Wanaharakati waitaka Afrika iiunge mkono ICC | Matukio ya Kisiasa | DW | 06.07.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Wanaharakati waitaka Afrika iiunge mkono ICC

Mashirika ya kutetea haki za binadamu ya barani Afrika kote yanapinga shutuma za Umoja wa Afrika juu ya Mahakama ya Kimataifa ICC. Yanazitaka serikali za nchi za Afrika ziunge mkono kazi ya mahakama hiyo

Aliekuwa Rais wa Ivory Coast Laurent Gbagbo mbele ya Mahakama ya ICC

Aliekuwa Rais wa Ivory Coast Laurent Gbagbo mbele ya Mahakama ya ICC

Mapema mwaka huu Umoja wa Afrika uliipa kamati ya mawaziri wa taasisi hiyo, jukumu la kuweka mkakati kamambe juu ya Mahakama ya Kimataifa ya mjini The Hague ,ICC ikiwa pamoja na kujumuisha kipengele juu ya kutafakari kujiondoa kwa nchi za Afrika kwenye mahakama hiyo.

Kamati hiyo ilikutana mnamo mwezi wa Aprili na kupitisha masharti inayotaka yatimizwe na Mahakama ya mjini The Hague .

Miongoni mwa masharti hayo ni kuwahakikishia viongozi wa Afrika waliomo madarakani kinga dhidi ya kushtakiwa, jambo linalozingatiwa kuwa linaenda kinyume na kanuni ya msingi ya mahakama hiyo.

Wanaharakati 12 kutoka barani Afrika kote wamepaaza sauti kuonyesha wasi wasi kuhusu sera ya Umoja wa Afrika juu ya Mahakama ya ICC.

Mwanaharakati Ibrahim Tommy kutoka kituo cha uwajibikaji na utawala wa kisheria nchini Sierra Leone amesisitiza ulazima wa kuwafikisha viongozi mahakamani pale wanapotenda uhalifu.

Mgongano washtadi:

Amesema mgongano mkubwa sasa ni juu ya viongozi wa Afrika yaani watu wachache wenye mamlaka makubwa wanaotaka kutenda makosa bila ya kuwajibishwa na hivyo kuwadhulumu wengi- wahanga wote wa barani Afrika wanaodai haki kila siku.

Mwanaharakati wa Nigeria Chino Obiagwu kutoka kitengo cha kutoa msaada wa kisheria anaunga mkono haja ya kuwapa haki watu wanaotendewa uhalifu.

Mikasa sita kati ya tisa iliyochunguzwa na Mahakama ya mjini The Hague kuhusu nchi za Afrika imetokana na maombi ya serikali za Afrika. Mikasa iliyochunguzwa na taasisi hiyo ilihusu yaliyojiri katika Cote d'Ivoire, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mali, Uganda, na Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Wakimbizi wa ndani katika jimbo la Darfur

Wakimbizi wa ndani katika jimbo la Darfur

Uchunguzi juu ya Jimbo la Darfur la Sudan na Libya ulirelejewa kwa mahakama iliyodhaminiwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Mapendekezo yaliyotolewa na Kamati maalumu ya Umoja wa Afrika ni miongoni mwa hatua za hivi karibuni za viongozi wa Afrika dhidi ya Mahakama ya mjini The Hague za kuelekeza lawama ,kwamba Mahakama hiyo inafanya maonevu kwa kuliandama bara la Afrika.

Mgongano baina ya mahakama hiyo na nchi za Afrika ulishtadi baada ya taasisi hiyo kutoa hati ya kisheria, mnamo mwaka wa 2009 ya kuwezesha kukamatwa kwa Rais Omar al -Bashir wa Sudan kutokana na tuhuma za kutenda uhalifu mkubwa katika jimbo la Darfur.

Mwaka uliopita Umoja wa Afrika ulipitisha rasimu ya kuipa mamlaka mahakama ya Afrika ya kuhukumu uhalifu, lakini pia katika mazingira ya kutatanisha inawapa viongozi waliomo madarakani kinga dhidi ya kushtakiwa.

Mwandishi:Mtullya Abdu/Amnesty International

Mhariri: Sssessanga Iddi

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com