1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanamgambo wa Ethiopia walaumiwa kwa mashambulio ya kigaidi

Amina Mjahid
1 Aprili 2021

Maafisa nchini Ethiopia wamesema kundi la waasi katika jimbo la Oromia, limetekeleza shambilizi la kigaidi wiki hii na kusababisha vifo vya watu wengi ambao idadi yao hadi sasa haijajulikana

https://p.dw.com/p/3rToH
Weltspiegel 01.03.2021 | Äthiopien Tigray | Trauer um Toten
Picha: Eduardo Soteras/AFP/Getty Images

Katika taarifa iliyotolewa na serikali ya jimbo la Oromia, shambulizi hilo lilitokea katika eneo la Magharibi la  Wollega ambako wanajeshi wa Ethiopia wamekuwa wakipambana na kundi la wanamgambo linalojiita jeshi la ukombozi la Oromo.

Taarifa hiyo ilisema licha ya wanamgambo hao kudhoofishwa na mikakati inayochukuliwa na serikali dhidi yao, pamoja na jamii ili kuhakikisha utawala wa sheria unafuatwa, bado linaendelea kutekeleza mashambulizi kwa raia wa eneo hilo.

Hata hivyo maafisa wa mawasiliano wa jimbo hilo, hawakutoa maoni yoyote kuhusu yale yanayoendelea katika jimbo hilo la Oromia na taarifa yao haikujumuisha maelezo zaidi ya waathiriwa au namna shambulizi lilivyotekelezwa.

Lakini mkaazi mmoja katika wilaya ya Babo-Gembel kulikotokea shambulizi, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba watu waliojihami kwa bunduki walifika saa tatu asubuhi siku ya Jumanne, wakawalazimisha wakaazi kukusanyika nje kwa makundi na kuwaua kwa kuwapiga risasi.

Mtu huyo ambaye ni mlinzi katika kanisa la Orthodox ambaye hakutaka kujulikana, aliendelea kusema kuwa eneo hilo halikuwa na ulinzi wowote kutoka kwa maafisa wa usalama wakati wa tukio, na alikutana na miili 29 iliyokuwa katika sehemu moja huku miili mingine ikiwa imetapakaa katika maeneo mengine.

Vurugu za kikabila zazidi kueleakea uchaguzi mkuu

Sudan Äthiopische Flüchtlinge Tigray Um Raquba
Picha: Hussein Ery/AFP

Walionusurika mashambulizi kama haya yaliyotokea hivi karibuni katika jimbo la Oromia, eneo linalokaliwa na kundi kubwa la kabila la Oromo nchini Ethiopia wamewashutumu wapiganaji wa jeshi la ukombozi la Oromo kwa kuwalenga wanachama wa kabila la Amhara ambalo ni la pili kwa ukubwa nchini humo wakiwataka waondoke.

Wapiganaji wa jeshi la ukombozi la Oromo, ambao sio wengi ni kundi lililojitenga kutoka kwa chama cha ukombozi cha Oromo, Oromo Liberation Front, kundi la upinzani lilichokuwa uhamishoni  kwa miaka mingi  lakini likakubaliwa kurejea nchini Ethiopia baada ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed kuchukua madaraka mwaka 2018.

Hata hivyo hakuna mafungamano ya aina yoyote kati vita vya Oromia na mgogoro unaoendelea katika jimbo la Kaskazini la Tigray. Serikali ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed imeelezea kampeni inayoendelea Tigray kama operesheni ya kuwadhibiti na kuwapokonya bunduki viongozi wa chama tawala katika eneo hilo TPLF.

Lakini maafisa wa serikali wamekishutumu chama cha TPLF kuungana na jeshi la ukombozi la Oromo ili kuchochea vurugu za kikabila na kuidhoofisha serikali ya Abiy Ahmed, madai ambayo serikali ya jimbo la Oromia iliirudia katika taarifa yake ya hapo jana. 

Ethiopia, taifa la pili barani Afrika lililo na idadi kubwa  ya watu inajizatiti kudhibiti malumbano ya kikabila ambako mara kwa mara mivutano inatokea juu ya ardhi, madaraka, na rasilimali. Mivutano hiyo inaendelea kupamba moto wakati serikali ya Abiy ikitarajia kuandaa uchaguzi ulio huru na haki mwezi Juni mwaka huu.

Chanzo: afp/ reuters