Wamalawi waendelea kusubiri | Matukio ya Afrika | DW | 27.05.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Wamalawi waendelea kusubiri

Tume ya uchaguzi ya Malawi inaendelea na zoezi la kuhesabu upya kura, katika jitihada za kuonyesha kuwa nchi hiyo inaweza kuutatua mgogoro mkubwa wa kisiasa kwa kufuata katiba ili kunusuru demokrasia yake changa.

Malawi Präsidentin Joyce Banda

Rais Joyce Banda

Tangu kufanyika kwa uchaguzi huo uliogubikwa na machafuko wiki iliyopita, rais wa sasa Joyce Banda amejaribu kuibatilisha kura hiyo, lakini jitihada zake ziligonga mwamba mbele ya mahakama.

Rais Banda anadai kuwa kura hiyo iligubikwa na mapungufu makubwa, na kutaka uitishwe uchaguzi mpya ndani ya siku 90, akisema kuwa hatashiriki uchaguzi huo mpya. Lakini haikuwa bayana iwapo anayo mamlaka ya kikatiba kuchukua hatua kama hiyo, na mahakama iliamuru zoezi la kuhesabu kura liendelee.

Wapigakura walivyopanga foreni kutumia haki ya kikatiba kuchagua viongozi.

Wapigakura walivyopanga foreni kutumia haki ya kikatiba kuchagua viongozi.

Uhakiki kura kuchukuwa siku 30

Mkuu wa tume ya uchaguzi Maxon Mbedera aliwataka Wamalawi jana kuwa watulivu, na kuongeza kuwa zoezi la uhakiki wa kura litachukuwa hadi siku 30.

Mbendera alisema asilimia 95 ya matokeo yalikuwa tayari yamerikodiwa na karibu malalamiko 100 kati ya 275 yaliyopokelewa ilikuwa lazima yashughulikiwe.

Katika baadhi ya maeneo, idadi ya kura zilizopigwa inaripotiwa kuwa kubwa kuliko idadi ya wapiga kura wenyewe. Mbendera alisema matokeo kutoka vituo vinavyolalamikiwa yametengwa na wanayakagua kwa umakini kuangalia kasoro zilizopo.

Kiongozi wa upinzani Peter Mutharika, ambaye siku ya Ijumaa baada ya theluthi moja ya kura kuhesabiwa alikuwa anaongoza kwa asilimia 42 ya matokeo yasiyo rasmi, alipinga kuhesabiwa upya kwa kura, na kumuelezea rais Banda kama mfa maji.

"Kwanza kabisaa alitaka kura zehesabiwe kwa mkono, nafahamu, na sasa amebadilisha kwa kutaka kufuta uchaguzi kama unavyojua chama chake cha PP kinataka kuwapiga watu mitaani, sijui kwa nini na sioni haja ya maandamano, kwanza waandamana dhidi ya nani?," alisema bwana Mutharika.

Siku ya Jumamosi Mutharika aliepuka kujitangazia ushindi lakini alidai kuwa umma umezungumza na kwamba uchaguzi huo ulikuwa wa haki na wa kuaminika.

Wafuasi wa Banda kwa upande mwingine, wanaamini uchaguzi huu haukuwa wa haki, na wanahofu kuwa ndugu huyo wa marehemu rais Bingu Mutharika anaweza kuwa anajaribu kupora madaraka.

Mpinzani mkuu wa Banda, Peter Mutharika (k) akiwasalimia wafuasi wake.

Mpinzani mkuu wa Banda, Peter Mutharika (k) akiwasalimia wafuasi wake.

Taasisi za serikali zasifiwa

Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya na Marekani zimetoa wito wa kuwepo na utulivu. Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani Marie Harf alisema katika taarifa kuwa Marekani inaungana na jamii ya kimataifa kutoa wito wa utulivu wakati ambapo tume ya uchaguzi ya Malawi ikiendelea kuhakiki kura na kutatua changamototo zozote na malalamiko.

Wachambuzi wameisifu tume ya uchaguzi ya Malawi na taasisi nyingine kwa namna zilivyoshughulikia mgogoro huo, ambao unaweza kuwa ndiyo mkubwa zaidi tangu nchi hiyo ilipopata uhuru wake mwaka 1963.

Mwangalizi kutoka kituo cha Sheira na haki za binaadamu cha Robert F. Kennedy chenye makao yake mjini Washington, Jeffrey Smith, alisema licha ya changamoto na wasiwasi uliyojitokeza, Malawi imeonyesha tena kwamba ina taasisi imara, zinazoheshimika na zisizoegemea upande.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe
Mhariri: Josephat Charo

DW inapendekeza