1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi wa Ethiopia waondoka Somalia

Charo Josephat13 Januari 2009

Wakaazi wa Mogadishu washangilia

https://p.dw.com/p/GXhQ

Wanajeshi wa Ethiopia ambao wamekuwa wakiisadia serikali ya Somalia wameanza kuondoka kambi zao mjini Mogadishu hii leo. Kuondoka kwao kunafungua ukurasa mpya katika eneo la Pembe ya Afrika linalokabiliwa na migogoro ya kivita.

Wakaazi wengi wa mji wa Mogadishu wameshangilia kuondoka kwa wanajeshi hao wa Ethiopia. Lakini swali linalojitokeza ni ikiwa furaha hiyo itadumu kwa muda mrefu.

Ethiopia imewaondoa wanajeshi wake kutoka kwenye kambi mbili kaskazini mwa Mogadishu katika awamu ya kwanza ya kuondoka kutoka mji huo mkuu wa Somalia tangu ilipoingia miaka miwili iliyopita.

Sheikh Hasan Osman, afisa wa kundi la wapiganaji wa kiislamu nchini Somalia, amethibitisha kuondoka kwa wanajeshi wa Ethiopia kutoka maeneo muhimu kaskazini mwa Mogadishu na kuongeza kwamba wapiganaji wa kundi lake wameyachukua maeneo hayo ili kuzuia kutokea pengo la mamlaka.

Wakaazi wengi wa mji wa Mogadishu waliwatazama wanajeshi wa Ethiopia kama wavamizi waliokuja kuikalia nchi yao. Na ndio maana kuondoka kwao kumezusha furaha mjini humo.

''Tunasema sifa zimrudie mwenyezi Mungu aliyewafanya wanajeshi wa Ethiopia kuondoka nchini mwetu,'' amesema Hussein Awale mkaazi wa eneo la kaskazini la mji wa Mogadishu, aliyekuwa miongoni mwa mamia ya watu waliokusanyika kwenye mojawapo ya kambi nne zilizoachwa na wanajeshi wa Ethiopia katika eneo hilo.

Naye Farah Abdi Warsame, mkaazi wa Mogadishu, amesema na hapa namnukulu, ''Ni siku ya furaha kuona eneo hili kwa mara kwanza likiwa bila wanajeshi wa Ethiopia katika kipindi cha miaka miwili. Tuna matumaini wale wengine wataondoka nchini mwetu.'' mwisho wa kumnukulu mkazi huyo.

Hata hivyo, wachambuzi wanahofu kuondoka kwa wanajeshi wa Ethiopia kutaacha pengo la mamlaka na hivyo kuzusha machafuko zaidi kutoka kwa wanamgambo wa kundi la al Shabaab ambao wamekuwa wakipambana na serikali na hata kupigana wenyewe kwa wenyewe.

Wakati wanajeshi wa Ethiopia watakapomalizika kuondoka Mogadishu, watakaobakia kushika doria ni wanajeshi wa jeshi la serikali ya Somalia linalokaribia kuvunjika, wakisaidiwa na wanajeshi takriban 3,000 wa Umoja wa Afrika kutoka nchini Uganda na Burundi.

Umoja wa Afrika unajaribu kuongeza idadi ya wanajeshi wa kulinda amani nchini Somalia lakini Umoja wa Mataifa umefutilia mbali kupelekwa kikosi cha kulinda amani nchini humo. Kundi la wanamgambo wa al Shabab, ambalo Marekani inadai lina mafungamano ya karibu na kundi la al Qaeda, litaonekana kuwa na nguvu zaidi ikizingatiwa udhaifu wa jeshi la serikali.

Roger Midleton, mchambuzi wa siasa za pembe ya Afrika, ameliambia shirika la habari la kijerumani DPA kuna uwezekano mkubwa kundi la al Shabaab likapingwa na makundi mengine ya wanamgambo, na hivyo kuzusha vita vingine vikali nchini Somalia.

Mwishoni mwa juma lililopita wapiganaji wa al Shabaab walikabiliana na waasi wa kundi la Guriel, yapata kilomita 500 kaskazini mwa Mogadishu ambapo watu 30 waliuwawa na zaidi ya 30 kujeruhiwa.

Kundi jipya la wapiganaji la Ahlu Sunna Wal Jamaa, limewahi kupigana na kundi la al-Shabaab katika majuma machache yaliyopita na kusababisha vifo vya madazeni ya watu.

Mjumbe mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, Ahmedou Ould-Abdallah, amewatolea mwito wapiganaji wa kiislamu wenye msimamo mkali, ambao waliweka sharti la kuondoka kwa majeshi wa Ethiopia kutoka Somalia kabla kushiriki kwenye mazungumzo ya kusaka amani, wakomeshe mapigano.

Kiongozi huyo aidha amesema Waethiopia wameheshimu ahadi yao na kutimiza jukumu lao. Kazi sasa iko upande wa Wasomali kuweka silaha chini, hususan wale waliosema wanapigana dhidi ya wanajeshi wa Ethiopia.