Wamethubutu, wameweza | IDHAA YA KISWAHILI | DW | 14.07.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

IDHAA YA KISWAHILI

Wamethubutu, wameweza

Baada ya kujaribu bila mafanikio kulitwaa Kombe la Dunia tangu walipofanya hivyo mara ya mwisho mwaka 1990, hatimaye ndoto ya vijana wa Jogi (timu ya taifa ya Ujerumani) ilitimia usiku wa Jumapili.

Mchezaji kiungo Mario Goetze - Super Mario - alijiandika kwenye vitabu vya historia pale alipopachika goli la ushindi katika fainali za kombe la dunia, lililoipatia Ujerumani ubingwa wa dunia. Nyota huyo wa klabu ya Bayern Munich alitegua kitendawili cha ubingwa katika dakika ya 113 na kuinyamanzisha Argentina, huku ndoto ya Lionel Messi ya kufuata nyayo za nguli Diego Maradona ikiishia kwa kushindwa.

Bastian Schweinsteiger akipongezwa na Kansela Angela Merkel huku mchezaji mwenzake Andre Schuerrle akipongezwa na rais Joachim Gauck.

Bastian Schweinsteiger akipongezwa na Kansela Angela Merkel huku mchezaji mwenzake Andre Schuerrle akipongezwa na rais Joachim Gauck.

Ushindi mtamu

Ujerumani sasa imeshinda Kombe la Dunia mara nne, na kulifanya taifa hilo kubwa duniani kuwa nyuma tu ya Brazil yenye rikodi ya ushindi mara tano. Muda wa maamuzi wa fainali hiyo iliyojawa na msisimko na magoli yaliyofungwa kwa ustadi mkubwa ulikuja wakati timu hizo zikinyemelewa na mikwaju ya penalti mbele ya watazamaji 74,738 katika uwanja maarufu wa Maracana, mjini Rio de Janeiro.

Mchezaji bora wa mechi hiyo ya fainali, Goetze, aliituliza kifuani krosi ya Andre Schuerrle na bila kufanya ajizi akasukuma mkwaju uliomduwaza mlinda mlango wa Argentina Sergio Romero, kwa goli la ushindi lililomfanya nahodha Philip Lahm kubeba Kombe la Dunia.

"Siamini kama sisi ndiyo mabingwa wa dunia. Suala la iwapo tuna mchezaji bora mmoja mmoja halijalishi hata kidogo, kilichomuhimu ni kuwa na timu bora. Tumekuwa tukiboresha mchezo wetu wakati wote wa mashindano, na hatukukata tamaa pale mambo yalipotuendea vibaya, tuliendelea kushika njia yetu, na mwishowe tumesimama hapa kama mabingwa wa dunia. Ni hisia isiyoelezeka," alisema Lahm

Baada ya kosa kosa za miaka mingi

Ujerumani ambayo iliinyeshea Brazil mvua ya magoli 7 -1 katika mchezo wa nusu fainali, imekuwa timu ya kwanza ya Ulaya kubeba Kombe la Dunia katika Amerika ya Kusini. Walianza kushinda taji hilo mwaka 1954 na kulirudia mwaka 1974 na 1990. Wamekuwa wakilikosakosa ama kwa kutolewa kwenye hatua ya nusu fainali au fainali katika miaka ya hivi karibuni.

Kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani Joachim Loew (Jogi).

Kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani Joachim Loew (Jogi).

Taji hilo ni matokeo ya mabadiliko katika mfumo mzima wa soka ya Ujerumani mwanzoni mwa karne hii, na kutawazwa jina la "kizazi cha dhahabu" kikiongozwa na Lahm na Bastian Schweinsteiger.

"Ninaamini kazi hii ilianza tangu miaka 10 iliyopita na Juergen Klinsman na sisi tulifanya kuendeleza kile alichokianzisha. Tumefanya kila kitu kuhakisha tunafika siku hii. Timu yetu imefanya kazi kubwa sana, imekuwa na hamasa kubwa na hasa katika wiki hii ya mwisho, kila mchezaji amejituma na ndiyo maana tumeweza kushinda fainali hii hapa," alisema kocha wa timu hiyo ya taifa, Joachim Loew.

Kina Messi wajilaumu wenyewe

Argentina ambao walishinda taji hilo mwaka 1978 na 1986 kwa kuifunga Ujerumani, wamemaliza wakiwa washindi wa pili kama ilivyokuwa mwaka 1930 na 1990, na nyota wao, Lionel Messi, hakucheza kama alivyotarajiwa. Kiungo wa kati, Javier Mascherano, alisema ni vigumu kueleza, kwani walifanya kila kitu kushinda na walikuwa na nafasi nzuri zaidi.

Messi, Gonzalo Higuain na Rodrigo Palacio walikosa nafasi nzuri wakati kichwa cha Benedikt Hoewedes kiligonga mwamba kwa upande wa Ujerumani mbele ya maefu ya mashabiki wakiwemo Rais Joachim Gauck na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani, Rais Vladmir Putin wa Urusi na mwenyeji wao Rais Dilma Roussef wa Brazil.

Lionel Messi akisononeka baada ya kupulizwa kwa firimbi ya mwisho.

Lionel Messi akisononeka baada ya kupulizwa kwa firimbi ya mwisho.

Upinzani usiotarajiwa

Ujerumani ilimiliki mpira kwa sehemu kubwa kama ilivyotarajiwa huku mashabiki wake wakiipa morali ya nyimbo za "ole", lakini Argentina ilionyesha upinzani mkali tofauti na ilivyokuwa katika mchezoi wa nusu fainali na Uholanzi. Tofauti na robo fainali dhidi ya Ufaransa, na nusu fainali dhidi ya Brazil, Ujerumani ilishindwa kupata goli la mapema dhidi ya safu imara ya ulinzi ya Argentina, ambayo ilikuwa haijafungwa katika michezo mitatu ya mwisho ya mtoano, na ilikuwa na haiba tofauti na Brazil.

Wakiwa wamebeba kombe mikononi mwao, wachezaji wa Ujerumani waliimba pamoja na mashabiki wao, wimbo maarufu wa "Am Tag Wie Diesen" (Katika Siku Kama Hii) uliyopigwa na bendi ya Ujerumani ya Die Toten Hosen na kuchezwa uwanjani. Ilikuwa ndoto iliyotimia baada ya subira ya miaka mingi.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/dpae,afpe
Mhariri: Bruce Amani

DW inapendekeza

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com