1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi wa Marekani kuondoka Afghanistan

30 Juni 2011

Mpango wa rais Obama wa kuondoa majeshi Afghanistan utaanza na wanajeshi 10,000

https://p.dw.com/p/11mKz
Gen. David Petraeus, Kamanda wa kikosi cha Marekani na wanajeshi wa NATO nchini Afghanistan.Picha: dapd

Wanajeshi wa Marekani wanaoongoza kikosi cha jumuiya ya NATO nchini Afghanistan wanaanza rasmi mpango wa kuondoka nchini humo na kukabidhi jukumu la usalama kwa kikosi cha Afghanistan.Hivi karibuni rais Barack Obama alilifafanulia taifa lake juu ya mpango huo wa kuondoa wanajeshi wa Marekani Afghanistan akisema wanajeshi 10,000 kati ya 100,000 watakuwa wameondoka nchini humo kufikia mwishoni mwa mwaka huu.

Kwa mujibu wa mpango huo wa rais Barack Obama wanajeshi wengine 23,000 wakimarekani watakuwa wameshaondoka nchini Afghanistan kufikia mwezi Septemba mwaka 2012,na kufikia mwaka 2014 jukumu la kusimamia usalama linatakiwa kukabidhiwa wanajeshi wa Afghanistan kama ilivyoamuliwa na washirika wote wa jumuiya ya NATO. Mkuu wa kikosi cha Marekani nchini Afghanistan Generali David Patraeus amesema mpango huo wa rais Obama ni kinyume na alivyopendekeza yeye na kwamba ni hatua nzito zaidi. Akifafanua zaidi kuhusu mpango huo  mbele ya baraza la seneti hivi karibuni amesema

Portugal NATO NATO-Gipfel Ankunft Hamid Kharsai Afghanistan
Rais Hamid Kharzai wa AfghanistanPicha: AP

''Kuna baadhi ya wanajeshi ambao tayari wameanza kurudi nyumbani na bila ya nafasi zao kujazwa kama ilivyoamuliwa. Na wengine wataorodheshwa katika ratiba ya kuanza kuondoka halafu na watafuata utaratibu uliowekwa wa kukamilisha operesheni ya kikosi hicho. Na mpango huo utaendelea kama inavyotakiwa na kama maamuzi yalivyopitishwa.''

Katika kipindi cha miezi 15 ijayo wanajeshi wa Marekani watahitajika kuwapa mafunzo wanajeshi kiasi cha 70,000 katika hatua ambayo itaweza kuwapa nafasi wanajeshi hao kuchukua nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na kikosi cha Marekani.

Generali Patreus mwenyewe halazimiki  kuleta kasheshe juu ya mpango huo wa rais Obama hasa ikizingatiwa kwamba anaachia ngazi na kwenda kuwa mkuu wa shirika la kijasusi la Marekani CIA. Kwa hivyo kuondoka kwake kuna maana ya kutoweka kwa ule mkakati wa vita katika medali ya mapambano ambao ulionekana kufanikiwa nchini Iraq,mkakati uliokuwa ukijikita katika kuwalinda raia na wakati huohuo kupambana dhidi ya waasi.

Afghanistan Anschlag auf Hotel Intercontinental in Kabul
Picha: dapd

Nafasi ya Generali David Patreaus itachukuliwa na  Generali John Allen ambaye atahitaji kutumia ujuzi wake kama Kamando alipokuwa magharibi mwa Iraq. Generali Allen anasema kupunguzwa kwa wanajeshi wa Marekani nchini Afghanistan ni hatua itakayopewa nguvu zaidi na kuongezwa kwa kikosi cha Afghanistan ambacho kinatazamiwa kufikia  hadi wanajeshi  70,000 ifikapo mwaka 2012 wakati kikosi cha kwanza cha Marekani kinahitajika kukamilisha zoezi la kuondoka Aghanistan. Ingawa baadhi ya wabunge nchini Marekani wanaoona uamuzi wa rais Obama umejikita zaidi kisiasa kuliko kuangalia hali halisi ya vita nchini Afghanistan.    

Mwandishi: Christian Bergmann ZPR/Saumu Mwasimba

Mhariri: AbdulRahman