Wanamibia waishitaki Ujerumani | Matukio ya Kisiasa | DW | 06.01.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Wanamibia waishitaki Ujerumani

Wawakilishi wa makabila mawili nchini Namibia wamefungua kesi katika mahakama nchini Marekani dhidi ya Ujerumani wakidai fidia kwa madai ya mauaji ya halaiki yaliyofanywa na watawala wa zamani wa wakoloni wa kijerumani.

Kesi hiyo ambayo imefunguliwa mjini New York na wawakilishi wa kabila la Ovaherero na Nama, inadai pia wawakilishi wao kujumuishwa katika majadiliano juu ya jambo hilo baina ya Ujerumani na Namibia.

Nchi hizo mbili zimekuwa katika mazungumzo kuhusu azimio la pamoja la mauaji ya halaiki ya mwaka 1904 na 1905, wakati  Ujerumani imekubali kuwa mauaji hayo yalitokea lakini mara kadhaa imekataa kulipa fidia.

Mmoja kati wa walalamikaji ambaye ni chifu mkuu wa watu wa kabila la Ovaherero Vekuii Rukoro amezungumzia kauli hiyo kwa kusema.

"Tunafahamu kwamba wanachotaka kukisema ni kuomba radhi bila kulipa fidia, kama hiki ndicho serikali ya Ujerumani inakusudia kufanya, tutawaomba wawakilishi wa watu wa Ujerumani wanaokutana katika Bundestag kuukataa kabisaa msimamo huu wa serikali kwa sababu litakuwa tusi siyo tu kwa akili za Wanamibia na vizazi vya jamii zilizoathirika, bali pia kwa Afrika yote na kwa ubinaadamu".

 Namibia Vekuii Rukoro Stammesoberhaupt der Herero (picture-alliance/dpa/J. Bätz)

Mmoja kati ya walalamikaji katika kesi hiyo Chifu Vekuii Rukoro

Walalamikaji wamesema, wamefungua kesi hiyo ya kudai hatua zichukuliwe na kutaka fidia ya mauaji kwa niaba ya watu ambao waliteseka katika mikono ya wakoloni wa mamlaka ya kijerumani. Pia wameongea kuwa wanataka azimio kuhusu haki yao kujumuishwa katika majadiliano kati ya Ujerumani na Namibia na kuongeza kuwa hakuna makubaliano yanayoweza kufikiwa bila wao kuwa kati ya watakaotia saini.

Historia ya kesi hiyo

Mgogoro huo unarudisha kumbukumbu za kipindi cha kati ya mwisho wa karne ya 19 na mwanzoni mwa karne ya 20 wakati  eneo la Kusini Magharibi mwa Afrika, ambayo sasa inatambulika kama Namibia ilipokuwa chini ya utawala wa kikoloni wa Ujerumani.

Kesi hiyo inadai kuwa mwaka 1885 mpaka mwaka 1903 robo ya eneo la Ovaherero na Nama lilichukuliwa  na walowezi wa Kijerumani kwa ridhaa ya utawala wa kikoloni wa Wajerumani pasipo kulipa fidia.

Madai mengine ni kuwa, mamlaka za wakoloni wa kijerumani zilifumbia macho vitendo vya ubakaji na kuwafanyisha kazi za lazima  wanawake na watoto wa kike wa makabila hayo ambavyo vilifanywa na wakoloni.

Kesi hiyo inadai kuwa karibu watu 100,00 wa makabila hayo walifariki  katika kampeni ya kuwaangamiza ambayo iliongozwa na  Generali wa kijerumani Lothar Von Trotha. Walalamikaji katika kesi hiyo ni pamoja na Vekuii Rukoro ambaye ametambuliwa kama chifu mkuu wa kabila la Ovaherero na David Fredrick chifu na mwenyekiti wa mamlaka ya muungano wa jadi wa Nama.

Mwandishi: Celina Mwakabwale/AFP

Mhariri:Iddi Ssessanga

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com