1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiNigeria

Watu wenye silaha wawateka wanafunzi wengine 15, Nigeria

Lilian Mtono
10 Machi 2024

Kundi la watu wenye silaha nchini Nigeria limeishambulia shule nyingine na kuwateka nyara watoto 15 katika tukio la tatu la utekaji nyara wa watu wengi katika muda wa wiki mbili.

https://p.dw.com/p/4dMTH
Nigeria | Wanafunzi watekwa na watu wenye silaha
Magari ya jeshi la Nigeria yakiwa katika eneo ambalo watu wenye silaha waliteka wanafunzi huko Chikun, Nigeria, Alhamisi, Machi 7, 2024. Karibu wanafunzi 287 walitekwaPicha: AP/dpa/picture alliance

Msemaji wa polisi Ahmad Rufai amesema wavamizi waliokuwa na silaha nyingi walivamia bweni la shule moja katika jimbo la Sokoto jana asubuhi. Pamoja na watoto, mwanamke mmoja kutoka kijiji cha Gidan Bakuso pia alichukuliwa mateka.

Polisi ilifahamishwa kuhusu tukio hilo saa kadhaa baadae kwa sababu kijiji hicho kipo katika eneo la mbali bila huduma ya simu za mkononi au barabara za lami. Msemaji wa polisi amesema iliwezekana tu kufika katika eneo la tukio kwa kutumia pikipiki.

Hakufichua ni kina nani waliofanya utekaji huo. Alhamisi iliyopita, wanafunzi 287 walitekwa kutoka shule moja ya kijiji cha Kuriga cha jimbo la kaskazini magharibi la Kaduna.