1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanaharakati watoa wito wa maandamano zaidi Myanmar

Saleh Mwanamilongo
27 Machi 2021

Wanaharakati nchini Myanmar wametoa wito kufanyike maandamano makubwa zaidi wikendi hii wakati jeshi litakapokuwa linaadhimisha siku ya Wanajeshi nchini humo.

https://p.dw.com/p/3rGyz
Myanmar | nach Militärputsch | Tag der Streitkräfte
Picha: AP Photo/picture alliance

Kabla ya alfajiri, ofisi za chama cha Aung San Suu Kyi cha National League for Democracy (NLD) zilishambuliwa japo kulikuwa na uharibifu mdogo.

Shambulio hilo limetokea siku moja tu kabla ya maadhimisho ya siku ya vikosi vya jeshi, wakati wanajeshi watakapopiga gwaride na kuonyesha uwezo wao wa kijeshi.

''Hatufahamu nani alifanya shambulio hilo, lakini sio jambo zuri hata kidogo,'' alisema Soe Win, mbunge wa chama cha NLD.

Toka mapinduzi ya kijeshi ya Februari Mosi, takriban watu 3,000 wamekamatwa, wengi wao kufuatia maandamano ya mitaani.

Wakati huo huo, afisa mwandamizi wa magereza ameliambia shirika la habari la AFP kuwa zaidi ya watu 300 waliokuwa wamewekwa kizuizini kufuatia maandamano wameachiliwa huru.

Hofu ya kutokea na machafuko zaidi 

Kuachiliwa kwa watu hao kunatokea siku chache tu baada ya jeshi kuwaachilia huru watu wengine zaidi ya 600 waliokuwa wamekamatwa wakati wa oparasheni ya kijeshi dhidi ya waandamanaji.

Waandamanaji wakabiliana na maafisa wa usalama mjini Yangon
Waandamanaji wakabiliana na maafisa wa usalama mjini YangonPicha: AP Photo/picture alliance

Inahofiwa kuwa huenda kukawa na machafuko zaidi kufuatia wito huo wa maandamano ya hapo kesho.

Wahanarakati walitoa mwito wa maandamano makubwa ya kupinga mapinduzi ya kijeshi hapo kesho.

''Ni wakati tena wa kupambana na ugandamizaji wa kijeshi,'' aliandika kwenye ukarasa wake wa Facebook, Ei Thinzar Maung mwanaharakati mkuu wa demokrasia nchini Myanmar.

Nchi hiyo imetumbukia kwenye machafuko baada ya mapinduzi ya kijeshi mnamo Februari mosi, yaliyomng'oa madarakani Aung San Suu Kyi, hatua iliyochochea maandamano ya kutaka kurejeshwa kwa utawala wa kiraia.