1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi wa Israel wajeruhiwa kufuatia shambulizi la roketi

Jane Nyingi11 Septemba 2007

Karibu wanajeshi 69 wa Israel wamejeruhiwa baada ya roketi iliyorushwa kutoka ukanda wa gaza na wanamgambo wa kipalestina kulipuka katika kambi ya vikosi vya Israel. Shambulizi hilo huenda likaongeza shinikizo kwa viongozi wa Israel kuchua hatua katika eneo hilo linalosimamiwa na kundi la Hamas.

https://p.dw.com/p/CB1M
Roketi iliyorushwa na wanamgambo wa kipalestina na kulipuka kambi ya kijeshi ya Israel
Roketi iliyorushwa na wanamgambo wa kipalestina na kulipuka kambi ya kijeshi ya IsraelPicha: AP

Hii ni idadi kubwa ya wanajeshi wa Israel kujeruhiwa kwa wakati mmoja na shambulizi moja la roketi kutoka ukanda wa gaza tangu kundi la hamas kuchukua usimamizi wa eneo hilo kufuatia makabiliano ya miezi mitatu na chama cha fatah kinachoogozwa na rais wa Palestina Mahmoud abbas. Majeruhi wengi wao kutokana na marisau ya roketi walikimbizwa katika hospitali zilizokaribu.Makundi mawili ya wanamgambo tayari yamekiri kutekeleza shambulizi hilo.

Msemaji wa vikosi vya Israel amesema roketi hiyo ilirushwa kutoka Beit Hanoun kaskazini mwa ukanda wa gaza na kulipuka katika kambi ya mazoezi ya kijeshi ya Zikkim wakati baadhi ya wanajeshi walipokuwa wamelala kwenye mahema. Jamaa na marafiki walifurika katika kambi hiyo kujua hatma ya wapendwa wao.

Saa chache baada ya shambulizi hilo, majeshi ya Israel pia yalirusha kombora lake na kuharibu kabisa nyumba zilizo katika eneo la beit Lahiya,mji wa kipalestina ulioko kaskazini mwa ukanda wa gaza.Wakati wa shambulizi hilo mama na mwanawe wa kike walijeruhiwa vibaya.

Wanamgambo walioko katika ukanda wa gaza mara kwa mara hurusha makombora kaskazini mwa Israel na kulipuka katika mji wa Sderot. Ni wiki jana tu ambapo wanagambo hao wa kipalestina walirusha kombora na kulipuka katika shule ya watoto chekechea,hatua iliyowafanya wazazi wengi kuwaondoa watoto wao shuleni humo na kuyataka majeshi ya Israel kulipiza kisasi.

Waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert tayari ameviagiaza vikosi vya Israel kuandaa mipango njisi ya kukabiliana na mashambulizi hayo ya mara kwa mara kutoka ukanda wa gaza.

Serikali ya Israel imelaumu kundi la Hamas ambalo lilichukua usimamizi wa ukanda wa gaza kwa kushindwa kudhibiti mashambulizi hayo.

Maafisa wa Israel wamesema kutuma vikosi vyake ili kukabiliana na wapiganaji hao wa kipalestina huenda kukasababisha idadi kubwa ya majeruhi kutoka pande zote mbili. Olmert na rais wa palestina Mahmoud Abbas wamekuwa wakifanya mashauri ya mara kwa mara kutafuta mbinu za kukabiliana na hali hiyo.

Serikali ya Israel iliyaondoa majeshi yake pamoja na walowezi wa Israel katika ukanda wa gaza mwaka 2005.Hata hivyo wanamgambo wa kipalestina wanaamini kuwa vikosi vya Israel bado havijaondoka kabisa kutokana na kusimamia maeneo ya mpakani, anga na mwambao wa bahari.