1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Sayansi

Wanaanga warejea duniani baada ya miezi anga katika za mbali

Daniel Gakuba
17 Aprili 2020

Wanaanga wa Urusi na Marekani wamerejea duniani baada ya kuhudumu kwenye kituo cha kimataifa cha anga za mbali, ISS kwa muda wa zaidi ya siku 200. Tahadhari imechukuliwa kuwalinda maambukizi ya virusi vya corona.

https://p.dw.com/p/3b4Pa
Kasachstan Baikonur ISS-Raumfahrer vor Start am Kosmodrom
Picha: Reuters/Roscosmos

Wanaanga hao, Jessica Meir na Andrew Morgan wa Shirika la Marekani la Anga za Juu, NASA pamoja na Oleg Skripochka wa Urusi wamewasili kwenye ardhi ya dunia nchini Khazakhstan majira ya saa tano na dakika kumi na sita (11:16 a.m), wakapokelewa kwa tahadhari kubwa kuwaepusha hatari ya kuambukizwa virusi vya corona.

Chombo chao chapa Soyuz kimetua kwa msaada wa parachuti yenye rangi ya chungwa na nyeupe, eneo ambalo ni umbali wa km 150 kutoka mji wa Dzheskazgan katikati mwa Kazakhstan.

Maafisa wa Urusi wamesema wafanyakazi waliokwenda kuzipima afya za wanaanga hao mara tu baada ya kuwasili duniani, walichunguzwa kwa muda wa takriban mwezi mzima kuhakikisha kuwa hawana virusi vya corona.

Baada ya siku zaidi ya 200 anga za mbali

Sojus MS-11-Kapsel bei Landung
Chombo maalum kilichotumiwa na wanaanga kutua tena dunianiPicha: Getty Images/AFP/A. Nemenov

Andrew Morgan alikuwa ameishi kwenye kituo cha kimataifa cha anga za juu kwa siku 272, na katika muda huo alitembea mara saba kwenye anga hilo, katika juhudi za kuboresha kifaa cha kituo hicho (Alpha Magnetic Spectrometer) kinachochunguza uwepo wa ''mada za giza'' katika anga hilo la mbali ya sayari ya dunia.

Jessica Meir na Oleg Skripochka wamekuwa kwenye kituo cha ISS kwa siku 205, ambapo Meir alishirika katika matembezi kwenye anga za mbali ya kuwashirikisha wanawake peke yao, akiwa pamoja na Christina Koch aliyerejea duniani Februari mwaka huu.

Walipokuwa wakichukuliwa vipimo na wataalamu waliovaa barakoa, waanaanga hao walionekana wachangamfu na wenye tabasamu. Baada ya vipimo hivyo ilitarajiwa kuwa Oleg Skripochka atasafirishwa kwa helikopta hadi mjini Moscow, wakati wenzake kutoka Marekani, Meir na Morgan watasafiri kwa ndege maalum ya NASA hadi mjini Houston.

Walifuatilia kwa mbali janga la COVID-19

Astronauten Hazza al Mansoori, Oleg Skripochka und Jessica Meir
Katika kituo cha kimataifa cha anga za mbali wanaaanga hufanya tafiti mbali mbali za kisayansiPicha: picture-alliance/dpa/S. Krasilnikov

Wanaanga hao watatu wamerejea duniani miaka 50 kamili tangu wanaanga waliokuwa katika chombo cha Apollo 13 walipoanguka katika bahari ya Pasifiki, baada ya tanki lao la Oksijeni kuripuka na kuivunja safari yao ya kwenda mwezini.

Kabla ya kuanza safari yao kurudi duniani, wanaanga hao walisema walihofia kile watakachokikuta katika sayari inayozongwa na janga la COVID-19, wakisema ilikuwa vigumu kwao kufikiria kinachoendelea huko (duniani).

Wamesema ukiitazama dunia kutoka anga za mbali unaiona ya kuvutia kama kawaida, bila ishara zozote za mtafaruku unaosababishwa na maambukizi ya virusi vya corona.

Wanaanga wengine watatu waliochukua nafasi zao kwenye kituo cha ISS, Chris Cassidy wa Marekani na Warusi Anatoly Ivanishin na Ivan Vagner, waliwasili kwenye kituo hicho Aprili 9.

 

ape, dpae