi na Usain Bolt na wenzetu wengine, tufanya kazi kwa bidii na kisha kitu kama hiki kikitokea kinatuondolea sifa. Hivyo, hakuna anayetaka kuona hilo. Unapaswa kufanya kilicho sahihi na tunaliachia shirika linalohusika na watu ambao kazi yao ni kuleta usawa michezoni.

Mwandishi: Bruce Amani/DPA/Reuters/AFP
Mhariri: Iddi Sessanga