1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi, polisi wauawa Misri

Admin.WagnerD7 Oktoba 2013

Vikosi vya usalama vya Misri vilishambuliwa katika maeneo mbalimbali nchini humo siku ya Jumatatu, ambapo maafisa tisa wa jeshi na polisi waliripotiwa kuuawa.

https://p.dw.com/p/19vnA
Bildnummer: 60566706 Datum: 06.10.2013 Copyright: imago/Xinhua Waandamanaji wakimbeba mwenzao aliejeruhiwa katika maandamano.
Waandamanaji wakimbeba mwenzao aliejeruhiwa katika maandamano.Picha: imago/Xinhua

Vikosi vya usalama vya Misri vilishambuliwa katika maeneo mbalimbali nchini humo siku ya Jumatatu, ambapo maafisa tisa wa jeshi na polisi waliripotiwa kuuawa.

Watu wanaoshukiwa kuwa wapiganaji waliwauwa wanajeshi tisa katika mashambulizi, siku moja baada ya kutokea makabiliano kati ya wafuasi wa rais alieondolewa Mohammad Mursi na jeshi la polisi, ambayo yalisababisha vifo vya watu wasiopungua 50, na kuondoa matumaini ya utulivu uliokuwa umerejea baada ya maoinduzi ya Julai 3.

Taarifa za jeshi la polisi zilisema kuwa mripuko wa bomu la kutegwa kwenye gari nje ya makao makuu ya polisi ya mkoa wa Sinai uliwauwa maafisa watatu wa jeshi hilo, wakati watu wenye silaha waliwapiga risasi na kuwaua wanajeshi sita karibu na mji wa Ismailiya uliyoko kwenye mfereji wa Suez.

Vurugu zikiendelea mjini Cairo.
Vurugu zikiendelea mjini Cairo.Picha: Reuters

Mashambulizi hayo yalikuja baada ya wafuasi wa vyama vya Kiislamu, wakiwa na matumaini ya kuimarisha vuguvugu lao la maandamano, kukabiliana na polisi wakati walipojaribu kuandamana kuelekea uwanja wa Tahrir mjini Cairo. Washambuliaji wanaofyatua maroketi ya gruneti waliharibu pia kituo cha mawasiliano ya setilaiti mjini Cairo, kinachounganisha simu za kimataifa.

Maandamano zaidi yatarajiwa
Wafuasi kadhaa wa rais Mohammad Mursi wa Udugu wa Kiislamu waliuawa siku ya Jumapili, ambapo vyombo vya habari vya serikali viliripoti kuwa idadi ya waliokufa ni watu 53 na 271 walijeruhiwa katika moja ya siku za mauaji makubwa zaidi tangu jeshi lilipompindua rais Mursi Julai 3.

Makabiliano zaidi yalikuwa yanatarajiwa kuitikisa tena Misri wiki hii, wakati ambapo wafuasi wa Mursi wameitisha maandamano mengine siku za Jumanne na Ijumaa. Wafuasi hao wanatarajiwa kughadhabishwa na kuchapishwa kwa mahojiano ya mkuu wa majeshi ya Misri siku ya Jumatatu, ambamo alisema kuwa alimuambia Mursi tangu mwezi Februari kuwa ni rais alieshindwa.

Maelfu ya wafuasi wa Mursi walipambana na vikosi vya usalama na wafuasi wa jeshi siku ya Jumapili, siku ambayo Misri ilikuwa inakumbuka vita vya mwaka 1973 kati yake na Israel, ambayo ilipaswa kuwa siku ya sherehe. Serikali ilikuwa imetahadharisha mapema kuwa yeyote ambaye angeandamana siku hiyo angechukuliwa kuwa ni wakala wa mataifa ya kigeni, na wala si mwanaharakati - lugha kali ambayo iliashiria kuwa waandamanaji hao wangeshughulikiwa kwa mkono wa chuma.

Machafuko Cairo.
Machafuko Cairo.Picha: AFP/Getty Images

Sekta ya utalii yaumia zaidi
Mashambulizi hayo yamezidi kuitia doa sekta ya utalii ya Misri, huku kukiwa hakuna dalili za mapatano kati ya Udugu wa Kiislamu na serikali inayoungwa mkono na jeshi. Jenerali Abdul-Fatah Al-Sisi alisema katika mahojiano yaliyochapishwa na gazeti binafsi la al-Masry al-Yaum, kuwa alimuambia Mursi mwezi Februari kwamba ameshindwa na mradi wake umekwisha.

Wachambuzi wanasema huenda miripuko inaonekana kutumiwa zaidi mjini Cairo, na matukio ya hivi sasa yanaashiria kuwa makundi ya wapiganaji yaliyoko katika rasi ya Sinai yamejipenyeza kaskazini mwa Misri kwa idadi kubwa, au uwezo wake unatumiwa na makundi mengine, ambayo yanaweza kuwa au kutokuwa na uhusiano na Udugu wa Kiislamu.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/rtre, afpe
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman