Wanajeshi wa MONUSCO huenda wakapunguzwa 2015 | Matukio ya Afrika | DW | 05.12.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

Wanajeshi wa MONUSCO huenda wakapunguzwa 2015

Kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, kinaweza kuwapunguza wanajeshi wake nchini humo kuanzia mwaka 2015, licha ya kuendelea kuwepo kwa umwagikaji damu mashariki mwa Kongo.

Kikosi cha MONUSCO kikiwa DRC

Kikosi cha MONUSCO kikiwa DRC

Mkuu wa kikosi hicho cha MONUSCO, Martin Kobler, amesema wanaweza kuwapunguza wanajeshi hao mwakani, ikiwa mamlaka ya serikali yatarudishwa mashariki mwa Kongo.

Kobler amesema kuwa tayari ujumbe kutoka New York, makao makuu ya Umoja wa Mataifa umeshafanya ziara katika eneo hilo kuangalia jinsi kikosi cha MONUSCO kinavyoweza kuwapunguza wanajeshi wake kutokana na kuimarika hali ya usalama kwenye maeneo mengi.

Hata hivyo, katika wiki za hivi karibuni, Umoja wa Mataifa umeelezea wasiwasi wake kuhusu kuzorota kwa hali ya usalama kwenye jimbo la Kivu Kaskazini, ambako makundi kadhaa ya waasi wa Kikongo na yale ya kigeni yanaendelea kufanya uasi.

Mauwaji yashuhudiwa Beni

Mauwaji kadhaa yameshuhudiwa katika eneo la Beni, kaskazini mwa Kivu na watu 200 waliuawa kati ya mwezi Oktoba na Novemba. Wahanga wa mauaji hayo ni pamoja na wanawake na watoto.

Martin Kobler (Kulia) akiwa kwenye mkutano na waandishi habari DRC

Martin Kobler (Kulia) akiwa kwenye mkutano na waandishi habari DRC

Waasi wa Kiislamu wa Allied Democratic Forces na waasi wa Uganda wa ADF-NALU, wanashutumiwa kuhusika na mauaji hayo.

Ghasia za hivi karibuni zilitokea siku ya Alhamisi, wakati wa mapambano ya makundi ya kijeshi, ambapo wapiganaji wanne wa ADF-NALU na mwanajeshi mmoja wa Kongo, waliuawa. Taarifa hizo ni kwa mujibu wa jeshi la Kongo.

Msemaji wa kikosi cha jeshi la Kongo kinachoendesha operesheni dhidi ya waasi wa Uganda, Kanali Celestin Geleka anasema kuwa mapambano yataendelea hadi watakapofanikiwa kuwafurumusha kabisa waasi wa ADF-NALU.

Kikosi cha MONUSCO, ambacho ni moja ya kikosi kikubwa zaidi cha Umoja wa Mataifa duniani, kimekuwepo katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo kwa miaka 15 na kwa sasa kina wanajeshi 20,000, wengi wao wakiwa wanaendesha operesheni kwenye eneo la Mashariki mwa Kongo.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE
Mhariri:Yusuf Saumu

DW inapendekeza

Matangazo

IJUE DW

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com