1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi wa nchi za jumuiya ya SADC kupelekwa Msumbiji

Saleh Mwanamilongo
23 Juni 2021

Marais wa nchi wanachama wa jumuiya ya SADC wamekubaliana Jumatano mjini Maputo kupelekwa wanajeshi kupambana na ugaidi kwenye jimbo la Cabo Delgado. 

https://p.dw.com/p/3vRoN
Demokratischen Republik Kongo Ankunft des kongolesischen Präsidenten Félix Tshisekedi in Maputo
Picha: Giscard Kusema/Präsidentschaft der kongolesischen Republik

Mkutano wa kilele wa marais wa Jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Kusini mwa Afrika, SADC wamekutana leo mjini Maputo,Msumbiji ilikujadili tatizo la ugaidi, maingiliano na manedeleo ya kikanda. Marais hao wamekubaliana kupelekwa wanajeshi wa nchi za SADC kupambana na ugaidi kwenye jimbo la Cabo del Gado. 

Marais na viongozi wa serikali wa nchi 16 wanachama wa jumuiya ya SADC wameadhimisha hii leo miaka 40 toka kuundwa kwa jumuiya hiyo.

Kikosi cha wanajeshi 3000 ?

Mkutano wa marais wa SADC Jijini Maputo

Kwenye mkutano huo wa kilele wa dharura marais hao walijikita hasa kuhusu hali ya kiusalama kwenye jimbo la Cabo Delgado, Kaskazini mwa Msumbiji.  Katibu mtendaji wa jumuiya ya SADC, Stragomena Pax amesema marais hao wamekubalian kupeleka nchini Msumbiji kikosi cha pamoja cha jumuiya hiyo.

 Faustin Luanga, Mshauri wa Maswala ya kimaitafa wa rais wa Congo Felix Tshisekedi,na amabyeni mgombea wa wadhifa wa katibu mtendaji wa jumuiya ya SADC, ameelezea ajenda ya mkutano huo.

''Mkutano ulianza toka Jumatatu ambapo wataalamu walikutana,wakifuatiwa jana na mawaziri na hii leo ni Marais ambao wameadhimisha miaka 40 ya kuundwa kwa Jumuiya ya SADC. Mkutano uliendelea vizuri,walizungumzia masuala ya siasa na hasa usalama huko cabo Delgado Msumbiji.'', alisema Luanga.

Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi ,mwenyekiti wa sasa wa jumuiya ya SADC
Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi, mwenyekiti wa sasa wa jumuiya ya SADCPicha: Reuters/G.L. Neuenburg

Mwenyeji wa mkutano huo, rais Filipe Nyusi wa Msumbiji ambaye pia ni mwenye kiti wa sasa wa Jumuiya ya SADC aliitisha mkutano huo ili kuomba usaidizi wa  marais wenzake kuhusu kitisho cha wanamgambo wanaohusishwa na kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS, ambao wamesababisha hofu na taharuki katika mkoa wa Capo Delgado,kaskazini mwa Msumbiji tangu mwaka 2017 kwa kufanya uvamizi wa vijiji na miji.

''Mbinu za pamoja dhidi ya ugaidi ''

 Kwenye barua ya wazi kwa Marais wa jumuiya ya SADC, mashirika ya kiraia huko mashariki mwa Congo yameomba hatua pia ichukuliwe na jumuiya hiyo kuhusu ongezeko la mashambulizi ya waasi wa ADF huko Beni. Omar Kavota ,Mkuu wa shirika la kiarai la haki za binadamu la CEPADHO,amesema Msumbiji na Congo zote zina changamoto za iana moja.

''Huo mkutano wa SADC ni fursa kwa viongozi wa  jumuiya ya SADC kukubaliana mbinu za pamoja ilikupiganisha ugaidi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Msumbiji'',alisema Kavota.

Mbali na maswala ya usalama marais wa jumuiya ya SADC wamejadili pia hali ya janga la Covid na vilevile juhudi za kupambana na ugonjwa wa ukimwi kwenye eneo hilo.

Kwa mara ya kwanza Rais wa Tanzania,Samia Suluhu ameshiriki mkutano wa kilele wa jumuiya hiyo. Mkutano huo wa maputo ulihuzutiwa pia na marais wa Afrika ya Kusini, Botswana, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Eswatini, Malawi, na Zimbabwe.