1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wamisri wameathirika pia na mashambulio ya Israel

Miraji Othman26 Mei 2009

Wamisri wanadai fidia kwa mashambulio ya Israel

https://p.dw.com/p/Hxln
Kivuko cha mpakani cha Rafah , baina ya Misri na Ukanda wa GazaPicha: AP

Wakaazi wanaoishi katika mpaka wa Misri na Ukanda wa Gaza bado wanangojea kulipwa fidia kutokana na mali zao kuharibiwa kutokana na mashambulio ya angani ya Israel walioyafanya kattika ukanda huo unaodhibitiwa na Chama cha Wapalastina cha Hamas. Wakuu wa Misri wanasema serekali yao haina dhamana kwa uharibifu huo ambao ulitokana moja kwa moja na mashambulio ya Israel. Hata hivyo, hali hiyo ina ugumu wake.

Wakati wa mashambulio ya wiki tatu yaliofanywa na Israel baina ya Disemba 27 na Januari 17 mwaka huu, maelfu ya majumba katika Ukanda wa Gaza yaliharibiwa kutokana na hujuma za angani na ya mizinga ya Israel, na zaidi ya watu 1,500 waliuliwa. Ardhi ya Misri pia haijaepukana na mashambulio hayo pamoja na uharibifu uliotokea. Wakati wa operesheni hiyo ya kijeshi ya Israel, mpaka wa urefu wa kilomita 14 baina ya Gaza na Misri pia ulishuhudia mashambulio mengi kutoka ndege za Israel. Kwa mujibu wa maafisa wa Israel ni kwamba mashambulio hayo yalilenga mahandaki yanayotumiwa kusafirishia kwa magendo silaha kuendea Gaza kutokea Misri.


Wakati wa mashambulio hayo, nyumba 86 katika maeneo ya mpaka ziliharibiwa vibaya kutokana na mabomu yaliotupwa na Israel; pia maeneo makubwa ya ardhi ya kilimo yaliharibiwa.


Hapo Januari 11, watu kadhaa katika mji wa Rafah unaosambaa mpakani baina ya eneo la Sinai la Misri na Ukanda wa Gaza walijeruhiwa kutokana na mabomu yaliolengewa upande wa Wapalastina wa mji huo. Wakati huo taarifa rasmi zilisema wakaazi walioharibiwa watalipwa fidia na serekali ya Misri kwa uharibifu wa mali zao. Lakini hamna malipo yaliotolewa kwa familia hizo. Imetajwa kwamba gavana wa jimbo la Sinai ya kaskazini alipendekeza kutolewe fidia, lakini fikra hiyo haijawahi kukubaliwa na wakuu wa mjini Kairo. Hivyo, suala hilo linabaki kuwa hewani. Kulifanywa tu uchunguzi wa majumba yalioharibiwa katika mji wa Rafah, lakini zaidi ya hapo hakuna hatua yeyote iliochukuliwa ya kuwaklipa wale wanaohusika.


Kuna tamaa kwamba fidia huweza ikatolewa na duru isiokuwa ile ya Misri, kwani hata ikiwa serekali ya Misri italazimika kutoa fidia, basi itakuwa ndogo mno.


Mwaka 2007, kuna baadhi ya maafisa huko Misri waliodokeza juu ya mipango ya kuwahamisha wakaazi wa Rafah hadi umbali wa angalau kilomita tatu kutoka mpaka na Ukanda wa Gaza. Lakini baada ya wakaazi wa eneo hilo kufanya maandamano yaliojaa hasira na kupambana na polisi, wakuu walirejea nyuma katika fikra yao na wakasema hawana nia hiyo.


Lakini kuna watu walioharibikiwa na nyumba zao kutokana na mashambulio ya Israel wanaohisi kwamba yafaa sasa kuondoka kutoka eneo hilo na kuhamia mahala kwengine. Kwa mujibu wa ripoti, ni kwamba eneo hilo la mpakani linaendelea kushambuliwa na ndege za Israel. Kwa hakika, wakaazi wa Rafah wanaishi katika hali ya hofu isiokwisha, wakifikiri huenda wakauliwa wakati wowote. Wengi wa wakaazi wa mji huo wanaondoka au wanajitayarisha kuuhama mji huo.



Pia wakaazi wanalalamika juu ya vikwazo vinavowekwa na polisi wa Misri kwa sababu za usalama. Mnamo miezi minne iliopita, mji wa Rafah umebadilika kuwa eneo la kijeshi, raia wakikatazwa kutembea katika mabarabara ya mji huo, isipokuwa katika barabara kuu, baada ya saa nne za usiku. Kuna hofu kwamba mji huo unaelekea kuwa kama mji wa mashetani, ukimya ukitanda.