1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi wawili wa Nigeria wameuwawa na wengine kujeruhiwa

Mohammed Abdulrahman
15 Oktoba 2018

Wanajeshi wawili wa Nigeria wameuwawa na wengine tisa kujeruhiwa kufuatia shambulizi la bomu la kutegwa ardhini. Hayo yametokea eneo ambalo jeshi linapambana na Boko Haram

https://p.dw.com/p/36YN9
Symbolbild Nigeria Armee
Picha: Getty Images/AFP/S. Heunis

Wanajeshi wawili wa Nigeria wameuwawa na wengine tisa kujeruhiwa katika miripuko miwili tofauti ya mabomu ya kutegwa ardhini katika eneo la kaskazini mashariki, ambako jeshi linapambana na wapiganaji wa kundi la itikadi kali la Kiislamu - Boko Haram. 

Duru za kijeshi na wanamgambo zimesema matukio hayo yalijiri mwishoni mwa juma lililopita.

Katika tukio la kwanza, wanajeshi waliokuwa wakipiga doria kwa miguu walikanyaga bomu lililofukiwa ardhini katika kijiji cha Kumshe karibu na mpaka na Cameroon na wanajeshi wawili wakauwawa. Saa chache baadaye, gari la wanajeshi waliokuwa wakipiga doria kwenye barabara kati ya mji wa Dikwa na Marte, kiasi cha kilomita 140 kutoka eneo la tukio la kwanza, liliripuka na kuwajeruhi wanajeshi 9 na wanamgambo 3.

Mnamo miezi ya karibuni, wapiganaji wa Boko Haram wameimarisha mashambulizi yao dhidi ya maeneo ya kijeshi katika mkoa wa  Borno na mkoa jirani wa Yobe.

Mgogoro huo wa miaka 9 na vita dhidi ya wapiganaji wa jihadi ambao umesambaa hadi n Nigeria, Cameroon na Chad, umeshawauwa watu 27,000 na kuwaacha wengine wapatao milioni 1.8 nchini Nigeria pekee bila ya makaazi.